MWANDISHI MAALUMU, LOLIONDO
OPERESHENI maalumu ya siku 10 iliyoanza Juni 22, 2022 ya kuwasaka wahamiaji haramu katika eneo la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha inatarajiwa kukamilika Juni 28, 2022.
Kuanza kwa operesheni hiyo kulitangazwa juzi na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Dk. Anna Makakala huko Loliondo muda mfupi baada ya kukagua eneo linalowekewa mipaka na Serikali kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji, mazalia ya wanyama na uhifadhi.
Kamishna Jenerali Makakala alisema operesheni msako wa wahamiaji haramu itakwenda sambamba na kazi inayoendelea ya uwekaji wa alama za mipaka katika Pori Tengefu la Loliondo na kwamba baada ya kukamilika siku 10 za operesheni maalumu, operesheni za kawaida zitaendelea katika eneo hilo.
Alisisitiza wageni kufuata sheria za nchi wanapotaka kuingia nchini na kwamba Jeshi la Uhamiaji lipo katika hali ya utayari kusimamia mipaka yote ya nchi.
“Nchi yetu imebarikiwa kwa kuwa na maeneo mazuri ambayo yanavutia wahamiaji haramu kufika nchini kwa sababu tofauti, hatutakubali hilo litokee wakati wowote ule,” alisema Makakala.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mwalimu Raymond Mangwala alisema wilaya hiyo inaendelea kutekeleza kazi ya uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo na itatoa ushirikiano wakati wa kuwasaka wahamiaji haramu ili wale wote watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi