Sunday, August 24, 2025
spot_img

DED KURUTHUM: NJOMBE MJI TUNAKANYAGA NYAYO ZA RAIS SAMIA

  

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Kuruthum Sadiki


 MAKALA MAALUMU

RIPOTA PANORAMA –
ALIYEKUWA NJOMBE

0711 46 49 84

KAZI ya kutafuta maendeleo na ustawi wa kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji Njombe inaendelea. Kiongozi wa kazi hiyo ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Kuruthum Sadiki.

Ni Mkurugenzi kijana aliyepata mafanikio makubwa ya kiuongozi ndani ya muda mfupi aliokabidhiwa jukumu la kuiongoza halmashauri hiyo ambayo sasa ni miongoni mwa halmashauri za miji zinazofanya vizuri katika ukusanyaji mapato kwa halmashauri za miji nchini.

Kuruthum ameingia katika historia ya kuiongoza Halmashauri ya Mji Njombe ambayo ni moja ya miji ya kihistoria hapa Tanzania. Kwa mujibu wa historia, jina Njombe lilitokana na Kijiji cha Mdandu ambacho zamani za kale, kilikuwa kikijulikana kwa jina la Mdzombe.

Historia inaonyesha kuwa Mdandu lilikuwa Boma la Wakoloni wa Kijerumani kipindi walipokuwa wakiitawala Tanganyika na jina Mdzombe ambalo lilikuja kuwa linatamkwa Mdandu, lilitokana na uwepo wa mti mkubwa ndani ya Kiijiji cha Njombe kabla ya utawala wa Wajerumani.

Jina Mdandu lilianza kubadilika na kutamkwa Njombe baada ya wakoloni wa Kijerumani kushindwa kutamka Mdandu, wakawa wanatamka Njombe; huo ndiyo ukawa mwanzo wa jina Njombe kukita mizizi na kuzikwa kwa jina la asili la Mdandu.

Katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni ofisini kwake Njombe, Kuruthum analielezea eneo lake la utawala la Halmashauri ya Mji Njombe kuwa; ilianzishwa Julai Mosi 2007 kwa tangazo la Gazeti la Serikali na GN namba 118 na 119 baada ya kugawanywa kwa Wilaya ya Njombe ambayo ndiyo iliyozaa Halmashauri ya Mji Njombe. Halmashauri ya Mji Njombe ndio makao makuu ya Mkoa wa Njombe. 

Kuruthum anaeleza zaidi kuwa kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya mwaka 2012, Mji wa Njombe una idadi ya watu 130,223 ukiwa na ukuaji wa asilimia 0.8 kwa mwaka.

Anasema ukuaji huo uko chini ya wastani wa ukuaji wa watu kitaifa ambao ni asilimia 2.7. Kwa maneno yake mwenyewe, anasema;

“Halmashauri ya Mji Njombe ina mpango kabambe wa 2018 – 2038 ambao umefanya maoteo ya idadi ya watu kufikia 259,926 ifikapo mwaka 2038.

“Halmashauri hìi ipo pembezoni mwa barabara ya Makambako – Songea, upande wa kusini inapakana na Wilaya ya Ludewa na Mkoa wa Ruvuma, upande wa mashariki inapakana na Mkoa wa Ruvuma na magharibi inapakana na Wilaya ya Makete.

“Halmashauri ya Mji Njombe ina Kata 13, Vijiji 44 na Mitaa 28. Kata 10 zina hali ya uendelezaji kimji na sehemu kubwa ni vijiji. Kata tatu zilizo katikati ya makao makuu ya mji zimeendelezwa kimji kwa asilimi 80.

“Kuhusu hali ya hewa ya Mji wa Njombe na Mkoa wa Njombe kwa ujumla ni baridi inayosababishwa na hali ya mwinuko unaotengeneza ukanda wa nyanda za juu, ukanda wa nyanda za kati na nyanda za chini. Ukanda wa kati una mwinuko kati ya mita 700 na 1700 kutoka usawa wa bahari na hupokea mvua kati ya milimita 1100 na 1300 huku joto likiwa kati ya nyuzijoto 10 mwezi Juni na Julai katika maeneo ya ukanda wa nyanda za juu.

“Katika mji wangu huu wa Njombe, joto kali lipo mwezi Novemba ambapo huwa linafikia nyuzijoto 18 na msimu wa baridi kali ni kuanzia mwezi Juni hadi Julai ambapo joto ni nyuzijoto 10 hadi 12.

“Hali ya sura ya nchi ina miinuko na mabonde yenye mita 1000 hadi 2000 kutoka usawa wa bahari. Mji una milima, vilima, mabonde na mito ambayo hutoa huduma za ekolojia. Mabonde katika eneo la kitovu cha mji yanapatikana Melinze, Ngalanga, Kilimani, Kihesa, Luhuji, Ijumilo, Kibena, Matarawe, Uwanja wa Ndege na Hagafilo.

“Mabonde haya hutumiwa kama vyanzo vya maji na maji haya hutiririsha maji yake katika Mto Ruaha Mkuu. Ni matumaini yangu utapata wasaa wa kutosha kutembelea mji huu na kuyaona yote haya ili upate picha nzuri ya kuitangaza halmashauri yetu. 

 

Ramani ya Mkoa wa Njombe ikionyesha mahali Mji wa Njombe uliopo (eneo lanye rangi ya pinki)

 

Unapaswa kutenga muda wako wa kutosha kuyafikia maeneo yote ili ukaandike kiunaga ubaga kuhusu Njombe yetu kwa sababu watu wengi hawaifahamu Njombe. Wakiifahamu watavutika kuja, mimi nataka waje hasa wawekezaji, tuje tuendeleze kazi.”
 

Kuruthum anazunguzia pia uwekezaji katika Halmashauri ya Mji Njombe kuwa mji huo una faida nyingi kwa kuwa Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania ambao unavutia uwekezaji wa aina zote kwani kuna ardhi nzuri yenye rutuba na barabara nzuri zinazopitika muda wote zinazounganisha Mikoa ya Tanzania na nchi jirani. 

Anasema hali ya hewa katika Mji wa Njombe inavutia kwa uwekezaji na utalii pamoja na mambo mengine mengi kwa ajili ya utalii wa ndani na kwa wageni kutoka mataifa ya nje. Anasema;

“Halmashauri ya Mji Njombe ifikapo Mwaka2038. Kupitia dira na dhima iliyopo kuna matarajio ya kuwa na ongezeko la viwanda kutokana na uwepo wa

maeneo yaliyotengwa kwa ajili yaviwanda vidogo, viwanda vya kati na vikubwa, ambapo asilimia 10.2 ya eneo la mji limetengwa kwa ajili ya uwekezaji.

“Ni matumaini yangu kuwa Halmashauri ya Mji Njombe itakua kitovu cha 

 

Ramani inayoonyesha mito na sura


kibiashara kutokana na ujenzi wa miundombinu ya barabara na utoaji wa huduma za jamii. Utekelezaji wa miradi mikubwa ya soko, stendi kuu ya mabasi na ujenzi wa kituo cha kuegesha magari makubwa kumechochea maendeleo ya Halmashauri ya Mji Njombe 


“Kiujumla, hali ya uchumi katika Mji wa Njombe. Niseme Mji wa Njombe una utajiri wa rasilimali nyingi ikiwemo ardhi yenye rutuba, hali ya hewa tulivu, vyanzo vya maji, madini, misitu ya asili, misitu ya kupanda na maporomoko ya maji. Rasilimali zote hizi zinaongeza fursa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na utoaji wa fursa za ajira na kupunguza umasikini kwa watu wetu.

“Nizungumzie kwa urefu kidogo fursa za uzalishaji na uwekezaji katika Halmashauri yangu ya Mji Njombe. Halmashauri ya Mji Njombe inazo rasilimali nyingi na hizi zinasababisha uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji.

“Kwanza kuhusu sekta za uzalishaji na uwekezaji nianze na kilimo. Sekta ya kilimo katika Mji wa Njombe inazo fursa nyingi za uwekezaji katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara ambayo ni mahindi, maharage, viazi mviringo na maharage ya soya. Pia yapo mazao ya kibiashara kama vile chai, kahawa na ngano. Aidha yapo mazao ya matunda ambayo ni parachichi, apples na nyanya. Katika mpango kabambe, jumla ya hekta 130,046.9 zimetengwa kwa ajili ya Kilimo.

“Niseme kidogo pia kuhusu ufugaji. Halmashauri ya Mji Njombe inazo fursa nyingi kwenye sekta ya ufugaji kwani mahitaji ya bidhaa zitokanazo na ufugaji ambazo ni nyama na maziwa ni makubwa. Kwa sasa kuna idadi ndogo ya wafugaji ukilinganisha na mahitaji.

“Ardhi ya kuchungia ipo katika Kata ya Kifanya na Iwungilo ambako kuna jumla ya hekta 1500 zilizotengwa kwa ajili ya machungio, Pia ufugaji wa ndani unaweza kufanyika katika maeneo yote.

“Kuhusu misitu; Niseme Halmashauri ya Mji Njombe uchumi wake unategemea kilimo cha miti ya kupandwa. Kuna jumla ya hekta 130,046.9 zimetengwa kwa ajili ya kilimo cha miti.

“Na katika sekta ya misitu kuna fursa za uwekezaji wa viwanda vya usindikaji miti ili kuongeza thamani ya mazao ya misitu, hivyo mpaka sasa kuna kiwanda kikubwa kimoja cha TAWATT na vingine vidogo vidogo.

“Lakini pia Nyuki; Halmashauri ya Mji Njombe ina hali ya hewa inayovutia uwekezaji katika ufugaji nyuki. Kuna aina mbili za ufugaji wa nyuki ambazo ni njia ya asili na njia za kisasa.

“Ufugaji wa Nyuki ukifanyika kwa njia za kisasa utafungua milango ya uwekezaji na kuongeza ukusanyaji wa mapato na kipato kwa wananchi ikiwemo pia kufungua milango ya ajira.

Shamba la Maua Uwemba


“Kwenye Samaki; Ufugaji wa samaki ni moja ya fursa zilizopo katika Mji wa Njombe, kwa sasa shughuli hii inafanyika kwa kiwango kidogo ukilinganisha na uhitaji wa mazao yatokanayo na ufugaji wa samaki. 

 

Mzinga wa Nyuki


“Hivyo, kutokana na mahitaji hayo wafanyabiashara wanaagiza samaki kutoka maeneo ya nje ya Mji wa Njombe kama vile Mwanza, Mtera, Ludewa, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika .
 

“Hivyo, endapo ufugaji wa samaki utafanyika kwa kiwango cha juu utafungua utoaji wa huduma, ajira na kipato kwa wananchi. Tunahitaji sana kujitangaza na naamini nyie wenzetu mtatusaidia katika hili na uanze wewe kuitangaza Njombe, anza na Halmashauri ya Mji Njombe.

“Hii ni nchi yetu sote, tuipambanie kwa pamoja. Sisi kwa upande wetu tunatimiza wajibu wetu, wenzetu tuungeni mkono na sisi tupo tayari kutoa ushirikiano kwenu.

“Utalii; kwanza nisema wazi kuwa utalii katika Mji wa Njombe unafanyika katika kiwango cha chini sana, ingawa mji unazo fursa nyingi za utalii kama vile Maporomoko ya Ruhuji, Hagafilo na Nyamiyuya na eneo oevu la Utengule.

“Pia kuna mapango ya kihistioria yanayohusu vita ya Wajerumani na Wabena ambayo yapo Ihalula, Watanzania wengi wa kizazi cha sasa hawayajui mapango haya. Andika uwaalike waje wafanye utalii wa ndani kwenye mapango hayo, vijana wanafunzi waje wajifunze sehemu ya historia ya Taifa lao.

“Pia kuna misitu ya asili kama vile Itoni, Mapala, Nguruka, Ikowe, Njilikwa, Nundu, Makowo na Idamba. Vivutio vingine vya utalii katika Halmashauri ya Mji Njombe ni kanisa la kihistoria la Yakobi.

“Kuna ngoma za asili zinazoenzi utamaduni wa Kiafrka na Kitanzania, Hali ya hewa. (Hapo ananyamaza na kucheka kidogo kisha anaendelea kuzungumza) Hali ya hewa ya baridi hapa Njombe ni kivutio tosha cha utalii. Mtanzania hahitaji kwenda Ulaya kujionea hali ya hewa ya baridi, hapa Njombe kuna hali ya hewa inayofanana na baadhi ya mataifa ya Ulaya na Amerika na mandhari ya mji ni ya kuvutia sana, ni kijani mtupu.

“Hali ya hewa ya baridi kali inaweza ikatumika kama utalii wa ndani kipindi cha baridi cha mwezi Juni mpaka Agosti. Na nisisahau Bonde la Nyikamtwe linayo historia ya vita ya majimaji. Ni historia hii. Nawaalika watanzania waje wafanye utalii wa ndani wajifunze uzuri wa kustaajabisha wa Tanzania yao uliofichika huku Halmashauri ya Mji Njombe.

” Huu mji, mji wa Njombe unaunganishwa na barabara za uhakika na zinazopitika wakati wote kwa hiyo Njombe inafikika kwa urahisi na pia wakati wote.

“Lakini pia Mji wa Njombe unao mto mkubwa, Mto Luhuji ambao hutiririsha maji yake katika Mto Ruaha, pia kuna mito mingine kama Hagafilo na mingine midogo ambayo yote hutiririsha maji yake katika Mto Luhuji. Mto huu ni kivutio kikubwa cha utalii.

“Mji wa njombe una miti ya aina mbalimbali ya kupanda na ya asili. Kwa kiasi kikubwa maisha ya Njombe ni kilimo. Kilimo cha miti kinapatikana katika maeneo yote ya Mji wa Njombe. Miti inayolimwa kwa wingi ni Mipaina (Pines), Mikaratusi na Miwati. Miti hii hutumika kwa shughuli za ujenzi, nguzo za umeme na mkaa kwa Miwati. Mtalii anapokuja Njombe ataona na kujifunza jinsi ya ustawishaji miti hii unavyofanyika, namna inavyovunwa na kuongezwa thamani.”

Kuruthum hakuishia hapo, bali alizungumzia pia Sekta ya Nishati na Viwanda. Na hapa anaeleza; “Mji wa Njombe unazo fursa za madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu inayopatikana katika maeneo ya Uwemba na Makanjaula. Pia kuna ‘Copper’ inayopatikana eneo la Iwungilo.

“Hata hivyo bado uibuaji wa madini au niseme utafiti haujafanyika kwa kina. Pia kuna uchimbaji wa madini ya ujenzi (Quarrying) katika mwamba uliopo eneo la Mfereke – Nyikamtwe na Matalawe ambao unafanyika kwa kutumia zana duni.

 

Maporomoko ya Hagafilo


“Tunahitaji wawekezaji wa ndani na nje waje wawekeze kwenye maeneo haya. Endapo njia za kisasa zitatumika, vikajengwa viwanda vya uzalishaji na uchakataji madini yetu haya, uzalishaji utaongezeka na hapo ajira na kipato kwa watu wetu vitaongezeka. Kwa hiyo niwaalike tena wawezekezaji wa ndani na kutoka nje wenye mitaji yao waje Njombe.

“Njombe inazo malighafi na rasilimali nyingi kama nilivyoeleza ambazo zinaweza kutumika katika viwanda ili kuongeza thamani ya malighafi zinazozalishwa katika sekta zote. Tumetenga hekta 32,674 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda katika maeneo ya Mjimwema, Njombe Mjini, Yakobi, Kifanya, Matola, Ramadhani, Uwemba, Luponde na Iwungilo.

“Eneo lipo tayari, mwekezaji akija sisi Njombe hatuna hadithi ya nenda rudi ilimradi tu awe mwekezaji kweli, anapata eneo anaanza kazi. Eneo la Yakobi kwa mfano, Halmashauri imepima maeneo ya uwekezaji yenye ukubwa wa ekari 150 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda. Hilo tayari limeishapimwa.

“Njombe ina nishati ya kutosha ya umeme na kuni ambazo hutumika kwa matumizi ya viwandani na majumbani. Kuna fursa ya kuwekeza katika uzalishaji wa Nishati ya Umeme utokanao na maji katika Maporomoko ya Mito Hagafilo na Ruhuji.”

Kuruthum anazungumzia pia siri ya halmashauri yake kuwa miongoni mwa halmashauri vinara wa ukusanyaji mapato kitaifa pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma za jamii. Anasema;

“Hapa ndugu yangu mwandishi ni kazi imaendelea mchana na usiku, hakuna kulala. Tunakanyaga mle mle anamokanyanga Mheshima Rais, mama akitoa mguu wake sisi tunaweka. Hivyo umenikuta niko mjini na watu wangu kwenye ukaguzi wa leseni. 

 

Maporomoko ya Mto Ruhuji


“Unajua wananchi wetu ni lazima kuwakumbusha kila mara. Sasa leo mimi na timu yangu tumeona mapumziko yetu sikukuu hii tuyatumie kuzungumza na wananchi ambao leseni zao zimeisha kwenda kulipa.

“Hakuna haja ya kuwakamata, sisi kwenye ukaguzi wetu tukikuta mtu wetu leseni yake imeisha tunamwambia kwa kumkumbusha atimize wajibu wake, akalipe. Nawashukuru sana wana Njombe wanatoa ushirikiano wa kutosha.

“Sasa kuhusu siri ya kuwa kinara wa ukusanyaji mapato kwa nchi nzima kwa halmashauri za miji, ni team work. Kufanya kazi kwa pamoja kwa kushirikiana ndiyo siri ya mafanikio yetu Halmashauri ya Njombe Mji. Bila ushirikiano tusingefanikiwa.

“Kwa hii robo ya tatu ya mwaka iliyopita tumevuka malengo ya ukusanyaji mapato kwa kukusanya asilimia 153. Kila mara tumekuwa tukivuka malengo yaliyowekwa lakini siri kubwa ni ushirikiano. Robo iliyopita ukiacha hii ambayo pia tumefanya vizuri nayo pia tulivuka malengo yaliyowekewa na tulikuwa miongoni mwa halmshauri za miji zilizofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato.

“Sisi huwa tunajiwekea malengo ya ukusanyaji kila wiki ambayo ni lazima tuyafikie kwa zaidi ya asilimia 100. Kila wiki tunahakikisha hivyo. Kiongozi mkuu wa nchi anamokanyanga na sisi tunakanyaga humo humo. 

“Vyanzo vyetu vya mapato kwa asilimia kubwa tunategemea mazao ya kilimo kama uvunaji wa miti. Tunavyo pia vyanzo vingine kama soko letu kubwa ambalo ni zuri na limejaa wajasiriamali, tuna stendi ya mabasi ya mji ambayo ni ya kisasa na tuna viwanda. Mapato yetu yanatoka huko.

“Kwa upande wa huduma, Mji wa Njombe unakua kwa kasi, hivyo uhitaji wa huduma ni mkubwa. Huduma zinazohitajika ni za elimu ya juu, hoteli, maeneo ya kupumzikia (Recreation Parks), afya, vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu.

“Elimu ya msingi na sekondari tunakwenda vizuri sana. Tulipokea Shilingi mil. 470 ambazo tumezitumia kujenga madarasa 37 na bweni moja ambayo yatasaidia sana kuondoa msongamano wa wanafunzi hasa hapa mjini maana hapa mjini ndiyo kuna msongamano wa wanafunzi hivyo kwenye shule ambazo wanafunzi wamefurika majengo haya yataondoa huo msongamano.

“Afya pia tunakwenda vizuri. Tuna zahanati za kutosha, vituo vya afya vya kutosha tunatumia hela zetu za ndani kuboresha huduma za afya kwa wananchi wetu na Serikali Kuu ilituletea Shilingi mil 500 za tozo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya. Kazi inaendelea usiku na mchana. Watanzania tunaweza.

“Kwa niaba ya timu yangu katika Halmashauri ya Mji Njombe, wananchi wa Mji wa Njombe tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuonyesha njia. Tunapita humo humo anamotuelekeza na mambo ndiyo hayo, sasa tunakimbia kwa kasi sana. Namuahidi, sitamuangusha.

Jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Mji Njombe


 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya