Wednesday, December 25, 2024
spot_img

WAZIRI MKUU ATATUA MGOGORO WA ARDHI WA MIAKA MITATU KINONDONI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

RIPOTA WA WAZIRI MKUU 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka mitatu katika eneo la Boko-Dovya, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam baina ya Aloyce Mwasuka na Salutari Massawe.

Katika mgogoro huo unaohusisha viwanja namba 393, 395 na 370 kwenye kitalu G (Boko Dovya) vilivyoko njiapanda ya Mbweni, Massawe alijenga ukuta ambao ulikuwa unazuia matumizi ya barabara na hivyo kumfanya Mwasuka apitie kwa jirani yake Oliver Semuguruka (kiwanja na. 395) ili aweze kufika nyumbani kwake (kiwanja na. 393).

Akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, watendaji wa Wilaya ya Kinondoni katika kikao alichokiitisha Jumatano, Agosti 17, 2022 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na hatua aliyoichukua Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe ya kusimamia uvunjaji wa ukuta huo ili kupisha eneo la barabara.

“Ninakushukuru Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na timu yako kwa kuchukua hatua tangu jana ili kusimamia haki ya wananchi wasio na uwezo. Haki ni ya kila mmoja, mwenye uwezo na asiye na uwezo. Ile barabara iboreshwe ili wananchi wote wanufaike,” alisema.

Waziri Mkuu alisema hatua hiyo inaenda sambamba na utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyowapa wasaidizi wake akitaka wahakikishe kuwa wananchi hawapati shida kwenye maeneo yao.

Akisisitiza usimamizi wa majukumu yao kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri Mkuu alisema: “Nendeni mkasimamie masuala ya ardhi ili watendaji wa Serikali nao wafanye kazi nyingine za kuwahudumia wananchi. Lazima tufanye mifumo isimamiwe ili kazi nyingine ziendelee,” alisisitiza.

Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni alisema eneo hilo limeainishwa kwenye ramani ya mipango miji ya mwaka 2002 (TP 2002) na kwamba Massawe alinunua eneo hilo mwaka 2004 na akalipima mwaka 2005, wakati Mwasuka alinunua eneo lake mwaka 2005 na akalipima mwaka 2006.

“Katika upimaji wao kila mmoja alitumia mpimaji wake lakini coordinates zinaonesha kuwa kuna barabara katikati yao na ramani zao pia zinatambua barabara hiyo. Wote wawili walipaswa kuheshimu michoro ya mipango miji ambayo ni michoro mama,” alisema.

Naye Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam, Idrissa Kayera alimweleza Waziri Mkuu kwamba licha ya kuwa ramani zote mbili zimeitambua barabara hiyo yenye upana wa mita 12, Massawe aliamua kujenga ukuta upande mmoja tu katika eneo lake ambao uliziba eneo hilo la barabara na hivyo kufunga barabara inayotenganisha viwanja namba 393, 395, 370, 391,390 na 369.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwan Kikwete


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwan Kikwete alisema wizara itaendelea kusimamia migogoro yote iliyopo na kuweka mpango wa kuishughulikia.


Aloyce Mwasuka alimshukuru Waziri Mkuu, Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya na timu yao ya watendaji kwa kutatua migogoro huo na akaomba timu hizo mbili ziendelee kushirikiana ili kuwasaidia wananchi wengine wasio na sauti. Massawe hakufika kwenye kikao hicho kwa sababu ya changamoto ya kiafya.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya