Diwani Mutta Rwakatare akiwa katika moja ya matukio yasiyokuwa ya kawaida |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
IKIWA imepita miezi michache baada ya Meya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Songoro Mnyonge kutangaza kuwa Diwani wa Kawe, Mutta Robert Rwakatare hajulikani alipo na kuliomba Jeshi la Polisi lisaidie kumtafuta kabla ya kukutwa akiwa kwa Ashura, mkazi wa Tabata alikofika akiwa katika hali ya ulevi wa kipundukia, diwani huyo sasa anadaiwa kuingilia mahusiano ya watu na kufumaniwa akiwa na wake za watu.
Taarifa zilizopatikani kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zimedai kuwa Diwani Rwakatare amekuwa akiingilia mahusiano ya watu hususan vijana walio katika uchumba wanaosali kwenye makanisa ambayo pia yeye ni kiongozi wa kiroho na kwamba amepata kufumaniwa mara kadhaa akiwa na wake za watu.
Inadaiwa katika mafumanizi hayo, Diwani Rwakatare amekuwa akipewa adhabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kurushwa kichura, kufanyiwa vitendo visivyo na staha na kutozwa pesa.
“Kama kweli tunataka kulinda maadili yetu ni lazima tuchukue hatua, viongozi hawa inapaswa wawe wanachujwa kwa kuangaliwa tabia zao. Unapokuwa na kiongozi anayefumaniwa na wake za watu, anayeingilia mahusiano ya watu kwa sababu ya fedha zake, anayejihusisha na magenge yasiyofaa hapo hatuwezi kusema tunasimamia maadili.
“Huyu Mutta ana matukio mengi mno yasiyofaa. Ndiye kiongozi wetu. Sasa kama hana maadili hao anaowangoza wanaiga mfano gani kutoka kwake? Huyu kafumaniwa na mke wa mtu pale Kinondoni, tena akiwa ndani kwa mwanamke wakakutwa kama walivyozaliwa. Mwenye mke alikuwa na mabaunsa wawili, akarushwa kichura kweli humo na mambo mengine huko kisha akatakiwa atoe hela. Ushahidi upo. Hivi kiongozi kama huyu anaongoza nini na anaipeleka wapi jamii anayoiongoza?” alisema mmoja wa watoa taarifa.
Diwani Mutta Rwakatare akiwa katika moja ya matukio yasiyokuwa ya kawaida |
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta mara nyingi Diwani Rwakatare kuzungumzia tuhuma zinazoelekezwa kwake lakini kila anapopatikana na kuulizwa husema yupo kwenye kikao apigiwe badaaye na akipigiwa tena hapokei simu.
Mei mwaka huu, Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyomge akiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani aliviomba vyombo vya dola na wanahabari kusaidia kumtafuta diwani huyo ambaye ni mtoto wa marehemu Dk. Getrude Rwakatare.
Siku chache baada ya ombi hilo la Meya Mnyonge, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, Jumanne Muliro alisema polisi wamefanikiwa kumpata Diwani Rwakatare maeneo ya Tabata akiwa nyumbani kwa Ashura ambako alifika akiwa katika hali ya ulevi wa kupindukia.
Mapema Mwezi Machi, Tanzania PANORAMA iliripoti kuwa kuna wasiwasi wa mahali alipo na hali ya afya ya Diwani Rwakatare.
PANORAMA iliripoti kuwa watu wake wa karibu wanadai haijulikani alipo na Tanzania PANORAMA Blog ilimtafuta bila mafanikio.
Hata hivyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge alipoulizwa kuhusu hilo alisema Diwani Mutta yupo na mara ya mwisho aliongea naye Machi 6, 2021 majira saa 7.30 mchana.
Meya Mnyonge aliombwa na Tanzania PANORAMA Blog kuiwezesha kumfikia au kuwasiliana naye kwa njia ya simu na aliahidi kufanya hivyo lakini hakutekeleza hilo licha ya kukumbushwa na kuelezwa sababu za msingi za PANORAMA Blog kumtafuta diwani huyo.
Diwani Mutta na ndugu zake watatu wanatuhumiwa na kaka yao, Tibe Kenneth Rwakatare kughushi nyaraka za mauzo ya kiwanja namba 259 kilichopo eneo la Udindifu Bagamoyo pamoja na kukwepa kulipa kodi ya Serikali.
Tibe alipoulizwa hivi karibuni kuhusu alipo mdogo wake Mutta alisema hana taarifa zake na kwamba yeye yupo Dodoma kwa shughuli zake.
Tanzania PANORAMA Blog ilifika mara kadhaa katika ofisi za Diwani Mutta zilizopo eneo la Afrika Sana, Mwenge na mara zote ilikuwa ikielezwa kuwa hayupo na haijulikani alipo.
Baadhi ya watumishi katika Ofisi ya Kata ya Kawe ambako PANORAMA Blog ilifika kumtafuta Diwani Mutta walieleza kuwa hajaonekana kwa muda mrefu.
Mmoja wa viongozi wa kata hiyo aliyezungumza na PANORAMA Blog kwa ombi la kihifadhiwa jina lake alisema katika kipindi cha mwezi mmoja hajapata kuonana naye isipokuwa siku moja alipewa taarifa kuwa diwani huyo alifika ofisini hapo kumuulizia.
“Nina zaidi ya mwezi mmoja sijamuona mimi, ila siku moja nilikuwa kwenye kazi za nje niliporudi nikaambiwa kuwa diwani alipita hapa kukuulizia, kwa hiyo nilipishana naye.
“Ofisi yake hiyo hapo imefungwa tu siku zote ila hapa huwa anapaswa kuwepo siku za Jumanne na Alhamis. Bosi wake ni Meya na Mkurugenzi na hata posho zake analipwa huko, mkimuuliza Meya wa Kinondoni atakuwa anajua yupo wapi na kama kuna jingine kumhusu yeye anajua,” alisema afisa huyo.
PANORAMA Blog ilijaribu mara kadhaa kumtafuta kwa simu yake ya kiganjani bila mafanikio na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake hakupata kujibu.
Taarifa zilizopo zinadai kuwa Diwani Mutta amekuwa akipotea mara kwa mara ikiwa haijulikani mahali anakokwenda na anaporejea huwa katika hali isiyokuwa ya kawaida.