Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa |
RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WAZIRI Muu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia tarehe 23 Agosti, ambayo ni siku ya sensa na makazi ya watu iwe ni siku ya mapumziko.
Akizungumza katika kikao cha saba cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kilichofanyika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, alisema Rais Samia ameridhia hilo ili Watanzania wawepo majumbani kuwapokea makarani wa sensa.
“Ninapenda kuwajulisha wajumbe wa kikao hiki kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia tarehe 23 Agosti iwe ni siku ya mapumziko ili Watanzania wawepo majumbani, waweze kuwapokea makarani wa sensa na kutoa maelezo husika,” amesema.
Alisema kutokana na uamuzi huo anaamini sensa ya watu na makazi itafanyika vizuri kama ilivyopangwa.
Mapema, Waziri Mkuu alipokea vishkwambi 600 kutoka kwa Balozi wa Korea Kusini, Kim Sun Pyo vyenye thamani ya shilingi milioni 202. Pia alipokea fulana 1,759 zenye ujumbe wa kuhamasisha sensa zenye thamani ya sh. milioni 20 kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Serikali wa Benki ya NMB, William Makoresho ambaye alikabidhi kwa niaba ya mtendaji mkuu wa benki hiyo.
Wajumbe wa kikao hicho walijulishwa kwamba utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebainisha kuwa uelewa wa wananchi kuhusu sensa umefikia asilimia 99 ikilinganishwa na asilimia 96 ya Juni, 2022.