Tuesday, December 24, 2024
spot_img

MAJALIWA ATETA NA FUMIO KISHIDA, AISHUKURU SERIKALI YA JAPAN


RIPOTA WA WAZIRI MKUU

TUNIS TUNISIA 

 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemshukuru Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida kwa misaada ambayo nchi yake inaipatia Tanzania ili kuleta unafuu kwenye maisha ya wananchi wake.

 

Wakizungumza kwa njia ya mitandao mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Palais des Congres, jijini Tunis, Tunisia ulikokuwa ukifanyika mkutano wa nane wa wakuu wa nchi na Serikali wa TICAD ambako Kishida alishindwa kuhudhuria kwa sababu ya maambukizi ya UVIKO 19, Majaliwa aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania kuwainua wananchi kiuchumi.

 

“Tanzania tunaishukuru sana Serikali ya Japan kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwakwamua wananchi wake kiuchumi na kuwezesha ujenzi wa miundombinu hadi vijijini,” alisema Majaliwa.

 

Majaliwa ambaye anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo alimweleza Waziri Mkuu wa Japan huyo kwamba Tanzania bado inaomboleza na wananchi wa Japan kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Shinzo Abe na akatumia fursa hiyo kutoa pole.

 

Akigusia miradi ambayo Serikali ya Japan imeisaidia Tanzania, Majaliwa alisema: “Iko miradi mingi ambayo imetekelezwa na Japan kupitia taasisi ya JICA, wako wawekezaji wanafanya biashara nasi na pia yako makampuni ambayo yamejitoa kusaidia sekta muhimu,” alisema.

 

Aidha, alitumia fursa hiyo kuiomba Japan ikamilishe ahadi yake ya kutekelza miradi iliyoiahidi kwenye mkutano wa TICAD 7 ambayo inahusu ujenzi wa barabara ya Arusha mpaka Holili mkoani Kilimanjaro, mradi wa maji wa Zanzibar, ujenzi wa Bandari ya Kigoma na Bandari ya Uvuvi Zanzibar.

 

Kwa upande wake Kashida, alimtumia salamu Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote na akataka uhusiano wa nchi hizo mbili kupitia taasisi yao ya JICA uendelee kudumu.

 

Mapema, akitoa tamko kwa niaba ya Rais Samia kwenye mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali, Majaliwa alisema Bara la Afrika linakabiliwa na matatizo ya kiuchumi ambayo kwa kiasi kikubwa chimbuk lake ni UVIKO 19.

 

“Nimewaeleza madhara ya UVIKO 19 ambayo yanaikumba Afrika; Tanzania ikiwemo, matatizo ya vita ya Ukraine na Urusi ambavyo vimesababisha bei za bidhaa nyingi kupanda. Nimewaambia uko umuhimu wa mataifa makubwa ya G20 kuungana na Japan ambayo ni ya tatu kwa ukubwa kiuchumi ili kuzisaidia Nchi za Afrika,” alisema.

 

Alisema iko haja ya kuziwezesha Nchi za Afrika kujitegemea ili ziweze kuwasaidia wananchi wake kupata fursa za elimu, kujenga uwezo wa shughuli za kilimo na utalii ili ziweze kukuza uchumi wake.

 

Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Rais Tunisia, Kais Saied ambapo Rais wa Senegal, Macky Sall alitoa hotuba ya ufunguzi na Waziri Mkuu wa Japan, Kishida Fumio akahutubia kwa njia ya mitandao kutokea Japan.

 

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo wa unatarajiwa kukubaliana kuhusu namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063).

 

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na Nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya