Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema barua aliyoandikiwa na mtoto wa aliyekuwa Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God- Mlima wa Moto na Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Marehemu Mchungaji Getrude Rwakatare hajaiona.
Waziri Mabula ameyasema hayo alipoulizwa hatua zilizochukuliwa na ofisi yake kushughulikia taarifa za kuwepo matendo ya jinai yaliyofanywa na watoto wa Marehemu Mchungaji Rwakatare katika uuzaji wa plot namba 259 iliyopo Udindifu, Bagamoyo kama yalivyoainishwa kwenye barua hiyo iliyoandikwa na Tibe Kenneth Rwakatare.
Tayari baadhi ya wanasheria wamekwishaeleza kuwa tuhuma zilizotolewa na Tibe Kenneth Rwakatare ambaye ni mtoto wa kiume mkubwa wa Marehemu Mchungaji Rwakatare dhidi ya wadogo zake, iwapo zitathibitika pasipo shaka mahakamani, wanaweza kukabiliwa na kifungo cha maisha gerezani.
Tibe Kenneth Rwakatare |
Tibe Kenneth Rwakatare katika barua yake ya Disemba 31, 2021 kwenda kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anaeleza kuwa yeye ni mmoja wa wasimamizi wa mirathi ya Marehemu Getrude Rwakatare na anaanishi malalamiko sita dhidi ya wadogo zake pamoja na ombi moja.
Anaandika kuwa plot nambari 259 ilikuwa ikimilikiwa na Marehemu Idd Hashimu Mbita ambaye aliiuzia St. Mary’s International Ltd.
Kwamba uhamishaji (transfer) kutoka kwa Idd Hashimu Mbita kwenda St Mary’s International Ltd haukufanyika hadi Mkurugenzi Mkuu, Marehemu Mchungaji Getrude Rwakatare alipofariki.
Anaendelea kuandika kuwa baada ya mama yao kufariki dunia, wasimamizi wenzake wa mirathi anaowataja kuwa ni Kellen Rose Rwakatare Kuntu, Humphrey Kaulila Kenneth Rwakatare na Mutta Robert Rwakatare kwa pamoja waliuza plot namba 259 kwa mdogo wake na mmiliki wa jengo la Kibo Complex bila kumshirikisha.
Kwamba hawakuwashirikisha pia wakurugenzi wengine wa St Mary’s International Academy Ltd anaowataja kuwa ni Adam Kondo na Alex Bernald Mengi.
Tibe anamwandikia waziri akieleza kuwa Rose, Mutta na Humphrey walifoji karatasi za mauzo zinazoonyesha muuzaji ni Idd Hashim Mbita ambaye ameishafariki huku St Mary’s International Academy Ltd ikiachwa pembeni.
Anaandika zaidi kuwa kutoonekana kwa St Mary’s International Academy Ltd katika mauzo hayo kulilenga kukwepa kulipa kodi ya Serikali ndiyo maana uuzaji ulifanyika juu kwa juu.
Tibe anamfahamisha Waziri kuwa taarifa zote anazo Afisa Ardhi wa Kanda ya Mashariki Dar es Salaam lakini anaamini hajazifanyia kazi kwa sababu ya rushwa.
Anahitimisha barua yake hiyo kwa kumuomba Waziri aingilie kati atengue mauzo hayo ili mali hiyo ibaki kuwa ya St. Mary’s International Academy Ltd.