Tuesday, December 24, 2024
spot_img

MAJALIWA AWAPA NENO WASAIDIZI WAKE

                                            Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusimamia na kuratibu kikamilifu miradi iliyoko kwenye mikoa, wilaya na halmashauri zilizo kwenye sekta wanazosimamia.

Agizo hilo alilitoa Mei, 31, 2022 jijini Dodoma katika kikao baina yake na Waziri wa TAMISEMI, naibu mawaziri, katibu mkuu, naibu makatibu wakuu na wakurugenzi na wakuu wa taasisi za wizara hiyo.

“Nendeni mkasimamie uratibu wa miradi kwenye mikoa, wilaya na halmashauri. Tambueni miradi iliyoko ni mingapi, mingapi iko vizuri, mingapi inasuasua kisha toeni taarifa kwa katibu mkuu,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, aliwapongeza kwa kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa kwa fedha zilizotolewa chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambayo kwenye elimu ilichukua muda mfupi sana kukamilika.

“Kama tuliweza kusimamia miradi ya fecha za UVIKO-19 na kuikamilisha chini ya miezi mitatu, ni kwa nini sasa hivi tushindwe kufanya hivyo kwa miradi mingine? Kuna miradi ilianza kujengwa kabla fedha za UVIKO-19 hazijatolewa, lakini hadi sasa haijakamilika. Ni kwa nini hali iko hivyo? mkurugenzi jiulize, ulipopewa mradi, ulipaswa kuisha lini? waziri na naibu mawaziri simamieni hilo na mfanye tathmini,” alisema.

Akizungumzia mgawanyo wa majukumu kwa wakurugenzi wa wizara na wakuu wa idara, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wakae ofisini na kutoa maamuzi ili kazi nyingine zifanyike badala ya kuweka msisitizo kwenye safari.

“Kaeni ofisini na kufanya maamuzi, hizo safari wapeni wasaidizi wenu na wakirudi wawape mrejesho.

“Katibu mkuu na naibu makatibu wakuu fuatilieni utendaji wa wakuu wa idara. Kuwe na utaratibu wa kuondoka, siyo mtu anatimka tu kwenda mkoani au wilayani,” alisema.

Aliwahimiza waandae mipango yao ya kazi kwa kufuata Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambayo imeainisha kila sekta na kutaja miradi inayotakiwa kusimamiwa kwenye mikoa, wilaya, halmashauri na kata nchini.

“Nilishaelekeza kila mkuu wa idara apate nakara ya Ilani ya CCM na awe nayo mezani kwake. Tunatakiwa tuipitie na tuainishe mpango kazi kila mmoja kulingana na sekta yake,” alisema.

Kuhusu matumizi ya fedha za umma, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwenye maeneo mengi alikopita amebaini kuwa matumizi ya fedha siyo mazuri na akasisitiza wasimamie eneo hilo ili kupata thamani halisi ya fedha kwenye miradi inayotekelezwa na Serikali.

Aliwataka wajiepushe na tamaa ya kutaka kuhusika kwenye manunuzi ya vifaa vya miradi hiyo. 

“Tuna kamati za ujenzi katika kila kata. Iweje wao wafanye manunuzi wakati kamati zipo na zinasimamia? Wakuu wa idara mjiondoe kwenye nafasi ya kutuhumiwa. Hebu cheki kanuni zenu kuhusu kamati za ujenzi na masuala ya manunuzi zinasemaje,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

 

 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya