Tuesday, December 24, 2024
spot_img

FILBERT BAYI ADAIWA KUFISADI FEDHA ZA TOC, YEYE AKANUSHA ASEMA ANACHAFULIWA

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi

 RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

KATIBU Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Filbert Bayi anadaiwa kuhusika na ufisadi wa fedha zinazotolewa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kwa ajili ya maendeleo ya mchezo wa riadha hapa nchini.

Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog kutoka kwa wadau wa mchezo wa riadha walio karibu wa TOC zimedai kuwa, Bayi ambaye sasa amekuwa kiongozi wa kamati hiyo kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akitia kibindoni kwake fedha zinazotolewa na IOC ikiwa ni pamoja na mradi wa michezo ulio chini ya Olimpafrica.

Katika mlolongo wa tuhuma zilizotolewa, inadaiwa IOC ilitoa fedha za ujenzi wa shule za michezo kwa nchi mbili za Afrika, moja ya nchi zilizonufaika na fedha hizo ni Tanzania lakini shule iliyojengwa ipo Dole,  Zanzibar huku Tanzania Bara ikiwa haipo.

Kwamba, IOC imekuwa ikituma wakaguzi kwa ajili ya kukagua mwenendo na maendeleo ya shule hizo lakini kila wanapotua nchini, vibao vya kuitambulisha Shule ya Fibert Bayi hubadilishwa na kuwekewa vibao vingine mpaka wakaguzi hao wanapoondoka ndipo hurudishwa vibao vyake vya awali.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi akitoa ufafanuzi wa madai mbalimbali anayoelekezewa kuhusu fedha zinazotolewa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na Olimpafrica kwa Tanzania nje ya geti la Shule ya Filbert Bayi, leo.  Pembeni yake ni mwandishi wa habari wa Tanznania PANORAMA Blog, Charles Mullinda.



Akizungumzia madai hayo leo ofisini kwake Kibaha, Bayi alisema hayana ukweli wowote bali yanatolewa na maadui zake katika sekta ya michezo yakiwa na lengo la kumchafua.

Akijibu kuhusu madai ya kuweka kibondoni fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha michezo, kwa maneno yake mwenyewe, Bayi alisema, “Hapa unavyopaona kuna nini tofauti? Nina mkopo benki ninashindwa kulipa hata wafanyakazi wangu.

“Haya maneno yalianza 2012 lakini ile kunisema sana walinipandisha ‘grade’ ulikuwa wakati wa uchaguzi lakini pamoja na kunichafua nilishinda uchaguzi.

“Olimpafrica ndiyo walioomba fedha IOC kwa ajili ya mradi wa michezo, fedha hizo Zanzibar walipewa kama Dola za Marekani 150,000 na kidogo hivi, huku sisi hatukupata kwa sababu hatukuwa na eneo la kujenga.

“Zanzibar walijenga hivyo wana kituo. Wao Olimpafrica ndiyo waliokuja kuomba hapa kwangu mimi nikawapa ofisi, niliwapa darasa moja ndiyo wameweka ofisi yao hapo hawaleti pesa yoyote, ni kujitolea tu, ninajitolea.

“Hivi sasa ndiyo tumepata kiwanja kipo kigamboni kwa hiyo wakileta fedha tutajenga hicho. Wataamua kama kituo kihamie huko au viwe viwili hapa na huko Kigamboni, kwa hiyo hakuna Shule ya Olimpiki ila kuna huo mradi ambao sisi tunatoa msaada tu,” alisema Bayi.

Akizungumzia madai ya kubadilisha vibao vya shule yake kila wanapokuja wakaguzi kutoka IOC alisema nao ni uzushi mtupu.

Alisema, “hakuna mkaguzi yeyote ambaye huwa anatumwa na IOC kuja kukagua miradi ya Olimpiki au Olimpafrica hapa nchini.

“Nakwambia ni mtu (anamtaja jina) anahangaika kunichafua, hakuna mkaguzi yoyote ambaye huwa anakuja kwa ajili ya kukagua mradi wowote wa Olimpiki au Olimpafrica hapa nchini.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi akionyesha ofisi aliyotoa msaada kwa Olimpafrica iliyopo ndani ya eneo la shule yake



“Umekiona kile kibao, ni cha chuma, wewe unavyoona kinaweza kubadilishwa hicho? Mimi ni Katibu Mkuu nachukuaje fedha kwanza, kuna mwenyekiti, kuna mweka hazina na kuna kamati wananiachia vipi mimi kuchukua fedha hizo?” alisema Bayi.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za yeye na mmoja wa viongozi wa juu wa TOC kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa matumizi mabaya ya fedha za TOC, Bayi alisema huo nao ni uzushi.

“Hivi TAKUKURU wananihoji kwa lipi? fedha ambazo kamati huwa inapokea siyo za hapa nchini zinatoka nje, TOC inapozitumia inalipa kodi, sisi tunalipa kodi, sasa TAKUKURU inakaguaje fedha kutoka nje? Itakuwa ajabu mno eti mimi kuitwa na TAKUKURU kwa ajili ya fedha za TOC na nasema hata siku moja sijawahi kuitwa wala kuhojiwa,” alisema Bayi.

Katibu Mkuiu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wa Tanzania PANORAMA Blog (hawapo pichani) kuhusu madai mbalimbali anayoekekezewa.



Tanzania PANORAMA Blog inaandaa makala maalumu itakayochambua kwa kina mwenendo wa mambo ndani ya TOC.    

Nyingine Zinazohusiana na Hii

2 COMMENTS

  1. Majibu yaliyonyooka kabisa bila kupinda Linda. Hongera Legend Bayi kwa utendaji uliotukuka katika uongozi wako.

  2. Majibu yaliyonyooka kabisa bila kupinda pinda. Hongera Legend Bayi kwa utendaji uliotukuka katika uongozi wako.REPLY

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya