Tuesday, December 24, 2024
spot_img

SHULE YA SEKONDARI GOLDEN YALIZA WAZAZI, AFISA ELIMU DAR AWATAKA KWENDA KORTIN

Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Abdul Maulidi



RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

UONGOZI wa Shule ya Sekondari ya Golden iliyopo Chanika, Dar es Salaam unadaiwa kukiuka maagizo ya Serikali ya kutowachuja na kuwaondoa shuleni wanafunzi ambao wastani wao kimasomo hauridhishi na kuwapeleka nje ya shule hiyo kwenda  kufanya mitihani.

Inadaiwa licha ya wazazi na walezi kulipa ada yote katika shule hiyo, kinapofika kipindi cha kufanya mitihani ya NECTA, wanafunzi ambao wastani wao hauridhishi huondolewa shuleni na kusafirishwa kwenda kufanya mitihani yao katika shule iliyokodishwa na mmiliki wa shule ya Golden kwa mpango mkakati wenye lengo la kuonyesha shule yake inafanya vizuri, waliyoitaja kwa jina la Kafurusu iliyoko Kibaha mkoani Pwani.

Madai hayo yametolewa hivi karibuni na baadhi ya wazazi ambao wamewaandikisha watoto wao kusoma katika shule hiyo kabla ya kuondolewa bila wao kutaarifiwa na kupelekwa shule nyingine.

Wakizungumza kwa sharti la majina yao kuhifadhiwa kwa kile walichodai iwapo itafahamika kuwa wanaushutumu uongozi wa shule hiyo kwa kukiuka maagozi wa Serikali, usalama wa watoto wao unaweza kuwa shakani, walisema uongozi wa shule hiyo umekuwa ukiwachuja na kuwaondoa shuleni hapo wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne ambao hawafikishi wastani wa kimkakati wa ufaulu wa shule hiyo.

Mmoja wa wazazi ambaye alimwandikisha mtoto wake katika shule hiyo lakini sasa ameondolewa shuleni hapo na kupelekwa shule nyingine bila ridhaa yake, amesema alimpeleka mtoto wake katika shule hiyo kwa sababu aliamini ina ubora unaoridhisha kutokana na kuwa na matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa na kulipa gharama zote zilizohitajika lakini sasa mwanae amepelekwa shule nyingine aliyodai mazingira yake siyo rafiki kwa mwanafunzi kusoma na kwamba hakutaarifiwa kuhusu kuondolewa kwa mtoto wake shuleni hapo.

“Shule ya Golden mimi niliona matangazo yake, nilipoifuatilia nilibaini watoto wanaosoma hapo wanapata kiwango kizuri cha ufaulu na shule yenyewe imekuwa kwenye shule ambazo zinafanya vizuri kitaifa. Nikampeleka mwanangu hapo na nikalipa ada na gharama nyingine zote, ajabu aliporudi likizo nikabaini kuwa hasomi tena hapo bali aliondolewa na kupelekwa shule nyingine iliyoko huko Kibaha ambayo kwa kweli siyo shule nzuri na mimi sikutaka mwanangu akasome huko.

“Nilipofuatilia jambo hilo linakuwaje pamoja na wazazi wengine waliopeleka watoto wao hapo shuleni tukabaini kuwa uongozi wa hiyo shule huwa unapokea watoto wengi sana ambao wazazi wao hulipa gharama zote za shule hiyo kisha wanawachuja watoto, unapofika muda wa kufanya mitihani wenye wastani mdogo wanawaondoa wanapeleka kuna shule moja huko Kibaha Madafu inaitwa Kafurusu, wanafanyia mitihani huko.

“Na hii hasa hasa ni kwa watoto wa kidato cha pili na cha nne na huwa wanafanya hivi kuwabakiza wenye wastani wa juu ili shule yao iwe na matokeo mazuri kwa sababu wenye ufaulu mdogo wote huwa wanaondolewa.

“Lakini pia tukabaini kuwa hili huwa linaanza kipindi cha usaili wa kuingia kidato cha kwnza ambapo wazazi ambao hukimbilia Shule ya Sekondari ya Golden, mmiliki wa shule huwa anaongea na wazazi kuwa walipe ada na gharama nyingine katika shule hiyo, ambazo ziko juu na yeye atawafutia shule nzuri lakini matokeo yake huwa anapeleka kwenye hiyo Shule ya Kafurusu ambayo tumebaini kuwa ameikodisha kutoka kwa mzee mmoja ambaye sasa ni marehemu na ni maalumu kwa ajili ya kupeleka huko watoto ambao hawana wastani wa juu katika masomo,” alisema mzazi huyo.

Mmiliki wa Shule ya Sekondari ya Golden, Rose Mshumba



Alipoulizwa mmiliki shule hiyo, Rose Mshumba kuhusu madai hayo alisema majibu ya maswali anayoulizwa kuhusu malalamiko ya wazazi anayo Kamishna wa Elimu. “Hao wazazi kwanini wamekuja kulalamika kwako. Mimi nina shule mbili wewe unazungumzia shule gani? Sikiliza nenda kamuulize Kamishna wa Elimu atakujibu kwanini shule yangu huwa inawaondoa hao watoto kwenye,” kisha akakata simu.

Alipoulizwa Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Abul Maulidi alisema mwongozo wa elimu unaelekeza darasa moja kuwa na wanafunzi wasiopungua 35 na kwamba kama shule haijakidhi vigezo kwa wanafunzi kufanya mitihani ya kitaifa huwa  inaandika barua na kuruhusiwa wanafunzi wake kwenda shule nyingine kufanya mtihani.

“Baraza la mitihani wameruhusu na hakuna sheria inayobana mmiliki wa shule kuondoa wanafunzi walioandikishwa kwenye shule yake kuwapeleka shule nyingine kufanya mitihani yao. Wanafunzi hao huwa wamehamishwa kwa sababu ili mwanafunzi afanye mtihani wa Taifa ni lazima awe amesajiliwa, kwa hiyo hao huwa wamesajiliwa katika shule wanazofanya mitihani.

“Makubaliano ya kumuhamisha mwanafunzi ni baina ya mzazi na shule anayosoma na anakompeleka mwanae kwenda kusoma, sasa kama kuna shule ambazo zinawafanyia wazazi mambo yasiyofaa kwa kuchukua fedha zao kisha wanawapeleka watoto mahali ambako wazazi wao hawajui na kusikolingana na gharama walizotoa, wazazi wanapaswa kushtaki, waende mahakamani,” alisema.

Kauli hii ya Alhaj Maulid inakinzana na kauli yake ya awali akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya 19 kwenye Shule ya Sekondari ya St, Anne Mariae Academy iliyopo Kimara, Dar es Salaam ambako alisema ni marufuku kwa shule kuchuja wanafunzi wasiofikia kiwango na ama kuwazuia kufanya mitihani ya kitaifa wanafunzi ambao wazazi wao hawajakamilisha kulipa ada.

Jitihada za kumfikia Waziri wa Elimu kuzungumzia suala hili zinaendelea.    

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

1 COMMENT

  1. Kuna kuchuja wanafunzi, na kuna kuhamisha wanafunzi. Kauli za Afisa Elimu wa Mkoa ni sahihi, kwa sababu amezungumzia mambo mawili tofauti. Mnatakiwa kwanza mthibitishe sababu za watoto kuhamisha, ni uchujwaji au kuna sababu zingine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya