Sunday, June 22, 2025
spot_img

MCHECHU ABEBA MATUMAINI MAPYA UIMARISHAJI WA SEKTA YA NYUMBA

  

Mradi wa ujenzi wa majengo ya Morocco Square unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.


     MAKALA YA MTANGAZAJI

IKIWA ni miezi takribani mitatu tangu ateuliwe na kurejeshwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Kyando Mchechu kwa kutambua mchango wake katika sekta ya nyumba, nuru ya matumani ya kuendelea kushamiri kwa sekta hiyo imeonekana.

Nyumba kama zilivyo sekta mbalimbali za maendeleo ya nchi hii, haijapewa uzito unaostahili ingawa kumekuwapo jitihada mbalimbali za kuiinua sekta hiyo ili iweze kuinua uchumi wa Taifa lakini pia wa mtu mmoja mmoja.

Mathalani inapochachuliwa sekta ya nyumba unatiwa chachu uchumi wa nchi nzima kwani sekta ya nyumba ni sekta mtambuka na athari zake zinakwenda kutoka kwa mjenzi, zinakwenda kwa muuzaji wa vifaa, fundi anayejenga, msafirishaji, wenye vifaa vya ujenzi na kadhalika.

Kabla ya kusomwa kwa Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkurugenzi Mkuu Mchechu alialikwa na Wizara kuweza kutoa mwelekeo wa Shirika kwa Waheshimiwa Wabunge wote juu ya vipaumbele na namna Shirika hilo litakavyozikabili changamoto za Shirikalakini pamoja na sekta ya nyumba kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Nehemiah Kyando Mchechu (aliye mbele) akiwa ameambatana na Meneja wa Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya muda mfupi baada ya kuwasilisha mwelekeo wa shirika kwa wabunge Jijini Dodoma


Mchechu hakusita kutoa mwelekeo huo ambapo aliwabainishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tangu kuteuliwa kwake tena kuongoza Shirika hilo ameweza kufanyia kazi Mpango Mkakati wa Shirika, kurekebisha muundo wa Shirika ili uweze kuendana na kasi ya utekelezaji wa majukumu yaliyokasimiwa kwa Shirika na Serikali, utekelezaji wa miradi ya nyumba kwa haraka na pia ukamilishaji wa miradi.

Kwa mwelekeo huo huo, Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/ 2023 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imetoa taswira ya Tanzania itakavyokuwa imepiga hatua katika sekta ya ujenzi wa majengo ya makazi, biashara na ofisi ifikapo mwaka 2024/2025.

Bajeti hiyo ikawasilishwa bungeni April 26, 2022 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula, kisha ikajadiliwa na wabunge kabla ya kupitishwa Aprili 27, 2022 ikiwa imebeba mageuzi makubwa ya kisekta na kitaasisi ambapo Shirika la Nyumba la Taifa NHC, pamoja na mambo mengine, likiwa na jukumu la kuwezesha ujenzi wa majengo kwa matumizi mbalimbali hususan makazi, ofisi na biashara limechorewa ramani ya utekelezaji wa majukumu yake yaliyo katika mpango mkakati wa miaka 10 wa uboreshaji sekta ya nyumba nchini.

Mchechu ambaye rekodi zake katika utumishi wa umma zimekuwa si za kutiliwa shaka hata kidogo, sasa amebebeshwa jukumu la kuiongoza timu ya Shirika hilo kutekeleza mpango mkakati wa shirika wa miaka 10 (2015/16 – 2024/25) ambao unalenga kukamilisha miradi ya Shirika iliyo katika hatua mbalimbali na kufanya ukarabati wa majengo ya shirika.

Hatua hizo ni pamoja na kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya ujenzi, kujenga majengo ya biashara na nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali, kuendeleza Miji ya Pembezoni (Satellite Towns); na kutekeleza miradi mbalimbali ya ukandarasi kama ilivyoainishwa katika bajeti ya 2022/2023 iliyolenga kufikia malengo yaliyowekwa katika kutekeleza mpango huo wa miaka 10.

