Monday, June 23, 2025
spot_img

RPC KINGAI AMKANA INSPEKTA ZAWADI, YEYE AELEZA KILA KITU

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

SAKATA la Mchina anayemiliki duka kubwa linalouza vifaa vya nyumbani, limechukua sura npya baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai kumkana Zawadi Mpumilwa anayedaiwa kuwa ni Askari Polisi wa Kituo cha Oysterbay mwenye cheo cha Inspekta kuwa siyo askari wa kituo hicho. 

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog mwishoni mwa wiki iliyopita kuhusu Zawadi kupigiwa simu na mfanyabiashara raia wa China anayetambulika kwa jina la Biao Sun akimuomba aingilie kati kuzuia waandishi wa habari kufanya mahojiano naye,  Kamanda Kingai alisema kwa ufupi kuwa jambo hilo halipo.

Alisema hakuna polisi anayepaswa kupigiwa simu na mfanyabiashara anapofikiwa na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kwa kujibu maswali waliyonayo na alipoelezwa kuwa tukio hilo limetokea hivi karibuni likimuhusisha Zawadi  na Biao Sun, Mchina anayemiliki Supermarket inayofahamika kwa jina la China Town, Kamanda Kingai alisema Kituo cha Polisi Oysterbay hakuna askari anayeitwa Zawadi.

“Jambo kama hilo halipo, hakuna jambo kama hilo… hakuna askari anayeitwa Zawadi katika Kituo cha Oysterbay,” alisema kwa sauti thabiti Kamanda Kingai.

Hata hivyo, wakati Kamanda Kingai akieleza hayo, Zawadi mwenyewe alizungumza na Tanzania PANORAMA Blog na kueleza kwa kina jinsi alivyofahamiana na Biao Sun na sababu iliyomfanya ampigie simu baada ya kufikiwa na waandishi wa habari kwa ajili ya mahojiano.

Zawadi alisema ni askari polisi na kituo chake cha kazi ni Oysterbay na kwamba wawekezaji na wananchi wanazo simu za polisi na wanapoona mtu ambaye hawamwelewi siyo kosa kupiga simu polisi kutoa taarifa.

“Mimi nilimfahamu huyo Mchina kupitia kwa mwandishi mwenzenu anayeitwa Mwang’onda. Ndiye aliyenifahamisha kwake. Hapa mjini kuna matapeli wengi sana siku hizi, wapo wanaojifanya usalama wa taifa, wengine TBS na wanakwenda kwa wawekezaji kwa malengo mabaya na wakiombwa vitambulisho huwa wanakimbia.

“Aliponipigia alisema hawaelewi na amewaomba vitambulisho hamjatoa ndiyo nikamwambia anipe huyo askari aliyekuwa amewasindikiza niongee naye nikijua kuwa kama siyo askari lazima angekataa kuongea na mimi.

“Nilipoongea naye nilimtambua moja kwa moja kuwa Inspekta Danny na nikamwambia ampe simu huyo Mchina, nikamwambia huyo ni msaidizi wangu hivyo awape ushirikiano na ajibu maswali yenu waandishi.

“Lakini badaaye nilipompigia Inspekta Danny aliniambia kuwa huyo Mchina alikataa kujibu maswali yenu.

“Siyo kosa kwa askari kutoa ulinzi kwa raia wakiwemo waandishi na wawekezaji na ninyi mlifanya vizuri kuomba ulinzi wa askari kwa sababu mngeenda peke yenu mngeweza kupigwa mkaumizwa, kuja kujulikana ni watu wema mmeishaumia.

“Nilimshauri Danny kuwa kama huyo Mchina amekataa kujibu maswali yenu basi nyie mwandikieni maswali kwa maandishi mumtumie kwa njia ya posta au vyovyote ili kuwe na ushahidi kuwa alipewa maswali akakataa kuyajibu hapo kunakuwa na ushahidi,” alisema Zawadi.

Awali Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa mke wa Sun ambaye ni raia wa China analalamikiwa na wafanyakazi wa China Supermarket hapendi kuitwa jina lake na badala yake anataka aitwe boss na anapotokea mfanyakazi kumuita jina lake humshambulia kwa maneno makali yasiyotamkika.

“Changamoto ni kubwa sana kazini kwetu na tuseme siyo changamoto ni matatizo. Tatizo kubwa lipo kwa bosi mama, yeye kwanza hapendi kuitwa jina lake anataka aitwe bosi. Ukikosea kumuita jina lake unayaoga matusi.

“Mbali na hilo ikitokea wamekuja watu wa Serikali kufanya ukaguzi maana wanakuja kila mara pale kwa sababu kuna maghumashi mengi sana. Sasa wakija huwa kuna mambo tunatakiwa kuyaweka sawa haraka, ikitokea umechelewa yaani bosi mama atakushambulia kwa matusi makubwa makubwa bila kujali wengine ni baba na mama zetu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao jina lake kapuni.

Katika madai yao mengine, wameleeza kuwa Supermarket hiyo, baadhi ya bidhaa zinazouzwa haziwekewi bei (price tag) kama ulivyo utaratibu wa kawaida na badala yake wateja hukutana na bei ya bidhaa kwenye kaunta ya malipo.

“Kuna bidhaa humu ndani nyingi huwa haziwekewi bei kama ulivyo utaratibu wa kawaida na Supermarket nyingi zinafuata utaratibu huo. Hizo bidhaa hatujui huwa anazitoa wapi tunachojua zinatoka nje ya nchi na wala haijulikana kama zinalipiwa kodi kwa sababu mteja anakutana na bei kaunta na anayotajiwa inatokana kichwani mwa bosi mama.

“Bidhaa zilizoisha muda wa matumizi humu haziondolewi, zinashushwa bei wateja wanauziwa. Hizo ni pamoja na vyakula na bidhaa nyingine za ndani. Sasa wakija watu wa Serikali ni kukimbizana kuweka mambo sawa na ndiyo hapo tunaponyanyasika hasa,” amesema.

Aidha wamedai zaidi kuwa mmiliki wa Supermarket hiyo amekuwa akijenga vyumba vya biashara katika eneo analomiki na kupangisha wafanyabiashara wengine kinyume cha taratibu na inapotokea watu wa Manispaa wanamfika kufanya ukaguzi, wakiondoka huanza kuwafokea wafanyakazi wake kwa kutoa siri zake.

“Huyu jamaa ni Mchina kabisa na mkewe ni Mchina lakini hapa ni kwake. Hili ni eneo lake na hivyo vyumba vya biashara vyote unavyoviona yeye ndiyo kavipangisha na analipwa kodi. Kuna baadhi ya watu wa Serikali wanajua hiyo issue hivyo huwa wanakuja kumtingisha. 

“Wakiondoka anatugeuzia kibao wafanyakazi anatutukana ile mbaya eti sisi tunatoa siri zake wakati siyo kweli, sisi tumekuja kwake kutafuta mkate wa watoto wetu hayo maghumashi yake hayatuhusu maana hata ukisema umripoti ni kazi bure maana anajuana na watu wengi wakubwa.

“Sasa uvumilivu huwa una mwisho, majuzi katutukana sana mpaka anatutukania wazazi wetu, tumeona bora hili sasa tulisema ili mamlaka za juu waje waangalie na kuchunguza hapa na watusikilize na sisi wafanyakazi kilio chetu,” alisema.

Aidha, PANORAMA Blog iliripoti zaidi kuwa,  Biao Sun ni mjeuri.

Kwamba Sun alikataa kujibu tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wafanyakazi dhidi yake pamoja na mkewe za kuwanyanyasa na kuwatolea maneno machafu huku akitaja baadhi nyadhifa za viongozi wa taasisi kuwa ndiyo wana uwezo wa kuzungumza naye.

Hayo yalitokea mbele ya Afisa wa Polisi ambaye ni Mratibu wa Usalama wa Kata ya Mikocheni mwenye cheo cha Inspekta.

PANORAMA Blog ililazimika kwanza kufika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mikocheni kueleza nia yake ya kufika kwenye Supermarket hiyo kufanya mahojiano ikizingatia agizo lililotolewa mwaka jana na uongozi wa Kata ya Mikocheni linalowataka waandishi wa habari kuripoti katani hapo kueleza lengo la kufika kwao eneo hilo kabla ya kufanya kazi yoyote ya kiuanahabari

Sun baada ya kuelezwa lengo la waandishi wa PANORAMA waliokuwa chini ya usimamizi wa Afisa Polisi, Mratibu wa Usalama wa Kata alisema hawezi kuzungumza chochote kuhusu madai hayo kisha alichukua simu yake ya kiganjani, akapiga kushtaki kwa afisa wa juu wa Polisi wa Kituo cha Oysterbay ambaye jina lake tunalifahadhi kwa sasa.

Baada ya kuzungumza na simu hiyo kwa muda mfupi. Sun alimpitia simu Mratibu wa Ulinzi wa Kata ya Mikocheni ambaye katika mazungumzo yake alisikika kwanza akijitambulisha na kueleza sababu ya kuwepo katika Supermarket hiyo.

Baada ya mazungumzo hayo mratibu huyo alirudisha simu kwa Sun ambaye alimweleza afisa huyo kuwa hayupo tayari kuhojiwa peke yake kwa sababu jirani zake ambao pia ni raia wa China wanaomiliki Supermarket kama yeye eneo hilo wana tuhuma zinazorandana na za kwake hivyo wanapaswa kuhojiwa wao kwanza.

Sun alimuhoji Mratibu wa Usalama wa Kata iwapo yeye ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Waziri au mtu mwenye wadhfa mkubwa serikali kiasi cha kuthubutu kufika katika Supermarket yake na kusisitiza kuwa hayupo tayari kujibu madai yoyote ya wanafanyakazi kwani yeye ana uhuru wa kufanya anachoona kinafaa.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya