Monday, December 23, 2024
spot_img

CHAWA ANAPODANDA KILEMBA CHA RAIS SAMIA (2)

MCHOKONOZI

0711 46 49 84

MILA, desturi na tamaduni za kiafrika zinatufundisha na kutuelekeza waafrika wadogo kiumri kuheshimu wazee wetu bila kujali kuwa ni watu wenye mamlaka makubwa au lah katika jamii.
Na hata inapotokea ulazima wa mdogo kumkosoa mkubwa, awe kaka, baba, babu na ama dada, mama au bibi, ukosoaji wa kijana wa kiafrika sharti uwe wa staha.

Inapotokea kijana wa kiafrika kumdhihaki, kumsimanga, kumkebehi, kumchafua na au kutenda mambo mengine kama hayo kwa mtu mwenye rika sawa na la baba yake au kaka yake mkubwa, huyo huwekwa kwenye kundi la wakosefu wa adabu. Mtu ambaye hakupata malezi sahihi kutoka kwenye chimbuko lake.

Kwa waafrika, mtu anayesimama hadharani kubagaza uongozi uliochaguliwa na watu. Mtu anayetumia ulimi au kalamu yake kudhalilisha, kukebehi, kutukana au kwa namna yoyote ile kuchafua au kuchonganisha mamlaka halali za nchi na wananchi kwa sababu zozote zile, huyo mbali na kubeba taswira ya chawa, anaweza pia kuwekwa kwenye kundi la vikaragosi.

Anaweza kuwa kikaragosi wa akili yake mwenyewe au wa anaowatumikia kwa sababu anakuwa hana tofauti na kinyango kinachochezeshwa kwa kutumia vijiti na kamba, na mchezeshaji anakuwa na uwezo wa kukichezesha kikarogi mchezo wowote ule anaoutaka.

Kikaragosi kinaweza kuchezeshwa uchi mbele ya kadamnasi ya watu na kikademka kwa namna mchezashaji wake atakavyo. Ni kikaragosi hakina uwezo wa kuchagua mtindo wa udemkaji. Kikaragosi kinaweza kumwaga radhi juu ya kaburi kwa sababu ni kikaragosi

Siyo utaratibu na si maadili ya kiafrika kushambulia wafu. Mtu anayeshambulia marehemu ambaye kabla hajayaonja mauti alikuwa akimsifia kwa kiwango cha kumtakatifuza lakini baada ya mtu huyo kufariki dunia akaanza kumtweza, mtu huyo ni hatari katika jamii.

Kama siyo kikaragosi ni mtu mpumbavu kwa maana ile ile ya mpumbavu tuliyoiona kwenye sehemu ya kwanza ya waraka huu wa Mchokonozi.

Watu wenye hulka za kipumbavu wanapotekeleza upumbavu wao hujiwekea uzio wa kutoguswa na yeyote. Huwa wanaijengea jamii dhana kwamba wao ndiyo wakweli, wanaopingana na mawazo au mitizamo yao ni masalia ya wanaowatweza.

Mwandishi Deodatus Balile katika makala zake kadhaa za kukashfu, kukebehi, kumsimanga na kumshambulia Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli na Serikali aliyokuwa akiiongoza ya awamu ya tano analifanya hilo bila woga.

Akiwa na dhamana ya uongozi wa baadhi ya wenzake na msomi mwenye vyeti kadhaa ambavyo binafsi sijui kama vina maana yoyote kwake, Balile anatekeleza matendo ya kikatili dhidi ya Hayati Rais Dk. Magufuli huku akijua fika kuwa Hayati Dk. Magufuli ana watoto, ana kaka na dada, ana mke, anao wanaCCM wenzake, ana jeshi kubwa la Watanzania, ana walimwengu, ana wazazi.

Wote hawa bado wana vidonda vya kuondokewa na mpendwa wao, katikati ya hudhuni zao yeye anatonesha vidonda vyao kwa ukatili wa hali ya juu.

Inawezekana anayo chuki dhidi yake ambayo sisi wengine hatuijui lakini yeye Balile kama kiongozi huko kwa wenzake, kijana kutoka moja ya vijiji vya Afrika na msomi, alipaswa kutambua kuwa Hayati Rais Dk Magufuli hakuwa malaika, alikuwa binadamu kama binadamu wengine. Anastahili heshima ya kibinadamu.

Balile anapoandika hivi; ‘Najua kuna baadhi ya wanufaika kwa kusema hivi mnafuka moshi kwa ndani. Sitanii, nafahamu bado kuna masalia. Hata huko kwenye mitandao ya kijamii kwenye hiyo inayoitwa Club House, nako masalia hayakosekani.

‘Nimesikiliza mjadala unaoendeshwa baadhi wakimmwagia matusi Rais Samia kwa kukutana na Lissu huko Ubelgiji. Wanamwita kila jina baya, ila unahitajika umakini kufahamu iwapo wanaorusha matusi si sehemu ya masalia.

‘Nafahamu hata baadhi ya watendaji kuna kambi. Kuna wale wenye mfumo dume, kuna wale waliokuwa wanufaika wa ukandamizaji wa Watanzania. Kwa sasa tumepumzika kusikia watu wakifikishwa Kisutu, maana ilifanywa mara nyingi, hadi watu wakaacha kuona anayefikishwa mahakamani ni mdhambi.’

Hapo Balile, kwanza anajijengea uzio, anaandika kwa kutishia, hataki watu watofautiane na maandiko yake ya kichochezi, kudhalilishaji, yasiyokuwa na adabu na kila aina ya ubaya. Anaharakisha kuwaita masalia wa Serikali iliyopita wale ambao hawatakubaliana na maandishi yake.

Tena anawagusa mpaka watendaji, eti, nao wana kambi za wenye mfumo dume na wapo wanufaika wa ukandamazaji wa Watanzania. Anakwambia wewe Rais Samia kuwa miongoni mwa watendaji wako wapo masalia wa Serikali anayoivika sifa ya udhalimu. Serikali ambayo wewe ulikuwa Makamu wa Rais.

Balile, anawaandikia Watanzania kuwa sasa wamepumzika kusikia watu wakifikishwa Kisutu, maana ilifanywa mara nyingi, hadi watu wakaacha kuona anayefikishwa mahakamani ni mdhambi. Anachowaambia Watanzania ni kwamba hivi sasa watu wanafikishwa mahakamani kwa nadra sana tofauti na awali walipokuwa wanafikishwa mahakamani hovyo hovyo. Wakati ule anaouita wa giza.

Polisi wetu hawajabadilika, watendaji wa mahakama wengi ni wale wale, wangali wapo ofisini. Hawa ndiyo Balile anautangazia umma kuwa walikubuhu kwa kuwapeleka watu mahakamani hovyo hovyo.

Maandishi huwa yanaishi, alichokiandika Balile kinasomwa na Watanzania na kitaendelea kusomwa ndani ya nje ya Tanzania, kitaishi. Watanzania watakisoma kwa muda mrefu, watasoma jinsi mwandishi anavyowaweka kwenye ugiza viongozi na watendaji hawa.

Lakini sehemu nyingine katika makala yake hiyo ameandika; ‘Kilichotokea nyakati zilizopita ni cha kuandikia kitabu, na naomba Mungu anijalie nipate nguvu niandike kitabu hiki, pengine miaka 500 ijayo Watanzania wasirejee makosa yaliyofanywa na kizazi chetu katika uchaguzi wa mwaka 2015.’

Balile anatuambia Watanzania na ulimwengu kuwa mwaka 2015 tulifanya makosa kumchagua mgombea urais wa CCM, Hayati Rais Dk. John Magufuli na Mgombea mwenza wake, Rais Samia Saluhu Hassan, hii ndiyo maana yake ingawa anaweza kuwa hajui.

Haya siyo maandishi ya kawaida, si maandishi kuonya, kufundisha au kuburudisha. Mwandishi mwenye akili sawasawa hawezi kuthubutu kuutangazia umma kuwa Serikali iliyopita ilikuwa Serikali kandamizi wakati iliyoyasimamia na kuyatekeleza ndiyo yanayoendelezwa sasa, kazi inaendelea.

Hawezi kuthubutu kuandika Watanzania walifanya makosa kuichagua Serikali hiyo na kwamba makosa hayo hawapaswi kuyarudia tena wakati aliyeshiriki kwa asilimia 100 kuwashawishi wapigakura waichague Serikali hiyo ndiye Rais wa Tanzania.

Rais wa sasa alikuwa sehemu ya taasisi ya urais ambayo Balile anawaambia Watanzania ilikuwa kandamizi. Makamu wa Rais wa sasa alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo, viongozi na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kiasi kikubwa ni wale wale waliokuwa kwenye Serikali hiyo ambayo Balile anaiita Serikali ya kikandamizaji. Nina mashaka kama Balile anajua athari za maandishi yake haya.

Inatia wasiwasi kama Balile anajua anachoiandikia jamii, kama anajua athari hasi za maandishi yake ya hovyo katika jamii. Ni vigumu kuamini kuwa Balile hajui kuwa anachokifanya hakilengi kumdhalilisha, kumkebehi, kumsimanga na kumchafua kwa namna zote anazofanya Hayati Rais Dk. Magufuli, bali maandishi yake yana athari hizo hizo kwa Serikali iliyopo sasa madarakani.

Lakini kwanini Balile anafanya hivyo? Jibu ni jepesi, ni hulka yake. Edward Lowassa anazo habari za Balile, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete naye anazo. Siwezi kumzungumzia Hayati Rais Dk. Magufuli katika hili kwa sababu sasa hana kauli, dada yangu Rais Samia bila kujali kama unazo au lah, kwa sababu maandiko yake mengi ya sasa amekuwa akiyaelekeza kwako, ninakudokeza kidogo, hiyo ndiyo hulka ya Balile.

Sasa kuhusu Tundu Lissu ambaye amekuwa akitumiwa sana na Balile kumchafua Hayati Rais Dk. Magufuli na kukuvika kilemba cha ukoka wewe dada yangu Rais Samia ili tu kutimiza ajenda zake.

Iko hivi; Baada ya kushambuliwa kwa Lissu, mambo mengi yalisemwa, mengi ya yaliyosemwa yalikuwa ni uvumi au habari za kusikia. Sijapata kuona ripoti yoyote ya kiuanahabari zaidi ya ripoti ya Mchokonizi aliyefanya utafiti kuhusu mwenendo mzima wa tukio hilo. Wote wamekuwa wakidemka demka tu, wakicheza ngoma wasiyoijua.

Lissu alishambuliwa Septemba 7, 2017 alipokuwa akitoka kwenye kikao cha Bunge kurejea nyumbani kwake eneo la area D, jijini Dodoma kwa mapumziko ya mchana. Nyumba aliyokuwa akiishi ilikuwa jirani na makazi ya Naibu Spika ambaye sasa ni Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Familia ya Spika Dk. Tulia ilihusika kwa karibu kutoa msaada kwa Lissu baada ya kushambuliwa na gari lililompeleka Hospitali akiwa mahututi baada kutendewa kitendo kile cha kikatili lilikuwa la Spika Dk.Tulia.

Balile na wenzake hawajapata kusema lolote kuhusu kitendo hicho cha Spika Dk. Tulia kutoa msaada wa kiutu kwa Lissu. Wanafahamu kuwa aliyemteua Dk. Tulia kuwa mbunge ni Hayati Rais Dk. Magufuli, wanafahamu kuwa harakati zake za kuwania unaibu Spika kama zisingekuwa na baraka za Hayati Rais Dk. Magufuli zisingefanikiwa hivyo kwa namna yoyote ile Hayati Rais Dk. Magafuli asingeshindwa kumshughulikia kama kungekuwa na ugiza unaohubiriwa na Balile.

Anayelengwa na akina Balile katika hilo ni Rais Samia. Wanajua kuwa kabla ya Rais Samia kwenda Kenya kumjulia hali, Spika Dk. Tulia alihusika moja kwa moja kusaidia kuokoa maisha yake lakini kwa sababu maslahi yao hayapo kwake hawana muda naye, wanashughulika na dada yangu Rais Samia.

Lissu akiwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, gharama za matibabu yake zilipaswa kubebwa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), kama ulivyo utaratibu wa matibabu kwa wabunge, mawaziri na maspika wastaafu. Balile anapaswa kufahamu kuwa wabunge wote ni wanachama wa NHIF kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji Bunge, Sura Na.115 ya Mwaka 2008.

Ifahamike hapa kuwa utaratibu wa matibabu kwa wabunge na mawaziri, matibabu yao nje ya nchi huwa yanasimamiwa na Bunge lenyewe.


Kunapokuwa na mahitaji ya mbunge kutibiwa nje ya nchi, jopo la madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) au Moi ndiyo hushauri na ndizo taasisi pekee zenye mamlaka ya kupendekeza kwa Wizara ya Afya.

Ni muhimu kufahamu kuwa kwa mujibu wa taratibu hizo ili matibabu ya nje yafanyike ni sharti mbunge atibiwe katika hospitali za ndani zilizosajiliwa na NHIF na inaposhindikana ndipo rufaa ya kwenda Muhimibili au Moi hutolewa. Hilo lilikuwa limeishaanza kufanyika kwa Lissu ambaye alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Kwa waliopata fursa ya kuperuzi makabrasha muhimu ya Bunge, wanaelewa kuwa mbunge anapopata rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi, Wizara ya Afya hutakiwa kuweka bayana hospitali anayokwenda kutibiwa, muda wa awali wa matibabu na endepo kuna hitaji la kusindikizwa na mwana familia, Daktari au muuguzi.

Wajibu wa Bunge baada ya kupokea rufaa ni kufanya maandalizi ya safari ikijumuisha gharama za matibabu ya mwanzo, kununua tiketi ya ndege, posho ya kujikimu kwa mbunge na msindikizaji au wasindikizaji na kibali cha kusafiri nje ya nchi.

Utaratibu wa kutolewa kibali na rais kwa kiongozi yoyote anayesafiri nje ya nchi uliwekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Lissu alipaswa kupata kibali hicho kabla ya kusafiri na hakukuwa na shaka yoyote kuwa angepewa kwa sababu haijapata kutokea mbunge akakosa kibali cha Ikulu cha safari ya nje ya nchi kwa matibabu.

Sasa Bunge linazo taratibu zake na mojawapo inaonyesha kuwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo, matibabu endelezo ya wabunge na familia zao hufanyika nchini India katika Hospitali ya Apollo isipokuwa kama inapendekezwa vinginevyo kulingana na aina ya matibabu yanayotakiwa kutokuwepo India na katika Hospitali ya Apollo, hapo uamuzi mwingine hufanyika.

Hivyo, taarifa zilizopo na ambazo hazijapata kukanushwa na yeyote ukiachilia mbali maneno ya uzushi ya akila Balile, jukumu la matibabu aliyoanza kupatiwa Lissu katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma lilibebwa na NHIF chini ya usimamizi wa Bunge.

Kama Serikali ya Hayati Rais Dk. Magufuli ingekuwa na nia mbaya na Lissu haina shaka hayo yote yasingefanyika.

Watanzania wanapaswa kufahamu kwamba wakati jitihada za kuokoa maisha ya Lissu ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Dodoma zikiendelea, baadhi ya wabunge wa Chadema wakiongozwa na Freeman Mbowe, na pamoja nao alikuwepo Dreva wa Lissu na wafuasi wengine wa Chadema, walizingira eneo la chumba cha upasuaji wakishinikiza kumchukua Lissu wamempeleke kumtibu mahali wanapopajua wao.

Taarifa hizi zipo wazi, Balile akizitafuta atazipata na atajua kuwa purukushani iliyosasabishwa na Mbowe na wenzake hospitali hapo ilidumu kwa muda mrefu huku walinzi wa hospitali wakipambana na kundi hilo lililokuwa na watu wenye hasira na jazba.

Ilikuwa ni purukushani hasa iliyoutisha uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ambayo iliomba msaada wa Askari Polisi kuja kuituliza.

Dada yangu Rais Samia siyo tabia ya Mchokonozi kuandika waraka mrefu unaochosha kusoma. Na katika umri wa utu uzima alionao sasa Mchokonozi, anahitaji kukata kiu kila baada ya muda mfupi, hivyo narejea tena kukuomba uridhie niweke kalamu yangu chini nirudi kwa mama yoyoo nikakate kiu, kisha nitarejea.

Kwenu ninyi wachokonozi, nimeikisikia kiu yenu ya kutaka kuusikia mkasa wa viongozi watakatifu wa dhambi. Narejea ahadi yangu kwenu. Waraka huo nitauleta haraka iwezekanavyo.

Nitafanya hivyo ili kuufahamisha uuma aina ya viongozi tulionao. Nitaandika kwa kuweka ushahidi hadharani ili kuondoa wasiwasi wa aina yoyote ya kile nitakachoandika. Nitaandika ili umma ufahamu kuwa wapo viongozi wanaocheka na viongozi wenzao kinafiki lakini wakiwapa mgongo, wanawapaka matope.

Sitaacha kuandika kuhusu nguvu walizonazo wanazozitumia kukiuka taratibu za taasisi nyeti. Sitagusa hata kidogo maisha yao binafsi ambayo ninayajua vizuri lakini nitaandika kwa tuo jinsi kauli na matendo yao yanavyoweza kuchafua taswira ya taaaisi nyeti za Serikali ikiwemo sura ya Dola.

NAKUJA…

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya