Sunday, June 22, 2025
spot_img

MFUPA WA UFISADI MGUMU KWA BAYI, TOC

 

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Filbert Bayi anayetuhumiwa kufisadi fedha zinazotolewa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa

RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84

IKIWA ni zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kutangaza kuitisha mkutano mkubwa wa waandishi wa habari kujibu tuhuma za ufisadi ambazo zimekuwa zikielekezwa zaidi kwa Katibu Mkuu, Filbert Bayi, kamati hiyo imeshindwa kutekeleza azma yake hiyo.

Mapema mwezi Mei, Bayi, Makamu Mwenyekiti wa TOC, Henry Tandau, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji na waandishi wa habari wawili, Cosmas Mlekani wa Gazeti la Serikali la Habari Leo na Imani Makongoro wa Kampuni ya Mwananchi Communition Ltd (MCL) waliiambia PANORAMA Blog kuwa wataitisha mkutano mkubwa wa waandishi wa habari kujibu maswali ya tuhuma za ufisadi anazoelekezewa Bayi kwa muda mrefu.

Tandau, ambaye aliongoza kikao cha pili kilichofanyika ofisini kwa Bayi Kibaha na kilichoitishwa na Bayi mwenyewe kwa ajili ya kujibu maswali aliyokuwa ameulizwa na PANORAMA Blog kuhusu tuhuma hizo, alisema maswali yote yaliyoulizwa pamoja na mengine yatakayojitokeza yatajibiwa katika mkutano huo.

Akisaidiwa na waandishi wa habari Mlekani na Imani, walimkataza Bayi kujibu maswali aliyoulizwa na PANORAMA na badala yake walisema mzigo wa tuhuma za Bayi utabebwa na Tandau, Mlekani, Imani na TOC na waliitaka PANORAMA kumfikishia Bayi maswali yote yaliyosalia inayotaka yajibiwe na kwamba yatajibiwa kwa ufasaha moja baada ya jingine, jambo ambalo hadi sasa TOC imeshindwa kulitekeleza.

Katika Mkutano huo ambao Tandau alitumia muda mwingi kujigamba na kutoa kauli zenye mwelekeo wa kutishia kabla ya kujaribu kuanzisha vurugu kwa kukwapua simu ya kiganjani ya PANORAMA Blog huku akihoji kwa ukali ni kwanini ilimrekodi Bayi katika mahojiano ya kwanza, alitulizwa na misuli imara ya PANORAMA Blog na kuonywa kuwa asifikirie kabisa kuanzisha vurugu ya aina yoyote kwa sababu itadhibitiwa kikamilifu na badala yake ajielekeze kumsaidia Bayi kujibu maswali aliyoulizwa.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Henry Tandau


 

Kwa upande mwingine, bado haijafahamika Mlekani na Imani walihusika kwa namna gani kwenye kikao hicho hata kubeba jukumu la kujibu tuhuma za Bayi na TOC na ni kwanini hasa waliitwa kumkingia kifua Bayi katika kikao hicho.

Maswali hayo hayajapata majibu stahiki kwani aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mhariri Mkuu wa Gazeti la Habari Leo, Beda Msimbe alipoulizwa kama mwandishi wake Mlekani ni mjumbe wa TOC au alitumwa na ofisi hiyo ya Serikali kwenda kumsaidia Bayi kubeba mzigo wa tuhuma zake, alisema mwandishi huyo hakutumwa na ofisi na kwamba Gazeti la Habari Leo halina taarifa zozote za yeye kuwepo kwenye kikao hicho.

Niquote hivi, Ofisi, Gazeti la Habari Leo halikumtuma Cosmas Mlekani kwenda huko kujihusisha na mambo hayo na wala halina taarifa zozote za kuwepo kwake huko hivyo Gazeti la Habari Leo halihusiki kwa namna yoyote na jambo hilo,” alisema Msimbe.

Mlekani mwenyewe alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani siku mbili baada ya kuhudhuria kikao hicho kuwa alihudhuria kama nani na kwenye mkutano wa waandishi wa habari wa kujibu tuhuma za Bayi atasimama kumkingia kifua kwa kofia gani, kwanza alisema yupo kanisani atafutwe kuanzia muda wa saa 10.00 jioni na alipotafutwa muda huo, simu yake iliita bila kupokelewa.

Kwa upande wa Imani alipopigiwa kuulizwa ushiriki wake kwenye kikao hicho na kofia atakayotumia kusimama upande wa TOC kumkingia kifua Bayi, kila alipopokea simu aliita helo, helo, helo kuashiria kwamba alikuwa hasikii na  alipotafutwa mapema leo, simu yake iliita bila kupokelewa.

Imani Makongoro

Afisa Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu alipoulizwa leo kuhusu hilo alisema hawezi kulizungumzia isipokuwa mhariri wa Imani ambaye aliahidi kutuma namba yake ya simu ili apigiwe kuulizwa lakini hakutekeleza ahadi yake.