Utekelezaji wa mpango huo umezingatia kazi za NHC zilizokwama katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 ukiwemo wa ujenzi wa majengo marefu yaliyopo eneo la Morocco Jijini Dar es Salaam. Katika mwaka wa fedha 2021/22, NHC ilipanga kukamilisha Mradi wa Morocco Square, Jijini Dar es Salaam ambao ulikwama tangu mwaka 2018 kutokana na changamoto za kifedha.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ilitoa idhini kwa NHC kukopa katika taasisi za fedha za ndani shilingi bilioni 173.9 ili kuukamilisha pamoja na miradi mengine iliyokuwa imesimama ambapo baada ya kutolewa kwa idhini hiyo, shirika limekwishakopa shilingi bilioni 44.7 ili kuukamilisha sambamba na mradi wa ujenzi wa majengo ya Regent Estate uliopo kiwanja nambari 300. Hivi sasa utekelezaji wa Mradi wa Morocco Square umefikia asilimia 93. Asilimia saba iliyobaki inatarajiwa kukamalika utekelezaji wake ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Mradi wa ujenzi wa nyumba Iyumbu unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)

  

Katika utekelezaji wa mradi wa Safaricity, upembuzi yakinifu unaendelea na katika eneo la Burka/Mateves ambapo uandaaji wa mpango kabambe umekamilika na uuzaji wa viwanja katika sehemu ya eneo hilo unaendelea wakati mpango wa ujenzi wa nyumba za awali bado haujaanza katika eneo la Usa River.

Miradi mingine iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2021/22 ambayo utekelezaji wake umeangukia katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 ni ujenzi wa nyumba 101 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na katika Jiji la Dodoma eneo la Iyumbu, nyumba 303 kwa ajili ya kupangisha na kuuza ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa nyumba 1,000.

Hadi Mei 15, 2022, ujenzi wa nyumba 100 na jengo la maduka katika Wilaya ya Chamwino umekamilika kwa asilimia  80 na mradi wa ujenzi wa nyumba 300 na majengo matatu ya huduma za kijamii katika Jiji la Dodoma eneo la Iyumbu nao umekamilika kwa asilimia 90.

Shirika pia lilipanga kuendelea na ujenzi wa majengo ya biashara katika Halmashauri za Manispaa za Lindi na Bukoba pamoja na kutekeleza miradi ya ukandarasi katika maeneo mbalimbali nchini katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Kazi ya usanifu wa jengo la biashara katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ilikamilika Mei 15, 2022 na marekebisho ya michoro yanaendelea kufanyika ili kuendana na taarifa ya uchunguzi wa udongo. Aidha, usanifu wa jengo la biashara katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba umefanyika na taratibu za ununuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi zinaendelea.

Kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya ukandarasi; Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere iliyopo mkoani Mara, awamu ya nne umekamilika kwa asilimia 96 na mradi wa ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mifugo la Buzirayombo lililopo mkoani Geita umekamilika kwa asilimia 94.

Hivi sasa NHC linaendelea na mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira kama Mshauri elekezi na pia linatekeleza kazi ya mapitio ya michoro na gharama za mradi wa ujenzi wa majengo ya Wizara ya Fedha na Mipango katika eneo la Mji wa Serikali, Mtumba.

Sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo NHC lilikuwa nayo katika mwaka wa fedha wa 2021/22, pia lilipanga kuandaa mipango ya uendelezaji wa maeneo mbalimbali nchini pamoja na kutekeleza mpango wa uendelezaji wa maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Institutional master plan) ambao unahusisha utekelezaji wa muundo jumuishi (Integrated System) wa TEHAMA.

Aidha, hadi kufikia Mei 15, 2022, NHC lilishiriki katika uandaaji wa mipango kabambe ya uendelezaji wa maeneo ya Kwala mkoani Pwani na Mji wa Tanzanite wa Mirerani mkoani Manyara. Lakini pia uandaaji wa mpangokina kwa ajili ya uendelezaji wa maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma unaendelea.

Mbali na hayo yote, NHC ili kutimiza azma ya kujenga nyumba za gharama nafuu nchini hususan kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini limeanza kutekeleza mpango wa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kutengeneza vifaa vya ujenzi hususan kokoto, matofali na mabati.

Yapo mafanikio makubwa yaliyofikiwa na NHC katika kutimiza azma hii kwani hadi Mei 15, 2022 lilikuwa limenunua maeneo kwa ajili ya uchimbaji mchanga na uzalishaji wa kokoto pamoja na kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kupata idhini ya utekelezaji wa miradi hiyo.

NHC lina mpango wa kuanza uzalishaji wa vifaa vya ujenzi katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Baadhi ya nyumba za mfano katika mradi wa ujenzi wa nyumba wa Safari City.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, kazi kubwa iliyopo mbele ya Mchechu na timu yake ya NHC kwa sasa ni kufikisha matarajio ya kukusanya shilingi bilioni 105.6 zilizolengwa kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 ambapo hadi Mei 15, 2022 zilikuwa zimekusanywa shilingi bilioni 76.22.

Iwapo malengo ya ukusanyaji mapato yaliyotarajiwa yatafikiwa ifikapo Juni 2022, historia ya NHC itaandikwa kwa mafanikio makubwa kutokana na changamoto mbalimbali zilizokaibali sekta ya nyumba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022.

Mbali ya hayo yote, NHC ya Mchechu inayoendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi, pia imeendelea kufanya ukarabati wa nyumba zake kupitia mpango wa ukarabati unaoendelea kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Tayari nyumba 53 zilizo karika mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Katavi zimeishafanyiwa ukarabati. NHC ilitenga shilingi bilioni nane katika mwaka wa fedha wa 2021/22 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba 350 lakini kiasi kilichotumika kwenye ukarabari wa nyumba 53 ni shilingi bilioni tatu ambazo hadi Mei 15, 2022 ukarabati wake ulikuwa umekamilika.

Ni mpango wa NHC katika mwaka wa fedha wa 2022/23, kukarabati nyumba 180 katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Tabora, Arusha, Kigoma, Morogoro, Lindi, Tanga, Mbeya, Mwanza, Singida na Kagera kwa gharama ya shilingi bilioni nane.

Kazi zilizopangwa na NHC kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ni kukusanya shilingi bilioni 268.03 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato, kuendelea na ujenzi wa mradi wa nyumba 1,000 za gharama nafuu Jijini Dodoma kwa ajili ya kuuza na kupangisha, kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Morocco Square na kuendelea na miradi katika kiwanja nambari 711 Kawe, Golden Premier (GPR-Project) na ujenzi wa nyumba 500 katika eneo la Kawe kwa ajili ya wananchi wa kipato cha kati cha chini ambapo nyumba 360 zitajengwa awamu ya kwanza na nyumba 140 zitajengwa awamu ya pili.

Kazi nyingine zitakazofanywa na NHC katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 ni kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa michoro katika miji ya pembezoni (Satellite Cities) ya Kwala uliopo Ruvu pamoja na Mbezi One Riffle Range uliopo Dar es Salaam na Kawe.

Pia kuendelea na ujenzi wa majengo ya biashara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bukoba, Mwanza, Dodoma, Kahama, Morogoro, Masasi na Lindi.

NHC pia litaendelea na utekelezaji wa miradi ya ukandarasi ikiwemo ujenzi wa majengo ya ofisi za wizara nane Jijini Dodoma, ujenzi wa Jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ujenzi wa majengo matano ya Wakala wa Ununuzi wa Serikali (GPSA), ujenzi wa jengo la Tanzanite Mirerani, ujenzi wa Jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya

Kikwete (JKCI) na miradi mingine itakayojitokeza.

Sambamba na miradi hiyo mikubwa, NHC limelenga kuendelea na usimamizi wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Soko la Kariakoo, kuendelea kutekeleza mpango wa miaka mitano wa ukarabati wa nyumba za shirika unaoishia mwaka 2027 na kununua ardhi ekari 400 katika maeneo mbalimbali ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na akiba ya ardhi.

Aidha, katika kipindi hicho NHC itaanza utekelezaji wa Sera ya Ubia itakayoruhusu Sekta Binafsi kushiriki katika uendelezaji wa maeneo ya shirika, NHC litaendelea na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi hususan kokoto na matofali na pia litaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya nyumba na kulitangaza shirika na Sekta ya Milki nchini kupitia vyombo vya habari.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya