![]() |
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WAKATI sakata la kuchafuka kwa maji ya Mto Mara likiwa halijapoa na sintofahamu iliyoibuka baada ya kamati ya wataalamu iliyoundwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo kuchunguza chanzo cha kuchafuka kwa maji hayo kupokelewa na wengi kwa hisia tofauti, Waziri huyo amekosa kauli dhidi ya chupa za plastiki za kinywaji cha Mo Energy zinazodaiwa kuwa ni hatari kwa uhai wa mazingira.
Chupa za plastiki za kinywaji cha Mo Energy zinadaiwa kuwa hatari kwa uhai wa mazingira huku baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaojihusisha na uokotaji wa taka za plastiki zikiwemo chupa hizo ambazo huziuza kwa wenye viwanda vya kutengeneza chupa za plastiki wakiwa hawaziokoti kutokana na kinachodaiwa kuwa ni uhatari wake kwa mazingira.
Mbali na hao, Mkuu wa Wilaya wa Morogoro (DC), Albert Msando naye amekwisha watahadharisha wakazi wa wilaya yake kuhusu uhatari wa chupa hizo kwa usalama za mazingira.
Tanzania PANORAMA Blog iliwasiliana na Waziri Jafo Machi 15, 2022 kwa simu yake ya kiganjani bila mafanikio na baadaye ilimtumia ujumbe wa whatsapp ikimuuliza iwapo wizara yake imekwishapata malalamiko au taarifa kuhusu uhatari wa chupa hizo.
Aidha, PANORAMA ilimuuliza Waziri Jafo utaratibu unaotumika kupasisha matumizi ya chupa za plasiti zinazotumika kuhifadhi vinywaji baridi vinavyotengenezwa hapa nchini na hatua zinazochukuliwa kwa watu au kampuni zinazotengeneza au kutumia chupa ambazo ni hatarishi kwa mazingira. Ujumbe huo aliupokea na kuusoma lakini hakujibu.
Machi 17, 2022, PANORAMA ilimtumia ‘link’ ya habari iliyoandikwa kuhusu madai ya chupa hizo kuwa hatari kwa mazingira. Waziri Jafo aliisoma habari hiyo na kuendelea kukaa kimya.
Machi 19, 2022 PANORAMA ilimtumia ujumbe Waziri Jaffo ikimkumbusha kujibu maswali aliyoulizwa na ilirejea kuyatuma kwake tena lakini katika hali ya kushangaza Waziri Jafo aliendelea kunyamaza kimya kabisa licha ya kupokea ujumbe na maswali na kuonyesha kuwa amesoma.
Chupa za kinywaji cha Mo Energy zinatengenezwa na moja ya makampuni ya mfanyabiashara Mtanzania mwenye asili ya kiasia, Ghulam Dewji ambaye alipoulizwa kuhusu hilo alijibu kwa ufupi kuwa yeye hutengeneza chupa hizo kwa kutumia chupataka za plastiki anazouziwa na waokota takataka za plastiki, kisha akakata simu.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira – NEMC Mhandisi Samuel Gwamaka alipoulizwa kuhusu hilo alisema yupo kwenye kikao mkoani Mara hivyo atafutwe wakati mwingine.
![]() |
Ghulam Dewji |
Rekodi zilizopo kuhusu Ghulam Dewji zinaonyesha kuwa hii si mara ya kwanza kwa kampuni anazomiliki kudaiwa kutengeneza au kuingiza bidhaa zisizofaa nchini.
Kwa mujibu rekodi hizo, Ghulam na baadhi ya kampuni zake, kwa nyakati tofauti katika miaka 1990 wamepata kuingia kwenye kashfa ya kuingiza nchini mchele usiofaa kwa matumizi ya binadamu.
Tukio hilo lilifikishwa katika vyombo vya sheria lakini haijapata kufahamika kesi hiyo ilivyomalizika baada ya wahusika wote muhimu kwenye kesi hiyo kufariki dunia ikiwa ni pamoja na waliokuwa Wakemia Wakuu wawili wa Serikali, Mahakamu, waendesha mashtaka na mashahidi wote.
Mbali ya hilo, rekodi zinaonyesha kuwa tukio jingine ni lile lililomuhusisha Ghulam Dewji na moja ya kampuni zake kuingiza nchini ngano isiyofaa kwa matumizi ya binadamu.
Tanzania PANORAMA Blog itaendelea kuripoti habari hii.