Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC) Simon Maigwa |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
HATMA ya tuhuma zinazoikabili Kampuni ya Mafuta ya Oryx zinazochunguzwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro iko mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro (RPC) Simon Maigwa alipoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu hatua iliyofikiwa na jeshi hilo kuchunguza tuhuma inazoelekezewa kampuni hiyo na Mfanyabiasha Peter Kaale ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Community Petroleum Ltd.
Kaale amefungua shauri lenye tuhuma za jinai dhidi Kampuni ya Mafuta ya Oryx lenye RB namba KR/CID/PE/09/2022 akidai ilihusika katika tukio la kuvamiwa maeneo yake ya biashara, kuharibiwa mali, kuibiwa na kukiuka amri ya mahakama.
Katika majibu yake kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu baada ya kuulizwa majina ya watuhumiwa wa tukio hilo, iwapo wamekwishafikishwa mahakamani na mashtaka yanayowakabili, RPC Maigwa aliandika; ‘uchunguzi ukikamilika kaka jalada litapelekwa kwa NPs (Mkurugenzi wa Mashtaka) naye atalisoma ndiye aliyepewa jukumu la kuandaa mashtaka.’
Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa baadhi ya watuhumiwa wa makosa hayo ya jinai wameishakamatwa, alijibu; ‘Suala la uchunguzi ni suala la kitaalamu na wala siyo la kumfurahisha mtu kutaka majina ya watuhumiwa na ikaja kubainika hawakuhusika wanaweza fungulia chombo kilichotoa hiyo habari kila mtu anayo haki yake tusiharakishe jambo kwa manufaa ya nani uchunguzi ukikamilika kila kitu kitakuwa hewani asante.’
Mfanyabiashara Kaale anadai kuwa, April 24, 2019 maeneo yake ya biashara ambayo ni Kituo cha Mafuta kilichopo Barabara ya Taifa, Kituo cha Mafuta kilichopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na mgahawa wa kisasa unaofahamika kwa jina la Mekus Pub yalivamiwa na wanyanyua vitu vizito (mabaunsa), walinzi wa kampuni moja binafsi waliokuwa wamejihami kwa silaha za moto wakiongozwa na viongozi wa Kampuni ya Mafuta ya Oryx ambapo waliiba fedha, waliharibu mali na kuchoma moto nyaraka za kibiashara huku wakitishia kumpiga risasi mfanyakazi yoyote ambaye angekaidi amri yao.
Katika mahojiano aliyopata kuyafanya na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu madai yake hayo, Kaale alidai kuwa kampuni yake ya Community Petroleum Ltd ina mkataba na Kampuni ya Mafuta ya Oryx wa kuendesha vituo viwili vya mafuta vya KIA na kile kilichopo Barabara ya Taifa pamoja na Mgahawa wa Mekus Pub na madai yake yanaenda mbali zaidi kuwa vitendo hivyo vilitekelezwa huku kukiwa na amri ya zuio la kuingia maeneo yake ya biashara lililotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba la Moshi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Oryx, Kalpesh Mehta |
Kampuni ya Mafuta ya Oryx imethibitisha kukabiliwa na tuhuma hizo za makosa ya jinai na kuchunguzwa na polisi lakini ikikataa kuzizungumza kwa madai kuwa hatua hiyo ni kuingilia mwenendo wa upelelezi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Oryx, Kalpesh Mehta alieleza hayo katika barua yake ya Agosti 15, 2022 iliyokuwa ikijibu barua ya Tanzania PANORAMA Blog ya Mei 17, 2022 iliyobeba maswali kadhaa kwenda kwa kampuni hiyo ikiomba kupatiwa majibu na ufafanuzi dhidi ya tuhuma na madai mbalimbali ambayo kampuni hiyo na baadhi ya maofisa wake wamekuwa wakielekezewa na Mfanyabiashara Kaale.
Katika barua yake hiyo, Mehta alieleza kuwa kampuni anayoiongoza inafuata sheria na taratibu za nchi na pia inatunza maadili katika utekelezaji wa majukumu yake na hivyo kwa kutambua hilo haiwezi kutoa taarifa yoyote ambayo itaingilia mwenendo wa kesi ambazo zinaikabili mahakamani pamoja na tuhuma zinazochunguzwa na polisi.
Mehta alizitaja kesi hizo kuwa ni kesi ya madai namba 258 ya mwaka 2020, kesi ya madai namba 19 ya mwaka 2019 na kesi za madai namba 10 na namba 45 za mwaka 2021, ambazo zinaendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakama ya Wilaya Moshi na Mahakama ya Wilaya ya Hai, Bomang’ombe.
Alieleza kuwa Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kilimanjaro inaendelea na uchunguzi wa kesi ya madai yenye namba KR/C/PE/09/2022 inayoihusisha kampuni anayoiongoza hivyo kwa kutambua hayo, kampuni yake haipaswi kutoa taarifa yoyote wakati kesi zikiendelea.