Afisa Habari wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Lwaga Mwambande |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema mabenki nchini yanayo ruksa ya kupanga kiasi cha fedha taslimu wanazotaka kuchukua wateja wake na hakuna ukomo ilioweka kwa benki hizo wa kuwapa wateja wake kiasi chochote cha fedha taslimu wanazozitaka kutoka kwenye amana zao.
BoT imeeleza kuwapo kwa ruksa hiyo katika majibu yake kwa Tanzania PANORAMA Blog iliyoyatoa hivi karibuni ya iwapo kuna utaratibu wowote iliyoweka kwa mabenki wa kutoa fedha taslimu kwa wateja wake na utaratibu huo unaziruhusu benki kutoa hadi kiasi gani cha fedha taslimu kwa wateja.
Tanzania PANORAMA Blog pia iliiuliza BoT ambayo ni msimamizi wa mabenki nchini kama imeweka utaratibu wa kuwepo ukomo kwa wateja kuchukua fedha taslimu, wateja wanaochukua fedha taslimu kuanzia Shilingi mil 100 wanapaswa kufuata utaratibu gani, taratibu za kibenki za uchukuaji fedha taslimu Shilingi mil 100 kwa wateja binafsi na kampuni na taratibu za kisheria zinazoweza kuchukuliwa kwa benki inayobainika kukiuka taratibu za utoaji fedha taslimu kwa wateja.
Katika majibu yake ya maandishi, Afisa Habari wa BoT, Lwaga Mwambade ameandika; “Katika kutimiza jukumu lake la kusimamia benki na taasisi za fedha, Benki Kuu ya Tanzania huzitaka Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Benki na taasisi za fedha kuweka sera, miongozo na taratibu za namna ya kuendesha shughuli zake za kila siku.
“Kutoa fedha taslimu kwa wateja ni moja ya kazi za kawaida za kiuendeshaji za kila siku za benki ambazo Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti zinapaswa kuziwekea utaratibu na siyo Benki ya Tanzania kama mdhibiti.”
Akijibu swali lililouliza utaratibu unaoruhusu benki husika kutoa hadi kiasi gani cha fedha taslimu kwa mteja, Mwambande ameandika; “Hakuna sheria, kanuni wala mwongozo uliotolewa na Benki Kuu ya Tanzania unaoweka ukomo wa kiasi cha fedha pindi mteja anapohitaji kuchukua fedha taslimu kutoka kwenye akaunti yake ya amana.
“Kama ilivyoelezwa kwenye jibu la swali namba moja jukumu la kuweka utaratibu wa kutoa fedha kwa wateja ikiwa ni pamoja na ukomo wa kiasi kinachoweza kuchukuliwa ni la Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti za Benki husika na siyo Benki Kuu ya Tanzania kama mdhibiti.”
Kuhusu ukomo uliowekwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki kwa mteja kuchukua fedha taslimu kutoka kwenye benki aliyohifadhi fedha, Mwambande ameandika; “Hakuna ukomo uliowekwa na Benki Kuu ya Tanzania kama mdhibiti.
“Hili ni suala la uendeshaji na kila benki hujiwekea ukomo kwa mujibu wa taratibu zake kwa kuzingatia matakwa ya sheria, kanuni na miongozo ya udhibiti wa utakatishaji fedha na uzuwiaji ufadhili wa ugaidi.”
Kwa upande wa wateja wanaochokua fedha taslimu kuanzia Shilingi mil 100 kama kuna utaratibu wanaopaswa kuuzingatia, Mwambande ameandika; “Kama ilivyoelezwa, jukumu la kuweka utaratibu wa kutoa fedha taslimu kwa wateja ikiwa ni pamoja na ukomo wa kiasi kinachoweza kuchukuliwa ni la Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki husika na siyo Benki Kuu ya Tanzania kama mdhibiti.
Kuhusu taratibu za kibenki za uchukuaji fedha taslimu zaidi ya Shilingi mil 100 kwa mteja binafsi au kampuni, Mwambande ameandika; “Kama ilivyoelezwa jukumu la kuweka utaratibu wa kutoa fedha taslimu kwa wateja ikiwa ni pamoja na ukomo wa kiasi kinachoweza kuchukuliwa ni la Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki husika na siyo Benki Kuu ya Tanzania kama mdhibiti.”
Akijibu swali kuhusu hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa kwa benki inayokiuka taratibu za utoaji fedha taslimu kwa wateja, Mwambande ameandika; “Endapo itabainika benki imekiuka matakwa ya sheria, kanuni na miongozo ya udhibiti wa utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi katika kuchukua na kuweka fedha taslimu, benki husika itachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Hatua hizo ni pamoja na adhabu ya faini ya fedha au kuondolewa ofisini kwa afisa anayehusika.”
BoT imetoa ufafanuzi huu wakati Tanzania PANORAMA Blog ikiwa na taarifa kuwa Benki ya I&M yenye makao makuu yake barabara ya Maktaba katika jengo la Maktaba iliidhinisha zaidi ya Shilingi bilioni mbili zikiwa ni fedha taslimu kuchukuliwa na mteja wake mmoja katika kipindi cha mwaka mmoja.
Taarifa za kuwepo kwa miamala hiyo, zimethibitishwa na mmoja wa waliokuwa wafanyakazi wa mteja huyo aliyeleeza kuwa bosi wake alikuwa wakala wa fedha wa watu ambao hawafahamu.
Katika mahojiano yake ya Tanzania PANORAMA kuhusu kampuni hiyo kuchukua zaidi ya Shilingi bilioni mbili zikiwa fedha taslimu alisema fedha hizo zilikuwa zikiingizwa kwenye akaunti ya bosi wake kwa makubaliano maalumu baina ya waingizaji na mtoaji.
Alisema, waingizaji fedha walikuwa wakiziingiza kwenye akaunti moja ile ile ya bosi wake iliyokuwa kwenye Benki ya I&M na jukumu alilokuwa nalo bosi wake huyo ilikuwa kuzitoa zikiwa fedha taslimu na kuzipeleka kwa wahusika huku yeye akilipwa bakshishi ya asilimia 20 kwa kila kiwango cha fedha taslimu kilichopitia kwenye akaunti yake hiyo.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, Meneja Biashara na Habari wa Benki ya I&M, Anitha Pallaghyo ambaye aliulizwa kuhusu miamala hiyo, ameshindwa kujibu chochote.