Tuesday, December 24, 2024
spot_img

DIWANI CCM KAWE AIBUA HOFU

Diwani wa Kata ya Kawe (CCM) Mutta Robert Rwakatare

  

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

KUNA wasiwasi wa mahali alipo na hali ya afya ya Diwani wa Kata ya Kawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mutta Robert Rwakatare.

Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa imekuwa ikielezwa na watu wake wa karibu kuwa haijulikani alipo na Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta kipindi chote hicho bila mafanikio.

Hata hivyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge alipoulizwa kuhusu hilo alisema Diwani Mutta yupo na mara ya mwisho aliongea naye Machi 6, 2021 majira saa 7.30 mchana.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge

 

Meya Mnyonge aliombwa na Tanzania PANORAMA Blog kuiwezesha kumfikia au kuwasiliana naye kwa njia ya simu na aliahidi kufanya hivyo lakini hadi sasa hajatekeleza hilo licha ya kukumbushwa na kuelezwa sababu za msingi za PANORAMA Blog kumsaka.

Diwani Mutta na ndugu zake watatu wanatuhumiwa na kaka yao, Tibe Kenneth Rwakatare kughushi nyaraka za mauzo ya kiwanja namba 259 kilichopo eneo la Udindifu Bagamoyo pamoja na kukwepa kulipa kodi ya Serikali.

Tibe alipoulizwa hivi karibuni kuhusu alipo mdogo wake Mutta alisema hana taarifa zake na kwamba yeye Dodoma kwa shughuli zake.

Tanzania PANORAMA Blog imefika mara kadhaa katika ofisi za Diwani Mutta zilizopo eneo Afrika Sana, Mwenge na mara zote imekuwa ikielezwa kuwa hayupo na haijulikani alipo.

Baadhi ya watumishi katika Ofisi ya Kata ya Kawe ambako PANORAMA Blog ilifika kumsaka Diwani Mutta walieleza kuwa hajaonekana kwa muda mrefu.

Mmoja wa viongozi wa kata hiyo aliyezungumza na PANORAMA Blog kwa ombi la kihifadhiwa jina lake alisema katika kipindi cha mwezi mmoja hajapata kuonana naye isipokuwa siku moja alipewa taarifa kuwa diwani huyo alifika ofisini hapo kumuulizia.

“Nina zaidi ya mwezi mmoja sijamuona mimi, ila siku moja nilikuwa kwenye kazi za nje niliporudi nikaambiwa kuwa diwani alipita hapa kukuulizia, kwa hiyo nilipishana naye.

“Ofisi yake hiyo hapo imefungwa tu siku zote ila hapa huwa anapaswa kuwepo siku za Jumanne na Alhamis. Bosi wake ni Meya na Mkurugenzi na hata posho zake analipwa huko, mkimuuliza Meya wa Kinondoni atakuwa anajua yupo wapi na kama kuna jingine kumhusu yeye anajua,” alisema afisa huyo.

PANORAMA Blog imejaribu mara kadhaa kumtafuta kwa simu yake ya kiganjani bila mafanikio na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake hajapata kujibu.

Taarifa zilizopo zinadai kuwa Diwani Mutta amekuwa akipotea mara kwa mara ikiwa haijulikani mahali anakokwenda na anaporejea huwa katika hali isiyokuwa ya kawaida.

“Sasa wanadai kapatikana, amerejea lakini wanasema hayupo kwenye hali ya kawaida kabisa, lakini sijui kama kweli kapatikana, hili jambo hili litakuja kuibuka na mengi yaliyofichika, sisi msitutaje nyie endeleeni kumtafuta,” alisema mmoja wa watoa taarifa.

PANORAMA Blog inaendelea na uchunguzi wa sintofahamu ya kutopatikana kwa Diwani Mutta.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya