Monday, December 23, 2024
spot_img

MAKOFI MATATU YA RAIS SAMIA TAMISEMI

Rais Samia Suluhu Hassan

                              

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

RAIS Samia Suluhu Hassan ameisisimua kwa makofi matatu mazito, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa (TAMISEMI).

Taarifa kuwa Rais Samia, ambaye TAMISEMI ipo chini ya ofisi yake imekumbana na makofi yake matatu mazito zimetolewa jana na waziri wa wizara hiyo, Innocent Bashungwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyikia Jijini Dodoma.

Katika mkutano huo, Waziri Bashungwa alieleza kuwa Rais Samia amekuwa akiachia makofi yake kwa vipindi tofauti katika muda wa takribani mwaka mmoja sasa tangu aliposhika madaraka ya urais na kwamba makofi hayo yamekuwa na uzito tofauti tofauti ingawa yote ni mazito.

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa

 

Waziri Bashungwa alisema thamani ya uzito wa makofi ya Rais Samia kwa TAMISEMI inafikia Shilingi bilioni 1.49, fedha nyingi ambazo zimeweza kuzisisimua sekta tatu zinazosimamiwa na wazira yake. Alizitaja sekta hizo kuwa ni elimu, afya na barabara.

Moja ya shule mpya zinazojengwa na Serikali ya Awamu ya Sita
 

Akifafanua, Waziri Bashungwa alisema kofi la kwanza la Rais Samia lililotua sekta ya elimu lilikuwa na thamani ya Shilingi bilioni 662.32 ambazo zilisisimua shughuli za miradi mbalimbali ya ujenzi wa shule mpya, vyumba vya madarasa, vituo shikizi na shule za sekondari.

Miradi mingine iliyosisimuliwa na kofi hilo la Rais Samia ambalo uzito wake una thamani ya Shilingi bilioni 662.32 ni ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari, ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya maabara, ujenzi wa matundu ya vyoo kwa shule za msingi na sekondari na ujenzi wa mabweni kwa shule za msingi na sekondari.

Alitaja pia miradi ya ujenzi wa nyumba za walimu kwa shule za msingi na sekondari, maabara kwa shule za sekondari, mabwalo kwa shule za sekondari, majengo ya utawala kwa shule za sekondari na

ukarabati wa shule kongwe za msingi na sekondari.

Waziri Bashungwa alisema fedha hizo zimewezesha kujengwa kwa shule mpya 257 za sekondari na shule tisa za msingi, vyumba vya madarasa 18,219 kwa shule za msingi, vituo shikizi na shule za sekondari, vyumba vya madarasa 4,525 kwa shule za msingi na sekondari, ujenzi wa vyumba vya maabara 1,399 na matundu ya vyoo 568 kwa shule za msingi na sekondari.

Pia ujenzi wa mabweni 170 kwa shule za msingi na sekondari, nyumba za walimu 42 kwa shule za msingi na sekondari, maabara 11 kwa shule za sekondari, mabwalo sita kwa shule za sekondari, majengo ya utawala manne kwa shule za sekondari na ukarabati wa shule kongwe nne za msingi na sekondari.

Akizungumzia kofi la pili la Rais Samia kwa wizara yake, alisema, lilielekezwa Sekta ya Afya na uzito wake ulikuwa na thamani ya Shilingi bilioni 234.41 ambazo ziliwezesha kusisimua miradi ya ujenzi wa vituo vya afya, hospitali mpya, majengo ya wagonjwa mahututi, majengo ya dharura, kituo cha afya na nyumba za watumishi wa sekta hiyo.

Mchoro wa Hospitali ya Mwalimu Julius Nyerere inayojengwa mkoani Mara

 

Alitaja pia ujenzi wa zahanati, hospitali za halmashauri, uendelezaji hospitali za halmashauri na ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa hospitali.

Akifafanua kwa kutaja idadi ya miradi iliyotekelezwa, Waziri Bashungwa aliwaambia waandishi wa habari kuwa miradi iliyotekelezwa kwa fedha hizo ni  ujenzi wa vituo vya afya 288, ujenzi wa hospitali mpya 28, majengo ya wagonjwa mahututi 26, majengo ya dharura 80 (Emergency Medical Department- EMD) na kituo kimoja cha matibabu ya magonjwa ya milipuko.

Miradi mingine na idadi yake ni ujenzi wa nyumba 150 za watumishi za tatu kwa moja katika maeneo ya pembezoni, ukamilishaji wa zahanati 615,ukamilishaji wa hospitali 68 za halmashauri  zilizoanza kujengwa mwaka wa fedha 2018/19, uendelezaji ujenzi wa hospitali 31 za halmashauri na ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa hospitali 31.

Kofi la mwisho la Rais Samia kwa wizara hiyo ambalo uzito wake ulikuwa na thamani ya Shilingi bilioni 597 aliliekeza katika Sekta ya Barabara na liliweza kusisimua miradi ya matengenezo na ukarabati wa barabara za wilaya zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini – TARURA, alizozitaja kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 213.36, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe zenye urefu wa kilomita 1,152.33, matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 25,059.4, ujenzi wa madaraja 201 ambapo ujenzi unaendelea, ujenzi wa maboksi kalavati 70 na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 123.05.

Mojawapo ya barabara zinazojengwa sasa nchini

 

Haina shaka kuwa makofi haya ya Rais Samia kwa TAMISEMI ni mazito na ambayo kwa mara ya kwanza yameweza kuisisimua kwa haraka wizara hiyo katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo yeye Rais Samia aliinadi kwa Watanzania na ambayo amekuwa akiihubiri kuitekeleza kikamifu kila uchao.

Na iwapo kasi ya mapigo haya ya Rais Samia itaendelea kuwa na mitikisiko yenye kishindo kikubwa kiasi cha kusisimua hata miradi iliyokwama kutekelezwa kwa muda mrefu, historia inaweza kuandikwa upya tena, na huenda ikabakia kusomwa hivyo kwa muda mrefu ujao, kuwa; ‘katika kipindi cha uraisi wa rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania ambaye hakutegemewa na wengi kuyamudu madaraka makubwa kabisa ya kuliongoza taifa hilo; Tanzania, Afrika na dunia ilimshuhudia rais huyo akiandika historia ya kiuongozi ambayo haijapata kuvunjwa kwa miongo kadhaa sasa.’

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2020

 

Tukiachilia mbali mapigo ya makofi matatu mazito ya Rais Samia kwa TAMISEMI, Waziri Bashungwa alieleza kuwa mwenendo wa makusanyo ya mapato ya ndani kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka wa fedha 2018/19 hadi 2021/22 (kwa kipindi cha Julai hadi Disemba) imeonesha ongezeko la makisio na makusanyo.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2018/19 makusanyo halisi yalikuwa Shilingi bilioni 661.69. 2019/20  makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 717.24, 2020/21 makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 757.05 na 2021/22 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai  hadi Disemba 2021, makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 460.16 kati ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 863.85.

Waziri Bashungwa alizungumzia pia utolewaji fedha za asilimia 10 zinazotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Katika hilo alieleza kuwa mikopo hiyo imekuwa ikitolewa kwa kipindi kirefu lakini baada ya kuwepo changamoto mbalimbali, mwaka 2018/19 Serikali kupitia sheria ya fedha, ilirekebisha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 na kuongeza kifungu cha 37A kinachoruhusu usimamizi wa utoaji wa fedha za mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri. 

Mikopo kwa vijana

 

Aidha, alisema kuwa mwaka 2019 zilitungwa kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo na mwaka 2021 kanuni hizo zilifanyiwa marekebisho.

Kwa maneno yake mwenyewe, alisema, “utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri umeendelea kuimarika hususan baada ya kutungwa kwa sheria inayosimamia utaoaji wa mikopo hiyo.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19 hadi Januari 2022, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 164.16 kwa vikundi 38,573 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Kati ya vikundi hivyo, vikundi 23,944 ni vya wanawake, vikundi 11,528 ni vya vijana na vikundi 3,101 ni vya watu wenye ulemavu. Aidha zaidi ya ajira 390,000 zimezalishwa kutokana mikopo hiyo.”

Mikopo kwa wanawake

 

Akihitimisha, alisema, “katika kipindi hicho Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeweza kukusanya  marejesho yanayotokana na mikopo zaidi ya  Shilingi bilioni 81 ambazo zimetumika kukopeshwa tena katika vikundi 46,610, ambapo vikundi 29,057 ni vya wanawake, 14,383 ni vijana na vikundi 3,170 ni vikundi vya watu wenye ulemavu.”

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya