RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Kyando Mchechu amepewa tuzo ya kutambua mchango wake kwa Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS).
Tuzo hiyo alikabidhiwa jana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Boneventure Rutinwa wakati wa mhadhara wa miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam uliofanyikia Hoteli ya Silversands Jijini Dar es Salaam.
Mchechu ambaye rekodi yake katika sekta ya nyumba imekuwa ya kupigiwa mfano huku akibeba mabegani taswira ya mapinduzi katika sekta nyumba, alikabidhiwa tuzo hiyo ikiwa ni shukrani ya kutambua mchango wake kwa UDBS.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mchechu alizitaka taasisi za elimu nchini kuangalia uhalisia wa mitàala ya elimu inayoendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira kitaifa na kimataifa.
Mchechu ambaye pia alipata fursa ya kutoa mada katika mhadhara huo ulioandaliwa na UDBS kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema, ipo haja kwa vyuo vikuu kuwa na kanzidata ya wahitimu wake ili kuwa na umoja utakaosaidia kuondoa changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo kusaidia wanafunzi wenye uhitaji wa kupata ufadhili wa masomo na kupata ajira.
Alisema umoja huo utaimarisha mawasiliano na kupashana habari mbalimbali za kitaifa na kimataifa kwa lengo la kufungua milango ya ajira, ujuzi na fursa mbalimbali.
Naye Makamu Mkuu wa UDBS, Profesa Rutinwa alipokuwa akizungumza katika mhadhara huo alisema, amefurahishwa kuona shule kuu hiyo imeweza kuanzisha mfuko wa kusaidia wasio na uwezo na hivyo inaendana na falsafa ya Chuo Kikuu hicho ya kuwa Chuo Kikuu bora duniani.
Alisema moja ya matatizo yanayowakabili wanafunzi kiasi cha kusababisha kupata msongo wa mawazo ni ukosefu wa fedha za kugharamia masomo yao na za kujikimu; na pia aliziomba taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za kuchangia ubora wa elimu Tanzania.