RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
TIMU ya kuchunguza uwepo wa dawa bandia za kuua wadudu waharibifu wa zao la pamba wanayouziwa wakulima wa zao hilo mkoani Simiyu, kesho inatarajiwa kukabidhi ripoti yake kwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Simiyu, David Kafulila.
Tamko hilo limetolewa jana na RC Kafulila alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Meatu waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ambaye yupo katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu.
Katika mkutano huo, wananchi wa Meatu walitoa malalamilo yao kuwa Bodi ya Pamba inasambaza mbegu bandia kwa wakulima, ambazo hazina uwezo wa kuua wadudu waharibifu wa zao hilo hivyo kuathiri mavuno.
“Dawa za pamba zilizosambazwa msimu huu ni feki. Hata uwachukue wadudu wenyewe uwaweke kwenye chupa ya dawa ya pamba hawafi” walisema wakulima kwenye mkutano huo wa Katibu Mkuu Chongolo.
Akizungumza RC Kafulila, aliwapongeza wakulima kwa kuitikia wito wa kulima kwa bidii zao la pamba na aliwahakikishia kutatuliwa kwa tatizo la dawa bandia ya kuua wadudu waharibifu wa zao la pamba.
“Kwanza ninawapongeza wakulima kwa mwitikio mkubwa msimu huu kiasi ambacho mwelekeo unaonesha tutavuna zaidi ya kilo milioni 200 kutoka kilo milioni 82 msimu uliopita kwa mujibu wa makadirio ya Bodi ya Pamba.
“Kilo zaidi ya milioni 200 ni rekodi ya kwanza tangu mkoa uzaliwe. Bei ya pamba msimu huu itavunja rekodi ya zaidi miongo mitatu lakini niwahakikishie kwamba timu niliyounda kutathimini ukubwa wa tatizo la dawa feki za pamba itanikabidhi ripoti Ijumaa, Juni, 3, 2022.
“Na niwahakikishie, Serikali itachukua hatua kali dhidi ya kampuni zilizoiuzia bodi dawa feki kisha bodi kusambaza kwa wakulima kwani kosa hilo ni sawa na uhujumu uchumi,” alisema RC Kafulila