Sunday, June 22, 2025
spot_img

WAZIRI MBAWARA AJITENGA NA SAKATA LA HISA ZA MECCO

Waziri na Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbawara

RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
 

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbawara amejitenga mbali na mfanyabiashara Adulkadir Mohamedi anayetajwa katika utata wa hisa za Kampuni ya Mwananchi Engineering and Construction Company Limited (MECCO).

Mohamedi, maarufu kwa jina la Bujeeti anamiliki asilimia 75 ya hisa za MECCO, kampuni iliyoanzishwa kwa malengo maalumu lakini pia anadaiwa kutaka kuchukua kinyemela asilimia 25 ya hisa zilizosalia mikononi mwa Serikali.

Katika mpango huo, mfanyabiashara huyo anadaiwa kuiingiza kampuni yake nyingine katika biashara na MECCO katika kile kinachodaiwa kuwa ni kurahisisha mpango wake huo.

Imeelezwa kwamba mipango yote hiyo anaifanya kwa kuwatisha watendaji serikalini na wafanyabiashara akiwapakazia viongozi waandamizi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM), huku ikibainika kwamba baadhi ya anaowataja hana hata mawasiliano nao.

Vitisho hivyo vya Mohammed vinafika hadi kwa wafanyakazi wake akiwambia kwamba anaweza kuwashughulikia au kuwafanya lolote kwa kuwa ana nguvu na mtandao mkubwa.

Waziri Profesa Mbawara ambaye inadaiwa jina lake ni miongoni mwa majina yanayotumiwa vibaya na Mohamedi kutishia, juzi alimkana akiiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa jambo hilo yeye halijui. Alisema mambo ya kutishana yamepitwa na wakati na kwake yeye Watanzania wote ni sawa.

“Hili silijui mimi, kwa maoni yangu umuulize yeye. Kwanza mambo ya kutishina yamepitwa na wakati. Kwangu Mimi Watanzania wote ni sawa,” alisema Profesa Mbawara katika majibu yake mafupi kwa PANORAMA Blog.

PANORAMA Blog ilimuuliza Waziri Mbarawa kuwa Abdulkadir Mohammed, maarufu kwa jina la mzee Bujeeti ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Kisomali amekuwa akitumia majina ya viongozi vibaya kujigamba kwa wafanyakazi wake na washindani wake wa kibiashara kuwa yupo karibu sana na viongozi wa juu wa nchi na baadhi ya majina ya viongozi anayodaiwa kuyatumia kujigamba hivyo ni jina la Waziri Mbawara.

Katika majigambo hayo anadaiwa kusema hakuna jambo lake linaloweza kukwama kwa sababu ya kuwa karibu na Waziri Mbawara hivyo iliomba kujua iwapo anamfahamu Mohamedi na au amepata kuwa karibu naye.

PANORAMA Blog pia iliomba kupata kauli ya Waziri Mbawara kuhusu madai kuwa Mohamedi amekuwa akiwatisha watendaji wa Taasisi za Umma, binafsi na wafanyabiashara wenzake kuwa ana nguvu serikalini na CCM kwa sababu yupo karibu naye jambo linalotia ukakasi rekodi zake nzuri alizojijengea katika utumishi wa umma na iwapo amepata kutoa msaada wa aina yoyote kwa Mohamedi.

Inadaiwa hadi sasa Serikali haijaambulia chochote kwenye fedha zaidi ya Shilingi Bilioni tano ambazo zinatokana na biashara inayofanyika katika eneo la MECCO kutokana na Mohamedi ambaye ana hisa asilimia 75 kwenye kampuni hiyo kutowasilisha fedha hizo serikalini.

Aidha, inadaiwa kuwa baada ya kifo cha kigogo mmoja serikalini ambaye alikuwa anaiwakilisha Serikali katika Kampuni ya MECCO (jina tunalihifadhi kwa sasa), Mohamedi amedaiwa kutaka kuchukua hata asilimia 25 ya hisa za Serikali zilizokuwa zikishikiliwa na kigogo huyo.

Hivi sasa inadaiwa Mohamedi ameshafanya mchakato wa kubadilisha umiliki na jina kutoka MECCO na kuwa MAS akianza kwa kutaka kufanya biashara ya kuhifadhi na kusimamia makontena.

Rekodi rasmi zilizopo Serikali kuhusu Kampuni ya Mwananchi Engineering and Construction Company Ltd zinaonyesha kuwa ilisajiliwa Aprili 3, 2007 ikiwa na mtaji wa Shilingi milioni 443,732,000 iliogawanywa katika hisa 443,732 na kila hisa moja ikiwa na thamani ya Shilingi 1,000.

Kwa mujibu wa rekodi hizo ambazo PANORAMA Blog imeziona, mwanasheria wa kampuni wakati inasajiliwa ni Dk. Harrison George Mwakyembe na wakurugenzi wake ni Abdulkadir Sheekh Mohamedi, Maungo Obadia Kwabhi, Peter Mhina na Agnes Enos Bukuku.

Kampuni hiyo ambayo ofisi zake zipo barabara ya Nyerere, Plot nambari 2 na 3 B ina wana hisa wawili ambao ni Sisi Construction Company Limited yenye hisa asilimia 75 na Msajili wa Hazina ambaye ana hisa asilimia 25.

Mohamedi mwenyewe amekuwa kimya kila alipoulizwa kuhusu sakata la MECCO. Hivi karibuni Mfanyabiashara huyo alitoa vitisho kwa mwandishi aliyeuliza kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake.

PANORAMA Blog imemtafuta bila mafanikio Msajili wa Hazina ili kuzungumzia suala hili lakini jitahada za kumpata zinaendelea.

Kampuni ya Mwananchi Engineering and Construction Company Limited ni moja kati ya kampuni kubwa hapa nchini na imetekeleza miradi mingi mikubwa.

Baadhi ya miradi mikubwa iliyotekelezwa na MECCO ni pamoja na ujenzi wa Jengo la
Benki Kuu ya Tanzania lililopo Arusha na Hotel ya Mount Meru. Mkoani Tanga MECCO imejenga Jengo la Hispotali ya Bombo na katika Mkoa wa Dar es Salaam imejenga Jengo la Makao ya Bima (NIC)

Miradi mingine iliyotekelezwa na MECCO katika Mkoa wa Dar es Salaam ni Ujenzi wa Soko la Kariakoo, Makao Makuu ya Kampuni ya Sigara pamoja na miradi mingine mingi ya ujenzi wa barabara, madaraja, barabara za kurukia ndege na mitaro ya maji.

Abdulkadir Mahomedi edi

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya