![]() |
Aina ya mdudu anayedaiwa kuzua hofu na usumbufu kwa wakazi wa Tegeta. |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WADUDU wadogo weusi, wanaotambaa na kuruka, wamevamia maeneo kadhaa ya Tegeta hususan Kitongoji cha Nyaishozi na kusababisha hofu na usumbufu kwa wakazi wa maeneo hayo.
Maskani ya wadudu hao yametambulika yapo ndani ya Kiwanda cha Kuzalisha Chakula cha Kuku cha Falcon, kilichopo Tegeta Nyaishozi.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog umebaini kuwa wadudu hao wadogo weusi huruka kutoka ndani ya mahindi yaliyohifadhiwa kiwandani humo kwa ajili ya kutengeneza chakula cha kuku na pia kutoka kwenye chakula cha kuku nyakati za jioni kuanzia majira ya saa 11 hadi nyakati za usiku.
Wadudu hao huingia kwenye makazi ya watu, kwenye chakula kilichopikwa na ambacho hakijapikwa hasa unga na vinywaji. Pia huruka na kutambaa katika nguo na miili ya binadamu na wanapong’ata, husababisha muwasho na uvimbe mdogo.
Baadhi ya wakazi wa Tegeta Nyaishozi waliohojiwa na PANORAMA Blog wameeleza kuwa wadudu hao wanapowauma watoto wadogo huwasababishia homa kali.
“Nadhani umeona wanaruka kutoka wapi hawa wadudu, wanatoka humo kwenye hicho Kiwanda cha Chakula cha Kuku cha Falcon wanakuja kutua kwenye chakula, maji na vinywaji vingine. Hata mkifunga milango mapema jioni wanaingia ndani kwa sababu ni wadogo hivyo ni rahisi kwao kupenya kwenye nyufa za madirisha na milango.
“Wakiuma watoto wadogo wanawasababishia homa kali inayodumu kwa siku tatu au nne kwa hiyo maeneo haya tuna kazi ya kuuguza tu kila siku. Lakini hiyo homa inayosababishwa na hao wadudu inapona baada ya muda huo, sasa hatujui kama.kuna madhara mengine ya kiafya yanayoweza kujitokeza huko mbele,” alisema mjasiliamali anayeuza chakula (mama ntilie) jirani na Baa ya Fair way aliyejitambulisha kwa jina la Bilhuda Alphonce.
James Kapinga, dereva boda boda anayeegesha pikipiki yake pembeni ya kituo cha daladala cha Nyashozi, yeye alisema wadudu hao wanawasababishia usumbufu mkubwa wanapopakia abiria nyakati za jioni kwa sababu wanaingia machoni na masikioni.
“Brother wewe si upo hapa na unawaona, muda huu jua kali lakini jioni ukisimama hapo kwa dakika 10 wanajaa kwenye fulana yako hiyo na wengine wanaingia ndani wanaanza kukuuma. Wakikuuma wanawasha sana na wanaacha kaupele kadogo.
“Kwa wanawake wanaingia kwenye nywele na kwa waliosuka ndiyo huwa wanapata tabu zaidi maana huwa wanapenya ndani ya nywele wanaanza kuwauma, wanajikuna mpaka wanatoka vidonda. Ni wadudu wasumbufu sana wanaingia masikioni, puani na machoni hivyo kama umepakia abiria kumuangusha ni rahisi sana,” alisema Kapinga.
Tanzania PANORAMA Blog imeutafuta uongozi wa Kiwanda cha Falcon bila mafanio baada ya kufika kiwandani hapo zaidi ya mara mbili na kuelezwa kuwa hakuna kiongozi yoyote anayeweza kuzungumzia suala hilo.
Alipotafutwa kwa simu ya kiganjani leo asubuhi mmoja wa viongozi ambaye namba yake iliyepatikana na aliyefahamika kwa jina la Arafa Ally, alisema hawezi kuliongelea suala hilo kwa sababu yeye siyo mtalaamu lakini aliahidi kulifikisha kwa Afisa Rasilimali Watu wa Falcon mara moja ambaye ataitafuta PANORAMA Blog kutoa kauli ya kampuni, jambo ambalo hakulitekeleza.
“Wewe namba yangu nani amekupa kwanza. Mimi ndugu yangu siwezi kusema chochote kuhusu hilo jambo kwa sababu mimi siyo mtaalamu wa hayo mambo. Siwezi kukupa namba yoyote kwa sababu hilo haliruhusiwi kwenye kampuni yetu ila acha nimpe namba yako HR wetu yeye ataongea, anakutafuta sasa hivi subiri dakika mbili tu,” alisema Arafa.
PANORAMA Blog imemtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi ya Mazingura NEMC Samuel Gwamaka bila mafaniko kwani simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na hata akipotumiwa ujumbe wa maandishi kwenye simu yake ya kiganjani pamoja na picha ya mdudu huyo, aliusoma ujumbe huo na kuangalia picha ya mdudu aliyotumiwa lakini aliendelea kukaa kinya bila kujibu chochote.