RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
BIAO SUN, Mfanyabiashara Raia wa China anayemiliki duka kubwa linalouza mahitaji ya nyumbani (Supermarket) linalofahamika kwa jina la China Town, lililopo eneo la Migombani, Kata ya Mikocheni mkoani Dar es Salaam ni mjeuri.
Sun amekataa kujibu tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wafanyakazi dhidi yake pamoja na mkewe za kuwanyanyasa na kuwatolea maneno machafu huku akitaja baadhi nyadhifa za viongozi wa taasisi kuwa ndiyo wana uwezo wa kuzungumza naye.
Hayo yametokea leo baada ya PANORAMA Blog kufika katika Supermarket ya China Town ikiwa imeambatana na Afisa wa Polisi ambaye ni Mratibu wa Usalama wa Kata ya Mikocheni mwenye cheo cha Inspekta kwa ajili ya kufanya mahojiano na Sun.
PANORAMA Blog ililazimika kwanza kufika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mikocheni kueleza nia yake ya kufika kwenye Supermarket hiyo kufanya mahojiano ikizingatia agizo lililotolewa mwaka jana na uongozi wa Kata ya Mikocheni linalowataka waandishi wa habari kuripoti katani hapo kueleza lengo la kufika kwao eneo hilo kabla ya kufanya kazi yoyote ya kiuanahabari
Sun baada ya kuelezwa lengo la waandishi wa PANORAMA waliokuwa chini ya usimamizi wa Afisa Polisi Mratibu wa Usalama wa Kata hiyo, alisema hawezi kuzungumza chochote kuhusu madai hayo kisha alichukua simu yake kiganjani, akapiga kushtaki kwa afisa wa juu wa Polisi wa Kituo cha Oysterbay ambaye jina lake tunalifahadhi kwa sasa.
Baada ya kuzungumza na simu hiyo kwa muda mfupi. Sun alimpitia simu Mratibu wa Ulinzi wa Kata ya Mikocheni ambaye katika mazungumzo yake alisikika kwanza akijitambulisha na kueleza sababu ya kuwepo katika Supermarket hiyo.
Baada ya mazungumzo hayo mratibu huyo alirudisha simu kwa Sun ambaye alimweleza afisa huyo kuwa hayupo tayari kuhojiwa peke yake kwa sababu jirani zake ambao pia ni raia wa China ambao pia wana Supermarket eneo hilo wana tuhuma zinazorandana na za kwake hivyo wanapaswa kuhojiwa wao kwanza.
Sun alimuhoji Mratibu wa Usalama wa Kata iwapo yeye ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Waziri au mtu mwenye wadhfa mkubwa serikali kiasi cha kuthubutu kufika katika Supermarket yake na kusisitiza kuwa hayupo tayari kujibu madai yoyote ya wanafanyakazi kwani yeye ana uhuru wa kufanya anachoona kinafaa.
Hivi karibuni, PANORAMA Blog iliripoti kuwa mke wa Sun ambaye pia ni raia wa China hapendi kuitwa jina lake na badala yake anataka aitwe boss na anapotokea mfanyakazi kumuita jina lake humshambulia kwa maneno makali yasiyotamkika.
“Changamoto ni kubwa sana kazini kwetu na tuseme siyo changamoto ni matatizo. Tatizo kubwa lipo kwa bosi mama, yeye kwanza hapendi kuitwa jina lake anataka aitwe bosi. Ukikosea kumuita jina lake unayaoga matusi.
“Mbali na hilo ikitokea wamekuja watu wa Serikali kufanya ukaguzi maana wanakuja kila mara pale kwa sababu kuna maghumashi mengi sana. Sasa wakija huwa kuna mambo tunatakiwa kuyaweka sawa haraka, ikitokea umechelewa yaani bosi mama atakushambulia kwa matusi makubwa makubwa bila kujali wengine ni baba na mama zetu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao jina lake kapuni.
Katika madai yao mengine, wameleeza kuwa Supermarket hiyo, baadhi ya bidhaa zinazouzwa haziwekewi bei (price tag) kama ulivyo utaratibu wa kawaida na badala yake wateja hukutana na bei ya bidhaa kwenye kaunta ya malipo.
“Kuna bidhaa humu ndani nyingi huwa haziwekewi bei kama ulivyo utaratibu wa kawaida na Supermarket nyingi zinafuata utaratibu huo. Hizo bidhaa hatujui huwa anazitoa wapi tunachojua zinatoka nje ya nchi na wala haijulikana kama zinalipiwa kodi kwa sababu mteja anakutana na bei kaunta na anayotajiwa inatokana kichwani mwa bosi mama.
“Bidhaa zilizoisha muda wa matumizi humu haziondolewi, zinashushwa bei wateja wanauziwa. Hizo ni pamoja na vyakula na bidhaa nyingine za ndani. Sasa wakija watu wa Serikali ni kukimbizana kuweka mambo sawa na ndiyo hapo tunaponyanyasika hasa,” amesema.
Aidha wamedai zaidi kuwa mmiliki wa Supermarket hiyo amekuwa akijenga vyumba vya biashara katika eneo analomiki na kupangisha wafanyabiashara wengine kinyume cha taratibu na inapotokea watu wa Manispaa wanafika kufanya ukaguzi, wakiondoka huanza kuwafokea wafanyakazi wake kwa kutoa siri zake.
“Huyu jamaa ni Mchina kabisa na mkewe ni Mchina lakini hapa ni kwake. Hili ni eneo lake na hivyo vyumba vya biashara vyote unavyoviona yeye ndiyo kavipangisha na analipwa kodi. Kuna baadhi ya watu wa Serikali wanajua hiyo issue hivyo huwa wanakuja kumtingisha anaongea nao.
“Wakiondoka anatugeuzia kibao wafanyakazi anatutukana ile mbaya eti sisi tunatoa siri zake wakati siyo kweli, sisi tumekuja kwake kutafuta mkate wa watoto wetu hayo maghumashi yake hayatuhusu maana hata ukisema umripoti ni kazi bure maana anajuana na watu wengi wakubwa.
“Sasa uvumilivu huwa una mwisho, majuzi katutukana sana mpaka anatutukania wazazi wetu, tumeona bora hili sasa tulisema ili mamlaka za juu waje waangalie na kuchunguza hapa na watusikilize na sisi wafanyakazi kilio chetu,” alisema.
PANORAMA Blog imemtafuta mmiliki wa Supermarket hiyo, Biao Sun kwa simu yake ya mkononi ili kuzungumzia madai hayo bila mafanikio na hata alipotumiwa maswali kwa maandishi katika simu yake, aliyasoma lakini hakujibu.