Sunday, June 22, 2025
spot_img

LNG KUIFANYA TANZANIA KINARA WA UCHUMI AFRIKA MASHARIKI

Rais Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya awali ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbani gesi asilia

  DAVID KAFULILA 

JUNI 11, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alishuhudia makubaliano ya awali ya uwekezaji wa Dola za Marekani 30 bilioni kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni kubwa tano za kimataifa ambazo ni Equinor, Shell, ExxonMobil, Medco Energy na Pavilion.

Hii ni hatua muhimu kuelekea makubaliano ya msingi kuhusu utekelezaji na uendeshaji wa mradi (Host Government Agreement) ambayo yanatarajiwa kufikiwa Disemba 2022 na hatimaye uamuzi wa mwisho wa uwekezaji unaotarajiwa kufikiwa mwaka 2025. 

Huu ni uwekezaji mkubwa kwa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika. Mwaka 2016, aliyewahi kuwa Gavana wa Benki ya Tanzania (BoT) Marehenu Profesa Benno Ndulu alisema uwekezaji wa awali tu (initial investment) ungeongeza asilimia mbili ya pato la Taifa.

Uwekezaji wa Dola za Marekani 30 bilioni ni nusu ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ambao ni Dola za Marekani 64 bilioni ni karibu sawa na uchumi wa Uganda kwa sasa ambao ni Dola za Marekani 34 bilioni na karibu mara tatu ya uchumi wa Rwanda kwa sasa ambao ni Dola za Marekani 11 bilioni na karibu sawa na theluthi moja ya uchumi wa Kenya kwa sasa ambayo uchumi wake ni Dola za Marekani 99 bilioni.

Iwapo mwenendo wa uchumi utaenda kama ulivyo (ceteris peribus), biashara hii itaifanya Tanzania kuwa nchi kinara wa uchumi kwa Nchi za Afrika Mashariki.

Huu ni mradi mkubwa unaohusisha weledi katika maeneo mengi ya nishati, biashara na uchumi wa kitaifa na kimataifa, sheria za kitaifa na kimataifa, mazingira na taalumu nyingi zinazohitaji weledi na uzoefu mkubwa. Ndio maana nilipata kuandika kwenye Gazeti la Raia Mwema – Mei 05, 2021 kwamba tulihitaji mshauri eneo hilo kumudu meza ya majadiliano. 

Ndio sababu, Januari 25, 2022 niliposoma kuwa Serikali imepata mshauri mwelekezi ambayo ni kampuni ya yenye uzoefu ya Boots Barker kutoka Uingereza, nilipongeza nikiamini kuwa ilikuwa hatua muhimu kutanzua mkwamo wa mradi huu ambao ulifika mahala ukazua maswali ya tunakwama wapi hasa ikizingatiwa nchi kama Msumbiji ilikuwa imepiga hatua mbele.

Ni kweli nchi yetu ina wasomi na vyuo vingi lakini ni ukweli usiopingika kuwa hatuna hazina yenye weledi na uzoefu wa kutosha kwenda mezani mwanzo mwisho kwenye mradi mkubwa wa kiwango hiki bila kujengeana uwezo wa ziada. 

Na kwa dunia ya leo, sio aibu kununua au kukodi utalaamu usiokuwa nao kufanikisha jambo kubwa kama hili. Nakumbuka Uingereza baada ya mgogoro wa kiuchumi walimteua Mark J. Carney ambaye alipata kuwa Gavana wa Canada kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza (New York Times, Novemba 26, 2012).  https://www.nytimes.com/2012/11/27/business/global/canadian-to-lead-bank-of-england.html#:~:text=LONDON%20%E2%80%94%20In%20a%20surprising%20departure,Britain’s%20most%20prominent%20public%20officials 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila

Au wakati Uingereza inafanya uamuzi wa kujitoa Umoja wa Ulaya, walimteua mshauri mwelekezi kutoka Newsland kuwa mshauri mwelekezi kwenye mikataba mipya ambayo Uingereza ilipaswa kuingia upya kama Taifa na mataifa mengine.

Alipoulizwa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa nini amefanya uamuzi wa kuteua mtaalamu kutoka nchi nyingine kuongoza timu ya wataalamu wake katika kushauri Serikali kuhusu mikataba kati ya nchi yake na nchi zingine, alijibu kuwa kwa muda ambao Uingereza imekaa Umoja wa Ulaya imepoteza uzoefu wake katika kuingia mikataba hiyo kwa kuwa miaka yote mikataba hiyo ilifanyiwa kazi Brussels Ubelgiji.

Sasa kama Taifa kubwa lenye vyuo bora duniani kuna mahala linakubali kupungukiwa na kukodi au kuazima utaalamu toka nje, sioni tatizo kwa nchi yetu kufanya hivyo, muhimu tunajua tunachokitaka na hivyo mshauri anatusaidia namna ya kukifikia.

Lakini pia miradi kama hii inahitaji uelewa na uvumilivu kwa sababu ni mradi unaokwenda kubadilisha kabisa uchumi wa Tanzania lakini unachukua muda (game changer). Ndio unaona mpango wa kufikia uamuzi wa uwekezaji unapangwa kufikiwa mwaka 2025 (investment decision) na mwanzo wa ujenzi mpaka kukamilisha itachukua miaka kadhaa pia.

Na hii ni kawaida. Nchi kama Canada iliwachukua miaka saba kufikia uamuzi wa uwekezaji (Investment Decision) na kampuni hizi za kimataifa kwenye mradi kama huu wa  kimkakati wenye thamani Dola za Marekani 31 bilioni.

https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/magazines/canada-offers-lessons-on-lng-project-for-tanzania-2661110

Kwenye dunia ambayo nishati ni mwamuzi wa uchumi duniani, makubaliano yake yanachagizwa na misukumo mingi ikiwemo ujasusi mkubwa kwani mafanikio ya nchi yoyote kuingia soko la LNG yanabeba tafsiri pia kwa nchi washindani ambao wana sura tofauti ama za kama kampuni za kimataifa zinazoshindana au nchi wahusika zinazoshindana.

Ndio sababu sio ajabu tena mbinu kama ugaidi kuweza kuwa sehemu ya mkakati katika kukabiliana kibiashara tofauti na dhana ya zamani kuhusu misingi ya ugaidi. 

Ni katika msingi huo, uwekezaji mkubwa kama huu unachukuliwa tahadhari zote. Wote tunakumbuka kilichotokea Msumbiji baada ya kuonekana wanaweza kuingia mapema kwenye soko la LNG wakiwa na LNG ya bei nafuu sana kutokana na mazingira ya gesi yao asilia. 

Msumbiji wana bahati kubwa ya gesi asilia karibu futi za ujazo trilioni 100 karibu mara mbili ya Tanzania ambapo gesi iliyokwishagunduliwa inafikia futi za ujazo trilioni 57. 

Zaidi gesi ya Msumbiji karibu asilimia 85 inapatikana kwenye eneo la kina kifupi (shallow water) kulinganisha na Tanzania ambayo karibu asilimia 90 ya gesi ipo bahari ya kina kirefu (deep sea). 

Niliwahi kugusia hili kama sababu ya Msumbiji kututangulia wakati bei ya gesi asilia dunia imeanguka kiasi ambacho ilihitajika kuzalisha kwa unafuu ili kuweza kuwa biashara. 

Tafiti zinaonesha kwamba gharama za kuchimba kisima cha gesi kwenye kina kirefu (deap sea) ni karibu mara mbili ya kuchimba kina kifupi. Kwa takwimu za mwaka 2015 ni kati ya Dola za Marekani milioni 50 mpaka Dola za Marekani milioni 70 kulinganisha na kisima kirefu (deap sea) ambacho ni kati ya Dola za Marekani milioni 100 mpaka Dola za Marekani milioni 120. https://www.sciencedirect.com/topics/engineering/drilling-cost

Naam, changamoto ni nyingi lakini tupo kwenye mstari sahihi. Tunahitaji kujenga mjadala wa uelewa ili kurahisisha mijadala kwenye masuala makubwa yenye maslahi mapana kwa Taifa letu leo na kesho. Tulipoamua kujenga uchumi wa gesi Tanzania kwa kiasi kikubwa tulizama kwenye mradi huu wa gesi asilia (LNG).

MWANDISHI WA MAKALA HII, DAVID KAFULILA NI MKUU WA MKOA WA SIMIYU NA MCHAMBUZI WA MASUALA YA SIASA NA UCHUMI.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya