Tuesday, December 24, 2024
spot_img

WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS SAMIA MAZISHI YA ABE



RIPOTA WA WAZIRI MKUU

TOKYO, JAPAN

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameungana na wakuu wa nchi na viongozi 700 kutoka nchi 195 na mashirika ya kimataifa 23 kuweka mashada kwenye mazishi ya kitaifa ya Waziri Mkuu mstaafu wa Japan, Shinzo Abe.

Waziri Mkuu ambaye yuko Tokyo, Japan akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, alitoa heshima hizo za mwisho Jumanne, Septemba 27, 2022 kwenye ukumbi wa Nippon Budokan akiwa ameambatana na mkewe, Mary Majaliwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika MasharikiBalozi Mbarouk Nassoro Mbarouk, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda na mkewe Consolata Luvanda.

Baada ya kutoa heshima za mwisho, Waziri Mkuu alikwenda kwenye Kasri la Kifalme la Akasaka, jijini Tokyo ambako hufanyika shughuli zote za kiserikali ili kumfariji Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Fumio Kishida pamoja na mjane wa Shinzo Abe, Bibi Akie Abe. Alikuwa miongoni mwa viongozi wengine wa kitaifa 40 ambao walipata fursa hiyo.

Viongozi wengine wa kitaifa walioshiriki mazishi hayo ni Marais kutoka Vietnam, Sri Lanka, Makamu wa Rais wa Indonesia, Marekani, Ufilipino, marais wastaafu wa Ufaransa, Ujerumani na Mfalme wa Falme za Kiarabu, mtawala wa Qatar na Amiri wa Kuwait. Mawaziri Wakuu 16 walihudhuria mazishi hayo.

Miongoni mwa mawaziri wakuu waliokuwepo ni Narendra Modi wa India, Justin Trudeau wa Canada, Han Duck-soo wa Korea Kusini na Antony Albanese wa Australia. Wengine ni Mawaziri Wakuu wastaafu, Maspika, Majaji, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mabalozi. Baadhi ya nchi na taasisi zilizowasilisha salamu za rambirambi, zilisomwa majina yao.  

Mapema asubuhi, wakazi wa Japan walijipanga kwenye misururu mirefu ili kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa kuweka mashada ya maua kwenye eneo maalum lililoandaliwa katika bustani nje ya ukumbi huo. Ukumbini kulikuwa na watu wapatao 4,300.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya