Pape Sakho, (aliyebinuka tiktak) mmoja wa wachezaji wa kigeni anayesakata kabumbu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara akichezea timu yenye mafanikio makubwa kitaifa na kimataifa, Simba Sports Club. |
DUKULE INJENI, PANORAMA
0711 46 49 84
NDOTO ya kila mchezaji mpira wa miguu ni kucheza kwenye ligi iliyo na ushindani na maslahi bora. Ndiyo maana jibu la haraka haraka unapomuuliza mchezaji angependa kuchezea timu gani atakutajia timu zinazoshiriki ligi barani Ulaya.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Ligi Kuu ya Tanzania Bara ndiyo inayoogoza katika kukusanya wadhamini na kuifanya ligi hiyo kuwa na mvuto. Hata hivyo swali la kujiuliza ni je, udhamini huo wa ligi unaendana na ushindani?
Wakati Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikijivunia udhamini unaokadiriwa kufika Shilingi 234 bilioni, ligi ya Uganda ina udhamini wa Shilingi 17 bilioni huku wadhamini wakifungasha virago vyao katika Ligi Kuu ya Kenya.
Takwimu zinaonyesha Ligi Kuu ya Tanzania Bara imeorodheshwa ya nane kwa ubora barani Afrika na udhamini unaomiminika umeweza kushawishi wasakata kambumbu kutoka Nchi za Zambia, Malawi, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali, Burundi, Ghana, Senegal na mataifa mengine kuja kukipiga Tanzania Bara.
Wadhamini wanaoing’arisha Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni Azam Media Limited ambao wametoa kitita cha Shilingi 225.6 bilioni kwa misimu 10, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambalo limemwaga Shilingi 3.5 bilioni pia kwa miaka 10 na National Bank of Commerce (NBC) ambao msimu huu walisaini mkataba wa Shilingi 2.5 bilioni.
NBC ndiyo wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara waliochukua nafasi ya Vodacom Tanzania na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa NBC, Theobald Sabi, waliamua kudhamini ligi kama moja ya ushiriki wao katika kuendeleza michezo na shughuli zingine nchini.
Akizungumzia udhamini huo kwa waandishi wa habari muda mfupi baada ya NBC kuchukua mikoba iliyokuwa akibebwa na Vodacom Tanzania, Sabi alisema Shilingi 2.5 bilioni ni kwa ajili ya msimu 2021/2022 licha ya kuingia mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), akiongeza kuwa wanajivunia ushirikiano wao na TFF katika kudhamini mchezo unaovutia mashabiki wengi.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, ambayo ni wadhamini wakuu wa Ligi ya Tanzania Bara. |
“Naipongeza TFF na klabu kwa mafanikio ambayo yameifanya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuorodheshwa ya nane kwa ubora barani Afrika na hii ndiyo sababu tunawekeza kwenye mchezo huu,” alisema Sabi.
Rais wa TFF, Wallace Karia, mwanzoni mwa msimu unaomalizika, alivitaka vilabu kutumia kwa ufasaha udhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ili iwe ya kiushindani zaidi.
“Hii ni hatua kubwa katika kuendeleza soka. TFF inapambana kupunguzia klabu mzigo ili washiriki ligi pasipo na bugudha na wachezaji waonyeshe kiwango chao bora,” alisema Karia.
Wakati wa utiaji saini mkataba kati ya TFF na NBC, Karia pia alikumbusha kuwa alipochaguliwa aliweka wazi lengo lake lilikua kuwepo na ligi bora Tanzania.
Wakati timu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zikinufaika na udhamini mnono, hali ni tete kwa Ligi Kuu ya Kenya kwani wadhamini wanajiondoa huku Serikali ikiunda kamati ya muda kusimamia shughuli za soka baada ya kumuondoa ofisini aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia |
Ligi Kuu ya Kenya ilikua na wadhamini wawili lakini wakapata pigo baada ya wadhamini kuondoka wakipishana kwa takribani miezi mitatu huku sababu kuu ikitajwa kuwa ni usimamizi mbovu wa soka.
Kwanza ilikua Kampuni ya Kamari kutoka Nigeria, BetKing, waliositisha udhamini wao wakidai ni makubaliano kati yao na FKF. Hata hivyo tetesi zinadai klabu mbili kubwa; Gor Mahia na AFC Leopards, ndiyo chanzo kikuu cha BetKing kujiondoa baada ya kulalamika kutolipwa.
Dili ambalo FKF ilipoteza ni mkataba wa miaka mitano yenye thamani ya Shilingi 24 bilioni kudhamini Ligi Kuu ya Kenya. Kwenye dili hilo, BetKing ilikua ianze kwa kutoa Shilingi 4.4 bilioni kwa mwaka wa kwanza na kuongeza kwa asilimia tano mwaka wa pili kisha asilimia 10 kwa miaka inayofuata.
Dili hili la BetKing lilimshtua aliyekuwa Rais wa FKF, Sam Nyamweya ambaye pia alihoji ni namna gani shirikisho linatumia fedha za udhamini kwa malengo ya muda mfupi.
“Inasikitisha udhamini ambao FKF wanadai haujapata kutokea katika historia ya Kenya haupo tena kutokana na waliopo ofisini kutofanyi kazi vizuri,” alinukuliwa Nyamweya akielekeza shutuma zake kwa uongozi wa Mwendwa.
Miezi chache baada ya BetKing kufungasha virago, Kampuni ya StarTimes yenye makao yake makuu jijini Beijing, China nao walisitisha udhamini wao wenye thamani ya Sh110 milioni kila mwaka.
FKF iliingia mkataba wa miaka saba na Kampuni ya StarTimes ambapo miongoni mwa makubaliano ilikua FKF kuwezesha urushwaji wa mechi za ligi, mechi 30 za Ligi Daraja la Kwanza na mechi za kirafiki zinazohusu Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars.
Lakini mwaka moja tu baadaye, StarTimes wamesitisha mkataba wao na FKF wakianisha mambo mengi ikiwemo malumbano ya mara kwa mara kati ya taasisi iliyopewa jukumu kusimamia soka nchini Kenya na wadau wake kama vile vyombo vya habari na klabu zinazoshiriki ligi kuu.
Aidha, StarTimes ilikerwa na kushindwa kuonyesha mubashara idadi ya mechi zilizoratibwa ikiwemo dabi la mashemeji, (Gor Mahia na AFC Leopards), msimu uliopita licha ya awali kudhibitisha kufanya hivyo.
Licha ya StarTimes kusitisha mkataba wake na FKF, bado wanabaki kuwa wadhamini wakuu na wenye haki ya kurusha matangazo ya mechi za Ligi Kuu ya Uganda baada ya makubaliano kati ya Chama cha Soka cha Uganda (FUFA) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu ya Uganda ambapo kwa pamoja na StarTimes waliingia mkataba wa miaka 10 ulioaza msimu wa 2018/19.
Mkataba huo wenye thamani ya Shilingi 17 bilioni umetajwa na Rais wa FUFA, Moses Magogo, kama mkubwa na utakaobadili soka la Uganda.
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa udhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara bado unabaki kuwa mkubwa ukilinganisha na mataifa jirani na hauna budi kuhakikisha ligi inakuwa ya ushindani.