Gabriel Mwita Thobias |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WAKATI Serikali ikiongeza nguvu kupambana na rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Mamlaka wa Bandari (TPA) Gabriel Mwita Thobias anadaiwa amekuwa akitumia madaraka yake kutekeleza vitendo hivyo.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimedai kuwa Thobias anatuhumiwa na baadhi ya wanawake waliopata kufanya kazi naye kwa matumizi mabaya ya madaraka, kuwaomba rushwa ya ngono na kuwanyanyasa kingono.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, hivi karibuni kuhusu madai hayo, mmoja wa wanawake hao alisema Thobias, akiwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Tanzania Leaf Tobacco Company Limited (TLTC), mkoani Morogoro alikuwa akitumia madaraka yake kuomba rushwa ya ngono na kuwanyanyasa kingono wafanyakazi wanawake.
“Nimefanya kazi naye Thobias, nimefanya kazi naye TLTC akiwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, ni Mungu tu aliyesaidia lakini nilipitia wakati mgumu sana kwa sababu nilikuwa kwenye shinikizo la kumpa mwili wangu au nisiharibikiwe kazini. Nilikataa, sikumpa. Nikayakubali mateso yote aliyonipatia mpaka alipofukuzwa kazi kwa makosa ya kuomba rushwa ya ngono na kunyanyasa wanawake kingono. Siyo peke yangu niyekutana na tanuru la moto la Thobias, tupo wengi.
“Baadaye nasikia alipata kazi serikalini. Sijui ya wanawake wa huko lakini sasa tunapoona hizi bidii za kupambana na vitendo vya rushwa ya ngono tunajiuliza kama wahusika wakuu wapo, wanahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hizo bidii zitafanikiwa? Angalia hizo nyaraka, angali ushahidi wa wenzangu pia wa matendo aliyowafanyia. Safari ya wanawake bado ni ngumu sana.”
Hati za maandishi ambazo Tanzania PANORAMA Blog imeziona zikithibitisha Thobias kutekeleza vitendo hivyo ni za Pola Takis, Josephine Mworia, Glady’s Almas na Aidat Mhidini, ambazo ziliwasilishwa kamati ya nidhamu ya TLTC, nayo ikamkuta na makosa yaliyomfukuzisha kazi.
Hati ya kwanza ya Pola Takis kwenda kamati ya nidhamu ya TLTC, pamoja na mambo mengine inasomeka kuwa Thobias alimfanyia vitendo vya unyanyasaji wa kingono na uonevu mahali pa kazi baada ya kukataa matakwa yake ya kukutana naye kimwili.
Katika hati hiyo, Takis anaandika kuwa Thobias alipata kumwita mara kadhaa nyumbani kwake ili wakanywe mvinyo pamoja, jambo ambalo hakuliafiki ndipo alipoanza kunyanyaswa na Thobias.
Mbali na Takis, hati nyingine ya maandishi inayomtuhumu Thobias ni ya Josephine Mworia ambayo inaeleza kuwa alishushwa cheo na Thobias baada ya kukataa kumpa rushwa ya ngono.
Hati ya Glady’s Almas, kwa uchache inaeleza kuwa alikuwa akihisi wasiwasi na hofu kazini kutokana na matendo ya Thobias baada ya kukataa kutekeleza matakwa yake.
Almas anaeleza zaidi kuwa akiwa na jukumu la kutoa mafunzo kazini kwa wafanyakazi wapya, Thobias alikutana na mumewe na kumweleza mambo yaliyomfanya akose utulivu wa akili kazini.
Ipo pia hati ya Aidat Mhidini ambayo inaeleza kuwa Thobias alimfanyia usaili alipoomba kazi TLTC na baada ya usaili kukamilika, alimtaka wakutane Hoteli ya Morogoro kwa ajili ya kuyapitia maombi yake ya kazi.
Anaeleza kuwa alikutana naye akiwa na wenzake kadhaa na kumtaka wakutane wakati mwingine kwa ajili ya mlo wa mchana.
Kwamba wakiwa wanapata mlo wa mchana, Thobias alimtamkia Aidat kuwa ampatie mwili wake kwa usiku huo ili awe na uhakika wa kupata kazi, jambo ambalo alilikataa.
Anaendelea kueleza kuwa baada ya siku kadhaa kupita, Thobias alimtafuta tena na kumwambia kama hataafiki takwa lake la kulala naye hatapa nafasi ya kazi aliyoiomba na kwamba baada ya kuona vitendo vya unyanyasaji wa kingoni vinazidi kushika kazi aliamua kuachana na maombi yake hayo.
Alipoulizwa Thobias kuhusiana na tuhuma hizo alisema ni mambo ya zamani na kwamba kamati iliyomtia hatiani kabla hajafukuzwa kazi ilikuwa kamati batili.
Wakili Kiongozi wa kampuni ya Haki Kwanza Advocates, aliyebobea katika mashauri ya ajira na mahusiano kazini, Alloyce Komba |
Wakili msomi mwandamizi aliyebobea katika mashauri ya ajira na mahusiano kazini na ambaye pia ni Wakili Kiongozi wa Kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza Advocates, Alloyce Komba ametoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu mtu anayefukuzwa kazi kwa makosa ya kuomba rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingoni kupata ajira nyingine, amesema;
“Hakuna sheria inayomzuia mtu aliyetiwa hatiani kwa makosa ya kuomba rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono kwa wanawake kisha akafukuzwa kazi, kupata kazi sehemu nyingine.
“Tena hasa kama ni kutoka Sekta Binafsi kwenda Sekta ya Umma, labda kuwe na uchunguzi makini (Vetting). Ni kama tu mwanafunzi aliyefukuzwa shule ‘A’ kwa utovu wa nidhamu anaweza kuomba kusoma katika shule ‘B’ au ‘C’ au ‘D’ ya sehemu nyingine.”
Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kumtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Salum Hamduni ili kupata kauli yake kuhusu suala hili.