Monday, August 25, 2025
spot_img

CHUPA ZA MO ENERGY HATARI

Chupa za Mo Energy zilizotupwa jalalani zikiwa zimeachwa na waokota taka wanaodai kuwa chupa hizo ni hatari kwa mazingira

  

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

Chupa za Plastiki za kinywaji cha Mo Energy ni hatari kwa uhai wa mazingira kwa sababu zikitupwa ardhini haziozi.

Hayo yameelezwa na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaojihusisha na uokotaji wa taka za plastiki ambazo huziuza kwa wenye viwanda vya kutengeneza chupa za aina hiyo.

Mbali na hao, Mkuu wa Wilaya wa Morogoro (DC), Albert Msando naye amekwisha watahadharisha wakazi wa wilaya yake kuhusu uhatari wa chupa hizo kwa usalama wa mazingira.

DC Msando alitoa tahadhari hiyo kwa kuandika kwenye mitandao ya kijamii, ameandika; “Hizi plastiki (plastics) ni hatari sana kwa mazingira yetu. Haziozi. Hizi za Mo Energy waokotaji plastiki hawaziokoti. Nitoe rai kwa wananchi wote, tulinde mazingira kwa wivu mkubwa. Mabadiliko ya tabia nchi siyo tishio, ni uhalisia.

“Hapo ulipo chukua hatua, hili ni taifa letu sote. Usibaki kulaumu tu.” Ameandika Msando ambaye ni kiongozi wa kwanza wa Serikali kutoka hadharani kuueleza umma tishio la chupa hizo kwa uhai wa mazingira.

Baadhi ya waokota plastiki waliozungumza na Tanzania PANORAMA Blog nao walieleza kuwa wenye viwanda vya kutengeneza bidhaa za plastiki ambao ndio wanunuzi wa bidhaa zao hawanunua chupa za Mo Energy kwa sababu zimetengenezwa kwa kemikali zisizofaa.

Walieleza kuwa chupa hizo huonyesha utofauti na chupa nyingine za plastiki hata zikiangaliwa kwa macho.

Mmoja wa waokota chupa hizo katika eneo la Lumumba, Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Alfred Manyama alisema zinaonekana kwa wingi zikiwa zimetupwa maeneo mbalimbali kwa sababu tofauti na nyingine hizo huwa hawaziokoti.

“Kwa hizi takataka za chupa za plastiki zilizokwishaondolewa vinywaji kwa watu kuvinywa kama ni juisi au maji au hivyo vya kuongeza nguvu, chupa za Mo Energy zinaonekana kwa wingi mabarabarani zikiwa zimetupwa kwa sababu hata tukiziokota wenye viwanda tunakopeleka kuuza hawazinunui.

“Na wamekwishatuambia kabisa kuwa chupa hizo hawazitaki kwa sababu zimetengenezwa kwa kemikali hatari hivyo wakikuta mzigo wako una chupa za Mo Energy hata kama ni chupa moja tu wanaweza kukataa kukulipa au kama hawajamwaga mzigo wanakurudishia wanakwambia uondoke nao,” alisema Manyama.

Muokota takataka mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jumbe Ramadhani wa Kimara Suka, naye alieleza kuwa haokoti chupa hizo kwa sababu hazitakiwa viwandani.

Alisema viwanda vingi vinavyotengeneza chupa za plastiki vinamilikiwa na wachina ambao wanakataa kuzipokea kwa madai kuwa hazifai.

“Wachina hawazitaki hizo chupa wanapoziyeyusha kutengeneza nyingine upya wanasema zina matatizo ndiyo maana zimezagaa mitaani na mabarabarani.

“Sisi waokota plastiki tunasaidia sana kufanya usafi wa kuziondoa hizi chupa sasa tusipoziokota na wanywaji wanaokunywa na kuzitupa hovyo ni wengi lazima zitazagaa kila mahali,” alisema Ramadhani. 

Ghulam Dewji


 

Mkurugenzi wa Mo Energy, Ghulam Dewji alipoulizwa kuhusu hilo alijibu kwa ufupi kuwa chupa hizo zinatengenezwa na kampuni yake kwa kutumia chupa za plastiki zilizokwishatumika na kutupwa ambazo huokotwa na kutengenezwa upya, kisha akakata simu.

Baadhi ya wenye viwanda vya kutengeneza chupa hizo waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao kwa maelezo kuwa hawataki kuingia kwenye uadui wa kibiashara na mmiliki wa kampuni hizo walisema chupa hizo hazifai na inashangaza kuona mtengenezaji ameachwa akiendelea kuzizalisha licha ya kuwepo wito wa kupambana na uharibifu wa mazingira.

Afisa mmoja wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira – NEMC (jina lake limehifadhiwa kwa sababu siyo msemaji) alipoulizwa, alisema taarifa kuwa chupa hizo ni hatari kwa mazingira hazijawafikia lakini aliahidi kuliwasilisha suala hilo katika dawati husika kwa ajili ya kufanyika uchunguzi.

“Mimi siyo msemaji hivyo nisingependa kutajwa ila suala la hizi chupa lilikuwa halijatufikia. Nitalipeleka sehemu husika uchunguzi ufanyike haraka. Ila kama kweli hata waokota chupa hawaziokoti basi hapo kuna tatizo. Wewe endelea kumtafuta msemaji lakini mimi nalichukua,” alisema.

Rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa hii si mara ya kwanza kwa kampuni zinazomilikiwa na mfanyabashara Ghulam Dewji kudaiwa kutengeneza au kuingiza bidhaa zisizofaa nchini.

Kwa mujibu rekodi hizo, Ghulam na baadhi ya kampuni zake, kwa nyakati tofauti wamepata kuingia kwenye msukosuko miaka ya 1990 baada ya kudaiwa kuingiza nchini mchele usiofaa kwa matumizi ya binadamu.

Tukio hilo lilifikishwa katika vyombo vya sheria lakini haijapata kufahamika kesi hiyo ilivyomalizika baada ya wahusika wote muhimu kwenye kesi hiyo kufariki dunia ikiwa ni pamoja na waliokuwa Wakemia Wakuu wawili wa Serikali, Mahakimu, waendesha mashtaka na mashahidi wote.

Mbali ya hilo, rekodi zinaonyesha kuwa tukio jingine ni lile lililomuhusisha Ghulam Dewji na moja ya kampuni zake kuingiza nchini ngano isiyofaa kwa matumizi ya binadamu.

Tanzania PANORAMA Blog itaendelea kuripoti habari hii

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya