![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo (DC), Zainab Abdallah |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
HALI si shwari katika Kijiji cha Fukayosi, Wilaya ya Bagamoyo baada ya baadhi ya wenyeji wa kijiji hicho kuanza kuyakimbia makazi yao kwa kuwahofia wananchi waliouziwa mashamba na viwanja kijijini humo wanaodaiwa kutapeliwa fedha na maeneo waliyouziwa.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimeeleza kuwa Kampuni ya VXP for Youth Development Ltd iliyokuwa ikiuza mashamba na viwanja katika Kijiji cha Fukayosi, Wilaya ya Bagamoyo kati ya mwaka 2016 na 2017 imewatapeli mamilioni ya fedha wananchi iliowauzia viwanja na mashamba.
Kwa mujibu taarifa hizo, baadhi ya wenyeji wa Kijiji cha Fukayosi wanaotajwa kushirikiana na kampuni hiyo katika uuzaji wa mashamba na viwanja wamekimbia makazi kwa kuhofia hasira za wananchi waliotapeliwa fedha zao na Kampuni ya VXP for Youth Development Ltd.
PANORAMA Blog imepata taarifa kuwa wananchi takriban 70 kutoka maeneo mbalimbali nchini walinunua mashamba katika Kijiji cha Fukayosi kupitia Kampuni ya VXP for Youth Development Ltd lakini kampuni hiyo baada ya kukusanya fedha za wananchi hao ilianza kuwazungusha kuwapatia maeneo yao kabla ya kutoweka na kuwaacha wakiwa hawajui la kufanya.
Baadhi ya nyaraka za mgogoro huo ambazo PANORAMA Blog imeziona zinaonyesha kuwa, Kampuni ya VXP for Youth Development Ltd iliyokuwa na dhamana ya Serikali ya Kijiji kupima na kuuza mashamba na viwanja katika Kijiji cha Fukayosi, ililipwa na wananchi hao na kuwaonyesha maeneo waliyolipia lakini muda mfupi baadaye ilitoa taarifa ya kubadilishwa kwa maeneo iliyokuwa imewapatia.
Moja ya nyaraka zilizoonwa na PANORAMA Blog inayoelezea mgogoro huo inasomeka; “baadhi ya wateja walioonyeshwa maeneo yao lakini baadaye Kampuni ya VXP for Youth Development Ltd ilitoa taarifa kwa wateja wake kuwa maeneo iliyowapa yamebadilishwa hivyo wasubiri watapewa maeneo mengine.
“Wapo baadhi walioonyeshwa maeneo mapya lakini kutokana na mwenendo wa Kampuni ya VXP for Youth Development Ltd wa kutoaminika, hawana uhakika na umiliki wa maeneo hayo na wapo baadhi walioahidiwa kuonyeshwa maeneo mapya tangu mwaka 2017 lakini hadi sasa ahadi hiyo haijatekelezwa na kampuni hiyo.”
Inadaiwa kuwa wananchi waliolipia mashamba na viwanja katika Kijiji cha Fukayosi sasa wameamua kupambana kupata haki yao jambo ambalo limeibua hofu kwa wenyeji wa kijiji hicho.
“Unajua hofu inatokea wapi? Huwezi kujua moyoni kwa mtu kuna nini na hasa anapokuwa anapigania haki yake. Maisha yenyewe kwa sasa ni magumu sasa mtu hawezi kukubali kudhulumiwa mamilioni yake hivi hivi tu. Wanakuja sana kufuatilia maeneo yao lakini wenye kampuni sasa hawaonekani, wamekuwa wanakuja na kuondoka kimya kimya lakini ni watu wenye uwezo tu, hilo ndilo linaloogopesha.
“Baadhi ya wenzetu waliokuwa pamoja na hiyo kampuni walitishwa na hiyo tabia ya hao jamaa maana walau wangefanya fujo ingeeleweka lakini watu wakimywa ni wabaya sana, mtu umemwibia au kumdhulumu lakini anakuangalia tu, inatisha maana huwezi kujua. Sasa wenzetu wameogopa, wamekimbia.
“Hatujui sasa hatma ya hili jambo ni nini lakini nasikia wamekwishafikisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya,” alisema mkazi mmoja wa Kijiji cha Fukayosi aliyezungumza na PANORAMA Blog.
Jitihada za kuupata uongozi wa Kijiji cha Fukayosi kuzungumzia suala hilo hazijaweza kufanikiwa mara moja na alipotafutwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallah kuhusu suala hilo, hakijibu lolote.
PANORAMA Blogi imeitafuta Kampuni ya VXP for Youth Development Ltd ili kupata kauli yake kuhusu tuhuma inazoelekezewa pasipo mafanikio kwani mahali zilipokuwa ofisi zake, eneo la Kwa Mkolombe, Gongo la Mboto ofisi hiyo ilikutwa imefungwa.
PANORAMA Blog inaendelea kuwatafuta viongozi wa Wilaya ya Bagomoyo na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi ili kuzungumzia sakata hilo.
Hao wanchi wa huko ni matapeli wakishrikiana na matapeli akina ibra kuuza maeneo ya watu na kutoa mabango yaliyowekwa