RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC) jana iliitisha Tanzania PANORAMA Blog kuhusu hatua yake ya kuripoti habari zinazomuhusisha Katibu Mkuu wa kamati hiyo, Filbert Bayi na ufisadi wa fedha zinazotolewa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kwa ajili ya kusaidia na kuendeleza shughuli za michezo hapa nchini.
Sambamba na hilo, TOC iliwatumia waandishi wa habari wa Serikali wa magazeti ya Habari Leo na Daily News kujaribu kuizuia PANORAMA Blog kuendelea kuripoti habari hizo.
Bayi, ambaye jana aliiita PANORAMA Blog ofisini kwake Kibaha kwa ajili ya kujibu maswali iliyomuuliza, ilimkuta akiwa na watu wengine saba aliosema amewaita wamsaidie kujibu maswali hayo kwa sababu ni watu wa karibu yake na wanaofahamu kinachoendelea ndani ya TOC.
Miongoni mwa watu hao, Bayi alimtambulisha Makamu Mwenyekiti wa TOC, Henry Tandau, waandishi wa habari wawili aliosema wanaandikia magazeti ya Daily News na Habari Leo ambao walishirikiana kwa karibu na Tandau kumkingia kifua Bayi.
Akijibu kwa niaba ya Bayi, Tandau ambaye alitumia dakika kadhaa kujigamba kuwa nguli wa uandishi wa habari aliyepata kufanya kazi na waandishi wa habari wanaoheshika nchini na wenye madaraka makubwa Serikalini kwa sasa, aliilaumu PANORAMA Blog kumuuliza maswali hayo Bayi kwa kile alichosema yanaelekeza cha kujibu na yameandaliwa na mtu mmoja na kupelekwa Bungeni, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na PANORAMA Blog.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Henry Tandau |
Tandau alimtuhumu moja kwa moja mmoja wa waliopata kuwa viongozi wa chama cha riadha (jina lake tunalihifadhi kwa sababu hajapatikana kuzungumza) kuhusika kutoa taarifa za TOC huku akisisitiza kuwa ndiye huyo huyo aliyefikisha madai ya ufisadi wa Bayi kwa PANORAMA Blog.
Alisema mtu huyu alipeleka madai hayo BMT kwa maandishi na BMT ilipeleka maandishi hayo na jina kwa TOC huku ikitaka ipatiwe maelezo kwa maandishi kuhusu yale yote yaliyotuhumiwa na mtu huyo.
Tandau alishinikiza PANORAMA Blog kukubali kuwa mtu huyo ndiye aliyeifikisha taarifa hizo huku akiitaka ibebe ujumbe wa kumfikisha na wakati waandishi waliokuwapo nao wakijitahidi kusaidia kulainisha mambo, lakini Tanzania PANORAMA iliwapuuza kwa kutowasikiliza na kujikita zaidi kwa Tandau
Aidha, Tandau alisema waliitwa na Bunge kwenda kutoa maelezo ya tuhuma hizo ambako waliwasilisha andiko lililoshiba kuhusu mwenendo, shughuli za TOC na ripoti ya fedha na baada ya kupokelewa na Bunge na kupitiwa, liliwasifu kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Alisema maswali aliyoulizwa Bayi hatayajibu bali TOC itaanzaa mkutano mkubwa na waandishi wa habari kwa ajili ya kujibu maswali yote aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog.
Maswali ambayo PANORAMA Blog ilimuuliza BAYI na ambayo Tandau anadai yameandaliwa na mtu mmoja na kupelekwa Bungeni, BMT na PANORAMA Blog na ambayo anadai yanambana Bayi kwa kumuelekeza cha kujibu ni haya hapa;
Swali la kwanza lilihoji; Kituo cha michezo kilichopo Zanzibar na kilichojengwa kwa fedha za Olimpafrica na kama ulivyoeleza kwenye mahojiano yetu ya awali kuwa kiligharimu zaidi ya Dola za Marekani 150,000 kinafanya shughuli gani? Na je Kituo hicho kinaendeshwa kwa fedha kutoka wapi?
Swali lililofuata hili hapa; Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa kuwa kituo cha michezo kilichopo katika Shule ya Filbert Bayi, Kibaha kinaongozwa au kusimamiwa na Sanka Bayi ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu wa TOC na mmiliki wa Shule ya Filbert Bayi. Je, taarifa hizi zina ukweli wowote? Na je, kiongozi/ msimamizi wa kituo hicho alichaguliwa na nani kukisimamia?
Na katika majibu yako kwenye mahojiano yetu ya awali ulieleza kuwa kiongozi/msimamizi wa kituo hicho anajitolea, halipwi chochote, PANORAMA Blog inaomba kujua IOC na au Olimpafrika haitumi fedha zozote kwa ajili ya uendeshaji wa kituo hicho hivyo jukumu lote limeachwa kwa Menejimenti ya Shule ya Filbert Bayi? Na iwapo Sanka Bayi ndiye msimamizi wa kituo hicho, Bodi na wewe kama mtendaji mkuu wa TOC hamuoni kuwa kuna mgongano wa kimaslahi?
Bayi aliulizwa pia kuwa; Eneo ambalo TOC imelipata hivi karibuni huko Kigamboni, Dar es Salaam kama ulivyoeleza katika mahojiano yetu ya awali kwa ajili ya kituo cha michezo kama kile kilichopo Zanzibar lilipatikaje? Na ama TOC ilinunua na au fedha za kulinunua zilitoka wapi?
Swali la nne lilihoji; Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa kuwa Kituo cha Zanzibar kinasimamiwa na mtu mwenye uhusiano wa kindugu na Rais wa TOC, Taarifa hizi zina ukweli wowote? Msimamizi wa kituo hicho analipwa au naye anajitolea? Na je hakuna fedha yoyote inayotoka IOC au Olimpafrika kwa ajili ya kusaidia au kuendesha kituo hicho?
Bayi aliulizwa pia; Tanzania PANORAMA Blog inaomba kujua Olimpafrika ina maradi mingapi hapa nchini na inasadia nini katika michezo ya Tanzania?
Swali na sita lilihoji kuhusu “Olympic Solidarity” na iwapo kuna fedha zozote zinazokuja TOC kama “Athletes Support funds?”
Aidha, Bayi aliulizwa; Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa kuwa TOC ina kiwanja kingine katika Mkoa wa Singida mbali na kile ulichokitaja katika mahojiano ya awali kilichopo Kigamboni. Je viwanja hivi vilipatikana lini?
INAENDELEA..