Bayi alipofanya mahojiano ya kwanza na PANORAMA ofisini kwake Kibaha, alisema tuhuma za ufisadi dhidi yake hazina ukweli wowote bali zinatolewa na maadui zake katika sekta ya michezo zikiwa na lengo la kumchafua.

Akijibu tuhuma za kuweka kibondoni fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha michezo, kwa maneno yake mwenyewe, Bayi alisema, “Hapa unavyopaona kuna nini tofauti? Nina mkopo benki ninashindwa kulipa hata wafanyakazi wangu.

“Haya maneno yalianza 2012 lakini ile kunisema sana walinipandisha ‘grade’ ulikuwa wakati wa uchaguzi lakini pamoja na kunichafua nilishinda uchaguzi.

“Olimpafrica ndiyo walioomba fedha IOC kwa ajili ya mradi wa michezo, fedha hizo Zanzibar walipewa kama Dola za Marekani 150,000 na kidogo hivi, huku sisi hatukupata kwa sababu hatukuwa na eneo la kujenga.

“Zanzibar walijenga hivyo wana kituo. Wao Olimpafrica ndiyo waliokuja kuomba hapa kwangu mimi nikawapa ofisi, niliwapa darasa moja ndiyo wameweka ofisi yao hapo hawaleti pesa yoyote, ni kujitolea tu, ninajitolea.

“Hivi sasa ndiyo tumepata kiwanja kipo kigamboni kwa hiyo wakileta fedha tutajenga hicho. Wataamua kama kituo kihamie huko au viwe viwili hapa na huko Kigamboni, kwa hiyo hakuna Shule ya Olimpiki ila kuna huo mradi ambao sisi tunatoa msaada tu.

Na kuhusu madai ya kubadilisha vibao vya shule yake kila wanapokuja wakaguzi kutoka IOC alisema nao ni uzushi mtupu.

Katika hilo nalo, kwa maneno yake mwenyewe alisema, “hakuna mkaguzi yeyote ambaye huwa anatumwa na IOC kuja kukagua miradi ya Olimpiki au Olimpafrica hapa nchini.

                                                                Filbert Bayi

“Nakwambia ni mtu (anamtaja jina) anahangaika kunichafua, hakuna mkaguzi yoyote ambaye huwa anakuja kwa ajili ya kukagua mradi wowote wa Olimpiki au Olimpafrica hapa nchini.

“Umekiona kile kibao, ni cha chuma, wewe unavyoona kinaweza kubadilishwa hicho? Mimi ni Katibu Mkuu nachukuaje fedha kwanza, kuna mwenyekiti, kuna mweka hazina na kuna kamati wananiachia vipi mimi kuchukua fedha hizo?” alisema Bayi.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za yeye na mmoja wa viongozi wa juu wa TOC kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa matumizi mabaya ya fedha za TOC, Bayi alisema huo nao ni uzushi.

“Hivi TAKUKURU wananihoji kwa lipi? fedha ambazo kamati huwa inapokea siyo za hapa nchini zinatoka nje, TOC inapozitumia inalipa kodi, sisi tunalipa kodi, sasa TAKUKURU inakaguaje fedha kutoka nje? Itakuwa ajabu mno eti mimi kuitwa na TAKUKURU kwa ajili ya fedha za TOC na nasema hata siku moja sijawahi kuitwa wala kuhojiwa,” alisema Bayi.

PANORAMA baada ya kuripoti habari hiyo ilimtumia Bayi maswali haya hapa chini kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi kutoka kwake kutokana na kuhusishwa na ufisadi wa fedha za TOC ambayo hata hivyo alikatazwa kuyajibu na Tandau aliyetoa sababu ya katazo hilo kuwa yaliandaliwa na mtu mmoja na kupelekwa Bungeni, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na PANORAMA Blog na kwamba yanambana Bayi kwa kumuelekeza cha kujibu.

Mosi: Kituo cha michezo kilichopo Zanzibar na kilichojengwa kwa fedha za Olimpafrica na kama ulivyoeleza kwenye mahojiano ya awali kuwa kiligharimu zaidi ya Dola za Marekani 150,000 kinafanya shughuli gani? Na je Kituo hicho kinaendeshwa kwa fedha kutoka wapi?

Pili; Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa kuwa kituo cha michezo kilichopo katika Shule ya Filbert Bayi, Kibaha kinaongozwa au kusimamiwa na Sanka Bayi ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu wa TOC na mmiliki wa Shule ya Filbert Bayi. Je, taarifa hizi zina ukweli wowote? Na je, kiongozi/ msimamizi wa kituo hicho alichaguliwa na nani kukisimamia?

Tatu; Katika majibu yako kwenye mahojiano yetu ya awali ulieleza kuwa kiongozi/msimamizi wa kituo hicho anajitolea, halipwi chochote, PANORAMA Blog inaomba kujua IOC na au Olimpafrika hawatumi fedha zozote kwa ajili ya uendeshaji wa kituo hicho hivyo jukumu lote limeachwa kwa Menejimenti ya Shule ya Filbert Bayi? Na iwapo Sanka Bayi ndiye msimamizi wa kituo hicho, Bodi na wewe kama mtendaji mkuu wa TOC hamuoni kuwa kuna mgongano wa kimaslahi?

Nne; Eneo ambalo TOC imelipata hivi karibuni huko Kigamboni, Dar es Salaam kama ulivyoeleza katika mahojiano yetu ya awali kwa ajili ya kituo cha michezo kama kile kilichopo Zanzibar lilipatikaje? Na ama TOC ilinunua na au fedha za kulinunua zilitoka wapi?

Tano, Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa kuwa Kituo cha Zanzibar kinasimamiwa na mtu mwenye uhusiano wa kindugu na Rais wa TOC, Taarifa hizi zina ukweli wowote? Msimamizi wa kituo hicho analipwa au naye anajitolea? Na je hakuna fedha yoyote inayotoka IOC au Olimpafrika kwa ajili ya kusaidia au kuendesha kituo hicho?

Sita; Tanzania PANORAMA Blog inaomba kujua Olimpafrika ina maradi mingapi hapa nchini na inasadia nini katika michezo ya Tanzania?

Saba; PANORAMA Blog inaomba kujua kuhusu Olympic Solidarity na iwapo kuna fedha zozote zinazokuja TOC kama “Athletes Support funds?”

Nane; Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa kuwa TOC ina kiwanja kingine katika Mkoa wa Singida mbali na kile ulichokitaja katika mahojiano ya awali kilichopo Kigamboni. Je viwanja hivi vilipatikana lini?

Kenda; PANORAMA Blog inaomba kujua utaratibu wa utoaji zabuni unaotumiwa na TOC kwa shughuli zinazodhaminiwa na kutolewa mafungu ya fedha na IOC, na je ni kweli kwamba wewe Filbert Bayi au mtu yoyote wa familia yako mmepata kunufaika na zabuni za TOC au shughuli nyingine za manunuzi ?

Kumi; Ni kweli kwamba kanuni za IOC zinazuia na zinatamka kwamba ni kinyume cha maadili kwa kiongozi wa TOC au familia yake kunufaika na zabuni za IOC au shughuli zake nyingine za manunuzi?

Kumi na moja; PANORAMA Blog inaomba kujua shughuli za TOC zinazofadhiliwa na IOC huwa zinapagwa na nani na je ni kweli kwamba shughuli zote za TOC hufanyikia katika Shule ya Filbert Bayi?

Kumi na mbili; Tanzania PANORAMA Blog inaomba kujua kama kuna fedha yoyoye inayotolewa na IOC kusaidia wanariadha katika maandalizi ya michezo ijayo ya Olimpiki ambayo huhusisha misaada ya ufadhili wa kimasomo yaani (Schorlaships).

Kumi na tatu; Inadaiwa kuwa IOC inafadhili Shule ya Filbert Bayi kama Kituo cha Olimpafrica, jambo hili lina ukweli kiasi gani? Na katika hilo inadaiwa iwapo ufadhili huo upo basi shule hiyo inapaswa kuwa mali ya Serikali badala ya mtu binafsi, hili nalo lina ukweli kiasi gani?.

Kumi na nne; Inadaiwa usajili wa Olympafrica hapo shuleni kwako ulifanyika kwa taswira ya rushwa baada ya kiongozi mmoja wa IOC, Raia wa Senegali kuja nchini April, 2019 kisirisiri na kukamilisha usajili huo kisiri kisha kuondoka bila hata Serikali kujua. Jambo hili unalizungumziaje kiongozi?

Kumi na tano; Inadaiwa kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa IOC ni washirika wa kampuni zako wewe Filbert Bayi, je ni kweli kwamba una ushirika wowote wa kibiashara na kiongozi yoyote wa IOC.

Kumi na sita; Inadaiwa kati ya mwaka 2009 hadi 2012 TOC ilipokea Dola za Marekani 680,192 kutoka IOC, wewe kama Katibu Mkuu wa TOC hili unalifahamu?

Kumi na saba; Ni kweli kwamba 2013 hadi 2016 TOC ilipokea Dola za Marekani 523,993. kutoka IOC?

Kumi na nane; Badaaye kati ya 2017 hadi 2020, TOC ilipokea Dola za Marekani 586,132 kutoka IOC, hili nalo lina ukweli wowote?

Kumi na kenda; Zipo taarifa kuwa IOC ilitoa ruzuku ya Covid-19 iliyotakiwa kupewa wanariadha kutokana na kuahirishwa kwa michezo ya Olimpiki ya Tokyo Japan, fedha hizi zilipokelewa na TOC? Na je wanariadha walipewa kama ilivyokusudiwa na IOC?

Makumi mawili; PANORAMA Blog ilimuuliza pia Bayi kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinadaiwa kuripoti taarifa kuwa Januari 20, 2022  Filbert Bayi na baadhi ya viongozi wenzako katika TOC mliteuliwa katika ANOCA, Taarifa hizi za kuteuliwa kwenu zilikuwa za kweli?

 

Cosmas Mlekani

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya