Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa |
RIPOTA WA WAZIRI MKUU
0711 46 49 84
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema viongozi wa dini hawana budi kuendelea kuiombea amani Tanzania pamoja na viongozi wake kwa sababu bila amani makusanyiko ya kidini hayawezi kuwepo.
Akkzungumza leo katika Ofisi za Makao Makuu ya BAKWATA zilizopo Kinondoni Dar es Salaam kabla ya kukabidhi tuzo kwa mshindi wa kwanza wa kuhifadhi Quran barani Afrika katika mashindano yaliyofanyika kwenye msikiti wa Mfalme Mohammed VI ulioko Kinondoni, Waziri Mkuu Majaliwa alisisitiza viongozi wa dinni kuombea amani.
Akinukuu Quran tukufu sura ya pili, aya ya 126 (Quran 2:126), Waziri Mkuu Majaliwa amesema Nabii Ibrahim aliuombea mji wake na wakazi wake amani na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
“Nami nitoe rai kwa viongozi wetu wa dini, waendelea kuiombea nchi yetu na viongozi wake ili waendelee kuliongoza vema Taifa letu ikiwa ni pamoja na kujenga umoja na mshikamano, kudumisha amani na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu alisema kusanyiko hilo ni kielelezo cha utukufu wa Quran barani Afrika kwa sababu limejumuisha washiriki 88 kutoka nchi 34 barani Afrika.
Alisema katika zama hizi dunia inashuhudia kuongezeka kwa vitendo viovu ikiwemo watoto kuuwa wazazi wao, ulawiti, ubakaji hususani kwa watoto na wanafunzi, watoto na vijana kutowaheshimu watu wazima, uvaaji wa mavazi yasiyo na stara hususani kwa wasichana na wavulana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Alisema Quran inapaswa kuwa chanzo cha kutegemewa cha mafunzo sahihi ya tabia njema, utii na kuheshimu mamlaka zilizopo.
“Tukiwalea vijana wetu katika mafunzo haya tutakuwa tunamsaidia mlezi wetu namba moja Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaguswa na suala zima la maadili hususan kwa vijana kuwa na wasaidizi wacha Mungu na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa rai kwa viongozi wa dini kuhakikisha vijana wanaweza kuhifadhi Quran lakini pia wawe wamehitimu katika fani mbalimbali.
“Kijana akihitimu fani yake siyo rahisi kumuona akienda kinyume na maadili ya taaluma yake. Kwa hiyo Quran ni mchunga wa nafsi ya mtaalamu huyo na hivyo kumfanya aonyeke dhidi ya kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na uadilifu,“ alisema Waziri Mkuu.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo ya kutoa tuzo kwa washindi, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir alimshukuru Mfalme wa VI wa Morocco ambaye Taasisi yake ya Ulamaa Afrika ndiyo iliyofadhuli mashindano hayo na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mfalme wa Morocco Ulamaa Afrika, Mohammed Rifqiy kwa kuamua kuleta mashindano hayo Afrika Mashariki.
“Uamuzi wao wa kuleta mashindano haya umetuwezesha kuona jinsi Quran ilivyokuwa inaandikwa kwa mkono hadi kufikia hatua ya sasa ya kuchapisha. Wenzetu wa Afrika Magharibi wamezoea kuyaona haya,” alisema.
Miongoni mwa washindi waliotia fora ni binti wa miaka 14, Saima Hassan Suleiman wa Dar es Salaam ambaye aliibuka mshindi wa kwanza katika kundi la pili la kusoma Quran na kuhifadhi juzuu 30.
Saima ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert ya jijini Dar es Salaam, alisema amekuwa akijifunza Quran tangu alipokuwa na miaka mitano. Kundi hilo lilikuwa na washindi wawili wa Tanzania akiwemo Ahmed Salum Mbweta ambaye ameibuka mshindi wa tatu.
Mshindi wa kwanza katika kundi la kwanza la kusoma na kuhifadhi Quran kwa mtindo wa riwaya ya warshi (Riwayat Warsh) ni Murtado Olatunji Katibi wa Nigeria. Wa pili ni Abdinassir Hassan Ibrahim kutoka Somalia na wa tatu ni Khatry Dakhay kutoka Mauritania.
Katika kundi la tatu ambalo ni la tajwid, mshindi wa kwanza alikuwa ni Ustaadh Ahmad Salim Mbwewa ambaye ni mwalimu wa watoto jijini Dar es Salaam.