Monday, June 23, 2025
spot_img

MABILIONI YASOMBWA KWENYE VIROBA BENKI YA I & M DAR

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

BENKI ya I&M ya mkoani Dar es Salaam inadaiwa kuidhinisha kutolewa kwa mabilioni ya fedha taslimu za kitanzania kutoka kwenye akaunti ya mteja wake mmoja ambaye amekuwa akizisomba fedha hizo kwenye viroba na maboksi akizipeleka mahali kusikojulikana.

Taarifa za kutolewa kwa fedha hizo Benki ya I&M na kusombwa kwenye viroba, zimetolewa na wasiri wa Tanzania PANORAMA Blog huku Benki ya I&M na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zikinyamazia kimya maswali yaliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa na mteja anayechukua mamilioni ya fedha taslimu na kuyasomba kwenye viroba na maboksi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, katika kipindi cha miezi mitano, zaidi ya shilingi milioni 800 zilitolewa katika benki hiyo na kusombwa huku muingizaji wa fedha hizo kwenye benki hiyo akiwa hafahamiki.

Vyanzo vya habari vya PANORAMA vimeeleza kuwa sakata la uchotwaji wa fedha hizo linaumiza vichwa vigogo. Kwamba kwa upande wa I&M Benki, hakuna afisa anayeweza kulizungumzia na kwa Benki Kuu ya Tanzania hali ni hiyo hiyo.

“Hii ni kashfa nyingine kubwa kuwahi kutokea , angalia mlolongo wa jinsi fedha zilivyokuwa zinachotwa, angalia. I&M ukiwauliza hili wanakimbia ofisini, watu wa Benki Kuu nao tulishawapenyezea hii lakini walikosa ubavu wa kulifikisha kwa wakubwa zao.

“Hata ukiwauliza wewe hawawezi kulizungumzia hili, wakisikia tu uchotwaji wa fedha kutoka I&M wanakuwa wa baridi kabisa. Ndiyo maana wakati mwingine wakubwa wanawafukuza watendaji wa chini, wapo wapo tu, wanapwaya sana, mikogo tu lakini hawana uwezo wowote, we waulize kama watakujibu.

“Hamna, watakupigapiga chenga tu watakimbia. Hapa labda apatikane Gavana mwenyewe, huyo nasikia hana mchezo, lakini hao wa chini ni kama wanajua kitu fulani, wapo wanasubiri mshahara mwisho wa mwezi, basi,” alisema mmoja wa watoa taarifa.  

Taarifa zinaonyesha salio la kwanza kwenye akaunti ambayo fedha hizo zimekuwa zikichotwa lilikuwa shilingi 16,230.06. Mwezi mmoja baadaye, akaunti hiyo iliingiziwa shilingi milioni 241,191,000.

Siku tatu baada ya kuingizwa kwa fedha hizo, zilitolewa shilingi milioni 50 taslimu na siku iliyofuata, kiasi kingine kama hicho, shilingi milioni 50, kikiwa ni fedha taslimu  kilichukuliwa.

Siku iliyofuata shilingi milioni 110, zikiwa ni fedha tasilimu zilichotwa katika mikupuo miwili kutoka kwenye akaunti hiyo, mkupuo kwanza zilichotwa shilingi milioni 60 na mkupuo wa pili zilichotwa shilingi milioni 50.

Taarifa zinaeleza zaidi kuwa siku iliyofuta, Benki ya I&M iliidhinisha kutolewa kwa fedha nyingine milioni 31, zikiwa ni fedha taslimu ambazo pia zilisombwa kwa utaratibu huo huo wa kubembwa kwenye maboksi.

Kwa mujibu wa mlolongo wa uwekwaji na utolewaji wa fedha hizo kwenye Benki ya I&M, takriban mwezi mmoja baadaye akaunti hiyo hiyo iliingiziwa shilingi milioni 150 na siku hiyo hiyo fedha hizo zilitolewa zote ambapo Benki ya I&M ilimlipa fedha taslimu mchukuaji.

Siku tisa baadaye akaunti hiyo iliingiziwa shilingi milioni 43 ambazo muda mfupi baadaye, mtu anayetajwa kwa jina la Deepak Patel alichukua shilingi milioni 42.


 

Taarifa zinazidi kuonyesha kuwa katika muda wa siku zisizozidi 14 akaunti inayotumika kuchota mamilioni hayo iliingiziwa shilingi milioni 250 kwa mikupuo miwili, mkupuo wa kwanza ukiwa wa shilingi milioni 100 na mkupuo wa pili ukiwa na kiasi cha shilingi milioni 150.

Siku hiyo hiyo ikiwa ni muda mfupi baada ya fedha hizo kuingizwa, Benki ya I&M ilidhinishwa kutolewa kwa fedha taslimu, shilingi milioni 149, kisha ikaruhusu tena kutolewa kwa fedha taslimu shilingi milioni moja.

Siku iliyofuata fedha hizo ziliendelea kuchotwa kwa mtindo huo huo kwa benki kumlipa mchotaji fedha taslimu ambapo aliidhinishiwa kuchotwa shilingi milioni 100.

Siku nane baada ya kutolewa kwa kiasi hicho, akaunti hiyo iliingiziwa shilingi milioni 126,256,000 na muda mfupoi baadaye Benki ya I&M iliidhinisha kutolewa kwa fedha taslimu shilingi milioni 126. Zote hizo zilisombwa kwa utaratibu ule ule.

