![]() |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasili katika viwanja vya Ofisi Kuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa ajili ya kuagana na wakazi wa Loliondo waliohamia Kijiji Cha Msomera, Tanga jana. |
RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WATU 233, waliokuwa wakiishi na kufanya shughuli zao katika eneo la Loliondo, Ngorongoro tayari wamekwishahama kwa hiari.
Watu hao walikuwa wakiishi katika kaya 48 na walikuwa wakimiliki mifugo 899 ambayo wamehama nayo kwa awamu mbili kwa usaidizi na msaada wa Serikali.
Hayo yameelezwa jana na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk. Christopher Timbuka kwenye viwanja vya Ofisi Kuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), mkoani Arusha alipokuwa akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu mwenendo wa kuwahamisha wakazi wa eneo hilo waliokubali kuhama kwa hiari yao.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa ambaye jana alikwenda Loliondo, Ngorongoro kuwaaga wakazi wa eneo hilo wanaohama kwa hiari kwenda Kijiji Cha Msomera, kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga kupisha shughuli za uhifadhi, aliwahakikishia wananchi hao kuwa hakuna shughuli zao zitakazosimama na kwamba wataendelea na ufugaji katika mazingira bora zaidi.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alizingumza na wakazi hao takribani 127 kutoka katika kaya 27 waolikuwa tayari kuelekea Kijiji cha Msomera, aliwapongeza kwa uamuzi huo na kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano.
Alisema uamuzi walioufanya wa kuhamia Msomera na kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Ngorongoro ni uamizi sahihi na alitumia fursa hiyo kuwahakikishia kwamba shughuli zao za kawaida hazitasimama bali wataendelea na ufugaji kwa kuwa Msomera kuna eneo kubwa na la kutosha.
“Ninawaomba msafiri kwa amani kabisa na mioyo yenu ikunjuke. Isikilizeni Serikali yenu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Sasa hivi mko huru, nenda mkakae kwenye nchi yenu kwa uhuru,” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk. Timbuka alisema awamu ya pili ya kuwahamisha wakazi wa eneo la Ngorongoro kwa hiari ilianza Juni 20, 2022, ikihusisha kaya 27 zenye watu 127 na mifugo 488. Aidha kaya moja kati ya hizo itahamia Karatu.
Dk. Timbuka alisema hadi sasa kaya zilizohama kwa hiari eneo la Ngorongoro katika awamu ya kwanza na ya pili ni 48 zenye jumla ya watu 233 na mifugo 899. Alisema utaratibu wa kuwahamisha umefanyika kwa kufuata hatua mbalimbali ikiwemo kuhakiki idadi ya watu.
Alizitaja hatua nyingine zilizofuatwa ni kusainisha vitabu vya fidia vya wakazi wanaohama kwa hiari awamu ya pili, kuhakiki idadi ya mifugo na kuiweka alama ili iweze kusafirishwa pamoja na kuhakiki na kutambua aina za nyumba za wakazi hao kwa ajili ya taratibu za ubomoaji.
Dk. Timbuka alisema mbali na kupewa nyumba, fidia na shamba kaya zote pia zitapewa magunia mawili ya mahindi kwa kipindi cha miezi mitatu ili waweze kujikimu katika kipindi cha mpito wakati wakijiandaa na msimu wa kilimo.
Naye, mmoja wa wakazi hao wanaohama kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, Emmanuel Saitoti wa Kijiji cha Nainokanona aliishukuru Serikali kwa upendeleo ilioutoa kwao kwa kuwa mbali ya kupewa nyumba pia Msomera wanakwenda kupata fursa zitakazowaongezea tija kiuchumi.
“Serikali tunaishukuru imetupendelea sana, tumepata hati za nyumba na mashamba pamoja fidia ya fedha, naishauri iendelee kuwahamasisha na wakazi wengine nao wahame kule hakuna maendeleo. Msomera tunakwenda kufanya shughuli nyingi za maendeleo.”
MATUKIO KATIKA PICHA WAZIRI MKUU AKIAGANA NA WAKAZI WA LOLIONDO JANA