RIPOTA WA WAZIRI MKUU
TOKYO, JAPAN
Akiwasilisha salamu hizo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema: “Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatoa pole nyingi kwako, kwa familia ya wafiwa na kwa wananchi wa Japan kutokana na msiba huo.”
Katika mazungumzo yao, mbali na kutoa pole, Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kusisitiza uwepo wa uhusiano mzuri baina ya Tanzania na Japan na kumuahidi nia thabiti ya Serikali ya awamu ya sita ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
Vilevile, Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kukumbushia masuala ambayo walijadiliana kwa njia ya mitandao wakati akiwa Tunisia kwenye mkutano wa TICAD 8 hasa utekelezaji wa miradi ya zamani ambayo Tanzania iliiwasilisha kwenye mkutano wa TICAD 7 inayohusisha ujenzi wa Bandari ya Kigoma, mradi wa maji wa Zanzibar na ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha hadi Holili mkoani Kilimanjaro.
“Nimemshukuru Waziri Mkuu wa Japan kwa ahadi yake kuwa wanafuatilia pia maombi ya miradi minane ambayo tuliiwasilisha kwenye mkutano wa TICAD 8 na majadiliano yameanza huko nyumbani.”
Miradi hiyo ni ya ukarabati wa barabara ya Morogoro-Dodoma kwa kiwango cha lami, mradi wa umwagiliaji katika Bonde la Ziwa Victoria, mradi wa kusambaza maji Lugoda (Mufindi), kujenga uwezo wa kituo cha utafiti cha ufugaji wa samaki Dar es Salaam, bandari ya kisasa ya uvuvi, kuanzisha maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi na ukarabati wa bandari ya uvuvi ya Wete na ujenzi wa njia ya umeme ya Somanga-Fungu-Mkuranga.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amesema watatekeleza ahadi yao ya kuzisaidia nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo ili zijitegemee kwa chakula. “Amesema kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) watatoa Dola za Marekani milioni 300 ili kuzisaidia nchi za Afrika zizalishe chakula kwa wingi na kukabiliana na upungufu wa chakula uliojitokeza baada ya kuzuka kwa vita baina ya Urusi na Ukraine.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na ujumbe wake akiwasilisha salama za pole kwa Waziri Mkuu wa Japan Fumo Kishida |
“Kwenye elimu, nimemuomba Waziri Mkuu Kishida aangalie uwezekano wa vijana wetu wa digrii ya kwanza waweze kupata fursa ya kuja Japan kusomea fani za udaktari, ICT, kwani hivi sasa wanachukua wanafunzi wa Master’s na PhD tu. Tunahitaji wanaosomea digrii nao wapate fursa kama hiyo,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kesho (Jumanne, Septemba 27, 2022) Waziri Mkuu atashiriki mazishi ya Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Shinzo Abe kwa kutoa heshima za mwisho kwenye ukumbi wa Nippon Budokan.