Sunday, June 22, 2025
spot_img

TANZANIA KUNUFAIKA NA DOLA MILIONI 100 ZA MFUKO WA UWEKEZAJI WA JAPAN

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa mkutano baina yake na timu ya Afrika ya Japan Association of Corporate Executives, uliofanyika jijini Tokyo Japan (Picha kwa hisani ya Ofisi ya Waziri Mkuu) 


*Ni za kukuza uchumi, ziliahidiwa katika Mkutano wa TICAD 8, Tunisia

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

TPKYO, JAPAN

TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Afrika zitakazonufaika na fedha za mfuko wa kukuza uwekezaji barani Afrika kutoka Serikali ya Japan zitakazotolewa kuanzia Machi, 2023.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa timu ya Afrika ya Japan Association of Corporate Executives (KEIZA DOYUKA) Mutsuo Iwai wakati akizungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Marunouchi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, Japan.

Alisema ifikapo Disemba mwaka huu, kampuni ya kusimamia mfuko huu wa uwekezaji wenye manufaa barani Afrika itazinduliwa na utekelezaji utaanza Machi, 2023.

“Tunataraji ifikapo Machi, 2024 tutakuwa tumetoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 100 kwa kampuni za vijana wanaochipukia ili kuwajengea ubia, kujifunza teknolojia mpya na kubadilishana ujuzi,” amesema Iwai.

Amesema fedha hizo za uwekezaji kwenye mitaji (start-ups) zimelenga kukuza biashara ambazo zitatatua changamoto za kijamii zikiwemo sekta za afya, kilimo, nishati na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Utolewaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida aliyoitoa Agosti 27, 2022 wakati akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) uliofanyika jijini Tunis, nchini Tunisia.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wakubwa wa Japan leo. (Picha kwa hisani ya ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu Kishida amesema Japan imelenga kukuza uwekezaji ambapo safari hii wamelenga kuwainua vijana wanaoanzisha makampuni kwani hatua hiyo itawapa fursa vijana wa Afrika na wa Japan kufanya kazi kwa karibu.

KEIZAI DOYUKAI ni taasisi binafsi iliyoanzishwa Aprili 30, 1946 yenye wanachama wapatao 1,500 ambao ni watendaji wakuu na wamiliki wa makampuni makubwa ya Japan wanaojihusisha na utoaji suluhisho kwa masuala ya kisera yanayohusu maendeleo ya nchi yao na dunia kwa ujumla.

Waziri Mkuu pia amekutana na wawakilishi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Japan (KEIDANREN) ofisini kwao Otemachi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, ambako mwenyekiti wa kamati ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Hajime Kawamura amemweleza jinsi shirikisho lao linavyojihusisha na miradi ya maji, barabara, nishati, mawasiliano, utengezaji wa kemikali na ununuzi wa mazao.

Wawakilishi wa kamati hiyo wanaotoka makampuni ya Sumitomo, Marubeni, Toshiba, Komatsu na Mitsubishi wamemweleza Waziri Mkuu nia yao ya kuwekeza kwenye miradi ya nishati ikiwemo uzalishaji wa umeme kwa kutumia jotoardhi, usambazaji wa umeme, usambazaji wa gesi (LPG), huduma za mawasiliano na TEHAMA.

KEIDANREN (Japan Business Federation) jumuiya ya kiuchumi iliyoanzishwa Agosti 16, 1946 yenye wanachama 1,494 ambao ni wawakilishi wa makampuni ya Kijapani, ina vyama 108 vya wenye viwanda na taasisi 47 za kiuchumi kutoka mikoa yote.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amewaeleza wafanyabiashara wa makundi yote mawili kwamba Serikali ya awamu ya sita iko tayari kufanya kazi na wawekezaji na ndiyo maana iliamua kuboresha miundombinu ili kurahisha upatikanaji wa huduma muhimu.

“Utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, utulivu na amani vilivyopo nchini, hali nzuri ya hewa, ujenzi wa bandari, reli na barabara, umeme na maji unawahakikishia wawekezaji uhakika wa mitaji pindi mnapoamua kuwekeza nchini Tanzania,” amesema.

Waziri Mkuu amewahamasisha waje nchini kuwekeza kwenye sekta ya utalii ikiwemo ujenzi wa hoteli za nyota tano na kuanzisha michezo ya majini kwenye fukwe za bahari Zanzibar na Bara. 

“Pia angalieni uwezekano wa kuwekeza kwenye kilimo cha mashamba makubwa  na ujenzi wa viwanda. Lengo la Serikali hii ni kuendelea kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali  ikiwemo viwanda,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikutana na Rais wa Taasisi ya Zimamoto ya Japan, Kamishna Akimoto Toshifumi na kujadiliana uwezekano wa taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa askari wa jeshi la uokoaji na zimamoto nchini.

Mikutano hiyo yote ilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika MasharikiBalozi Mbarouk Nassoro Mbarouk na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda.

 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya