Mkuu wa Mkoa (RC) wa Simiyu, David Kafulila |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini, (LATRA) limeeleza kufarijika na uamuzi wa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Simiyu, David Kafulila, kupiga marufuku matumizi ya magari madogo, maarufu kwa jina la mchomoko, kusafirisha abiria.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na LATRA imeeleza kuwa faraja iliyotokana na uamuzi wa Kafulila ulioanza kutekelezwa Julai 13, 2022, msingi wake ni ukweli kuwa unalenga kukomesha ajali za barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa Kafulila unalenga kukomesha ajali zinazoua abiria wengi wakati ‘mchomoko’ zinapohusika kwenye ajali za barabarani.
“Ni nani asiyejua athari za ajali za barabarani hasa kwa abiria ambapo kwa kipindi chote wamekuwa kama mbuzi wa sadaka. Sasa itoshe tu kusema basi.
“Mbali na athari za ajali, vyombo vidogo vya usafiri vina athari nyingi kiuchumi na kiafya. Abiria wanapotumia vyombo vidogo wanatumia nauli kubwa zaidi na hivyo kupoteza mapato bila uzalishaji.
“Aidha, abiria hukaa kwa shida sana ndani ya vyombo hivi na mzunguko wa hewa ndani ni mdogo, watu warefu na wanene huteseka sana. Kweli itoshe tu kusema sasa basi kutumia vyombo vidogo kwenye njia zote kuu,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Inaeleza zaidi kuwa kwa sababu abiria wanateseka wanapaswa kuacha dhana kwamba vyombo vidogo vinawasafirisha haraka na kupuuza athari za vyombo hivyo.
Aidha, LATRA imetumia taarifa yake kutoa wito kwa abiria wa Mkoa wa Simiyu na wananchi wote wanaotumia magari aina ya ‘mchomoko’ kuunga mkono agizo la Kafulila na pia wakuu wa mikoa yenye vyombo vya usafiri vya aina hiyo kuvipiga marufuku ili kunusuru maisha ya watu.
LATRA imewakumbusha pia abiria wanaotumia usafiri wa bajaj na pikipiki kwenye njia kuu kutambua kuwa nao wapo kwenye hatari kubwa wanapopata ajali za barabarani wakiwa kwenye vyombo hivyo.