Monday, June 23, 2025
spot_img

WAFANYAKAZI CHINA TOWN SUPERMARKET WALALAMIKA KUNYANYASWA

Mahali ilipo Supermarket ya China Town


RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

WAMILIKI wa duka kubwa la kuuza mahitaji ya nyumbani (Supermarket) linalojulikana kwa jina la China Town lililopo eneo la Migombani, Kata ya Mikocheni mkoani Dar es Salaam wanadaiwa  kuwanyanyasa wafanyakazi wao.

Madai hayo yametolewa na baadhi ya wafanyakazi wa Supermarket hiyo mapema wiki iliyopita katika mahojiano waliyoyafanya na PANORAMA Blog jijini Dar es Salaam.

Wamesema mke wa mwenye Supermarket hiyo ambaye ni raia wa China hapendi kuitwa jina lake badala yake anataka aitwe boss na anapotokea mfanyakazi kumuita jina lake humshambulia kwa maneno makali yasiyotamkika.

“Changamoto ni kubwa sana kazini kwetu na tuseme siyo changamoto ni matatizo. Tatizo kubwa lipo kwa bosi mama, yeye kwanza hapendi kuitwa jina lake anataka aitwe bosi. Ukikosea kumuita jina lake unayaoga matusi.

“Mbali na hilo ikitokea wamekuja watu wa Serikali kufanya ukaguzi maana wanakuja kila mara pale kwa sababu kuna maghumashi mengi sana. Sasa wakija huwa kuna mambo tunatakiwa kuyaweka sawa haraka, ikitokea umechelewa yaani bosi mama atakushambulia kwa matusi makubwa makubwa bila kujali wengine ni baba na mama zetu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao jina lake kapuni.



Katika madai yao mengine, wameleeza kuwa katika Supermarket hiyo, baadhi ya bidhaa zinazouzwa haziwekewi bei (price tag) kama ulivyo utaratibu wa kawaida na badala yake wateja hukutana na bei ya bidhaa kwenye kaunta ya malipo.

“Kuna bidhaa humu ndani nyingi huwa haziwekewi bei kama ulivyo utaratibu wa kawaida na Supermarket nyingi zinafuata utaratibu huo. Hizo bidhaa hatujui huwa anazitoa wapi tunachojua zinatoka nje ya nchi na wala haijulikana kama zinalipiwa kodi kwa sababu mteja anakutana na bei kaunta na anayotajiwa inatokana kichwani mwa bosi mama.

“Bidhaa zilizoisha muda wa matumizi humu huwa haziondolewi, zinashushwa bei wateja wanauziwa. Hizo ni pamoja na vyakula na bidhaa nyingine za ndani. Sasa wakija watu wa Serikali ni kukimbizana kuweka mambo sawa na ndiyo hapo tunaponyanyasika hasa,” amesema.

Aidha wamedai zaidi kuwa mmiliki wa Supermarket hiyo amekuwa akijenga vyumba vya biashara katika eneo analomiki na kupangisha wafanyabiashara wengine kinyume cha taratibu na inapotokea watu wa Manispaa wanafika kufanya ukaguzi, wakiondoka huanza kuwafokea wafanyakazi wake kwa kutoa siri zake.

“Huyu jamaa ni Mchina kabisa na mkewe ni Mchina lakini hapa ni kwake. Hili ni eneo lake na hivyo vyumba vya biashara vyote unavyoviona yeye ndiyo kavipangisha na analipwa kodi. Kuna baadhi ya watu wa Serikali wanajua hiyo issue hivyo huwa wanakuja kumtingisha anaongea nao. 

“Wakiondoka anatugeuzia kibao wafanyakazi anatutukana ile mbaya eti sisi tunatoa siri zake wakati siyo kweli sisi tumekuja kwake kutafuta mkate wa watoto wetu hayo maghumashi yake hayatuhusu maana hata ukisema umripoti ni kazi bure maana anajuana na watu wengi wakubwa.

“Sasa uvumilivu huwa una mwisho, majuzi katutukana sana mpaka anatutukania wazazi wetu, tumeona bora hili sasa tulisema ili mamlaka za juu waje waangalie na kuchunguza hapa na watusikilize na sisi wafanyakazi kilio chetu,” alisema.

PANORAMA Blog imemtafuta mmiliki wa Supermarket hiyo, Biao Sun kwa simu yake ya mkononi ili kuzungumzia madai hayo bila mafanikio na hata alipotumiwa maswali kwa maandishi katika simu yake, aliyasoma lakini hakujibu.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya