RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
CHAMA cha ACT Wazalendo kimeishauri Serikali kusitisha nyongeza ya mkataba wa kukodisha kitengo cha makasha kati yake na kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena (TICTS) kwa kile ilichoeleza kuwa imeshindwa kukidhi matarajio ya kukodishwa kwake.
Akizungumza leo na waandishi wa habari makao makuu ya ACT Wazalendo, Kijitonyama, Dar es Salaam, Msemaji wa Sekta ya Mawasiliano, Teknolojia, Habari na Uchukuzi wa chama hicho, Ally Saleh alisema chama chake kina mapendekezo matano kwa Serikali kuhusu uendeshaji wa kitengo cha makasha bandarini na hatua zinazopaswa kuchukuliwa TICTS.
Pamoja na kushauri mkataba huo usitishwe, Salah aliyataja mapendekezo mengine kuwa ni ACT Wazalendo kuungana na wadau waliotoa mapendekezo yao kuhusu mkataba wa TICTS yanayotaka kampuni hiyo isipewe mkataba mwingine baada ya huu wa sasa kumalizika na kwamba suala la ukodishaji au kutokodishwa tena TICTS lifanywe kizalendo kwa maana ya kujali maslahi ya Taifa.
Saleh alisema mapendekezo mengine ya chama chake kwa Serikali ni kufanya uchambuzi wa kina wakati wa utoaji wa zabuni kwa kampuni zenye sifa ya kimataifa kwa kupima utendaji wa TICTS katika kipindi cha miaka 20, faida na uwezo wa kufikisha malengo mapya yatakayokuwa katika mkataba utakaoingiwa.
“Serikali, iiwezeshe mamlaka ya bandari kusimamia kitengo cha makasha cha Bandari ya Dar es Salaam wakati wa mpito ambapo itakuwa kwenye mchakato wa kutafuta mwekezaji mwingine.
Aidha, kwa kuwa imetajwa kuwa moja ya kilichochangia hali ya sasa ni kuwa Serikali kutowekeza ipasavyo kwa yale inayowajibika nayo, ni vyema jambo hilo sasa lisimamiwe kwa umuhimu mkubwa ili kuongeza ufanisi,” alisema Salehe.
Alisema mapendekezo hayo ACT Wazalendo kwa Serikali yamefikiwa baada ya kuwepo mjadala wa mara kwa mara juu ya utendaji kazi usioridhisha wa TICTS.
Saleh alisema matarajio ya kukodisha kitengo cha makasha katika Bandari ya Dar es Salaam kwa makampuni binafsi yalikuwa ni kuboresha utendaji ili kuongeza mchango wa Sekta ya Bandari katika uchumi wa Taifa na kupunguza gharama za kuhudumia shehena za makasha zinazopita bandarini ili kuhimili ushindani na nchi jirani,
Alisema matarajio mengine yalikuwa kuvutia shehena za ndani na nje ya nchi zinazopita katika Bandari ya Dar es Salaam na kuingiza teknolojia mpya na kuwawezesha wazawa kupata mbinu mpya za usimamizi na uongozi wa bandari.
“Hivi sasa, mkataba wa TICTS unapoelekea ukiongoni, kuna hoja kwamba taasisi hiyo haikufanikiwa kufanya yaliyotarajiwa kwenye matakwa ya mkataba,” alisema Saleh.
Alisema malalamiko ya utendaji wa kampuni hiyo yametiliwa mkazo zaidi na wafanya biashara na waagizaji, ambao wamekuwa wakibeba mzigo wa gharama za uchelewaji wa kufunga meli na kuondosha mizigo yao madai yakiwa dhidi ya TICTS.