Serengeti Girls |
*Ni kwa ajili ya timu za Serengeti Girls na Tembo Warriors
RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WADAU wa michezo wamechanga jumla ya Shilingi bilioni 1.26 wakiitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuzisaidia timu za Serengeti Girls na Tembo Warriors ambazo zinafuzu kushiriki michuano ya kimataifa huko India na Uturuki.
Akizungumza mara baada ya kupokea ahadi na michango ya wadau hao, leo usiku kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema michango waliyoitoa inaleta ujumbe kuwa wanataka makombe ya dunia yaje Tanzania.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
“Kikao hiki kimeitishwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mimi nimekiongoza kwa kushirikiana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Mchengerwa.”
Mbali ya michango ya fedha, wadau hao waliahidi kulipia tiketi za safari kwa timu zote mbili, kulipia bima kwa wachezaji wa timu zote mbili, kutengeneza na kuzibrand jezi na tracksuit, kununua viatu na soksi kwa wachzaji wa timu zote mbili.
Amewashukuru wadau wote kwa michango yao na kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuthamini michango waliyoitoa. Michango hiyo imetolewa na wadau kutoka sekta za fedha/mabenki, mitandao ya simu, viwanda, taasisi za Serikali, vyombo vya habari, wadau binafsi na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau hao, Waziri Mchengerwa alisema ili timu hizo zipate maandalizi ya kutosha zinahitajika shilingi bilioni 3.76 ili kugharimia timu zote mbili ambapo kati ya hizo, Serengeti Girls inahitaji sh. bilioni 2.57 na Tembo Warriors inahitaji sh. bilioni 1.19.
“Ili kujiandaa vizuri tumepanga kuzipeleka timu zote nje ya nchi kwa ajili ya kambi za mwisho kabla ya kuelekea kwenye mashindano hayo. Tumepanga kuipeleka timu yetu ya Serengeti Girls nchini Uingereza katika kambi ya timu ya Southampton na baadaye Dubai katika mashindano maalum.
“Vilevile, timu yetu ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu tutaipeleka Uturuki wiki mbili kabla ya mashindano ili kuipatia mafunzo na kuzoea hali ya hewa. Awali, timu hii tuliipeleka nchini Poland kwa ajili ya mashindano maalumu,” amesema.
Amesema timu ya soka ya watu wenye ulemavu ya Tembo Warriors ambayo tayari iko kambini inatarajiwa kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia Oktoba, mwaka huu na ile ya Serengeti Girls inatarajiwa kushiriki mashindano yake nchini India, Novemba mwaka huu.
Tembo Worrios |