Wiki mbili baadaye akaunti hiyo iliingiziwa shilingi milioni 145,376,000 ambazo zilizotolewa hapo hapo kwa utaratibu ule ule wa fedha taslimu. Kwanza zilichotwa shilingi milioni tatu kisha Benki ya I&M ikaidhinisha kuchotwa kwa shilingi milioni 142, zikiwa ni fedha taslimu.

Februari 4, 2022 Tanzania PANORAMA Blog ilifika Makao Makuu ya Benki ya I&M, yaliyopo barabara ya Maktaba katika jengo la Maktaba, ghorofa ya kwanza ili kujua undani wa mtiririko wa uingizwaji na uchotwaji wa fedha hizo kwa mtindo wa uchukuaji fedha taslimu na namna ya usafirishaji wa fedha hizo ambapo ilikutana na Meneja Biashara na Habari wa benki hiyo, Anitha Pallangyo.

Meneja Biashara na Habari wa Benki ya I&M, Anitha Pallangyo

 

Pallangyo alipoulizwa kuhusu utaratibu na mwenendo wa uwekwaji na kutolewa kwa njia ya fedha taslimu kwa mamilioni hayo aliomba apewe muda ili aweze kuwasiliana na mabosi wake ndipo atoe majibu.

Muda mfupi baadaye, Pallangyo alirejea akiwa na kurasa chache za magazeti zilizochapishwa tangazo la Benki ya I&M likionyesha viwango vya fedha vya ufungaji akaunti na mambo mengine na kuomba aandikiwe maswali ambayo Tanzania PANORAMA Blog ilitaka kupatiwa majibu kisha atumiwe kwa njia ya barua pepe ili ayajibu akiwa ametulia.

Takwa hilo la Pallangyo lilitekelezwa na Tanzania  PANORAMA Blog ambayo alikuwa ameipatia kadi yenye mawasiliano yake. Hata hivyo, Pallangyo alikaa kimya, hakujibu maswali hayo.

Februari 8, 2022 Tanzania PANORAMA ilimwandikia ujumbe mfupi Pallaghyo ikimtaarifu kuwa imekwishamtumia maswali kama alivyotaka lakini katika hatua ya kushangaza, alijibu akihoji alichotumiwa ni nini. Alipopigiwa simu hakupokea, muda mfupi baadaye, aliizima kabisa, ikawa haipatikani.

Februari 9, 2022, Blog hii ilimtumia tena ujumbe wa maandishi kwenye simu yake Pallaghyo kumweleza kuwa inamtafuta kwa simu lakini hapatikani, ujumbe huo hakuujibu.

Ili kujiridhisha na taarifa ilizokuwa imepewa na wasiri wake, Februari 14, 2022 timu ya PANORAMA ilifika tena Benki ya I&M kuonana na Pallangyo ambaye alikuwa amekata mawasiliano ya simu na PANORAMA, hapo ilielezwa kuwa yupo kwenye kikao na haifahamiki atatoka baada ya muda gani.

Ombi la kuonana na meneja wa benki au kiongozi mwingine yoyote lilikataliwa kwa maelezo kuwa katika benki hiyo, afisa anayeruhusiwa kuonana na kuzungumza na waandishi wa habari ni Pallangyo peke yake.

Tanzania PANORAMA kabla ya kuondoka kwenye benki hiyo iliandika ujumbe wa kumfahamisha Pallangyo kuwa ilifika ofisini kwake na pia kusikitishwa na kitendo chake cha kukata mawasiliano ya simu na PANORAMA Blog na pia kutojibiwa kwa maswali yake.

Saa 5.54 ya Februari 12, 2022, Pallaghyo aliandika ujumbe mfupi akitaka atumiwe upya maswali na pia yatumwe kwa mwenzake aliyemtaja kwa jina la  Debora Mwakyoma. Dakika moja baada ya kutuma ujumbe huo, alituma ujumbe mwingine akieleza kuwa hakuwepo ofisini kwa siku kadhaa na simu yake iliibiwa hivyo hakuwa hewani.

Februari 15, 2022 Blog hii iliwasiliana na Pallangyo kumkumbusha kujibu maswali aliyoulizwa, naye alijibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi kuwa yupo hospitali kwa matibabu, lakini maswali yanashughulikuwa na wahusika na ndani ya nusu saa yeye au Debora watatuma majibu. Kauli hiyo nayo haikutekelezwa na Pallangyo.

Tanzania PANORAMA Blog haikuchoka kusaka kauli ya Benki ya I&M kwani saa 12. 33 ilimwandikia tena Pallangyo kumkumbusha, naye dakika moja baadaye aliandika akiomba akumbushwe kesho yake asubuhi.

Februari 16, 2022 PANORAMA iliwasiliana na Pallangyo ikimkumbusha kujibu maswali aliyotumiwa. Saa 3.59 aliandika alijibu kwa ujumbe wa maandishi kuwa wanayafanyia kazi maswali hayo.

Alipokumbushwa mchana wa siku hiyo, akaandika tena ujumbe mfupi kuwa anamkumbusha bosi wake ajibu.

Baada ya mawasiliano hapo, Pallangyo alikata tena mawasiliano na Tanzania PANORAMA Blog mpaka hivi sasa hapokei simu wala kujibu ujumbe wa simu.

Afisa Habari Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Vicky Msina

 

Kwa upande wa BoT, nako hali ilikuwa ile ile iliyoelezwa na wasiri wa PANORAMA. Awali PANORAMA ilimtafuta msemaji wa taasisi hiyo, Vicky Msina kuzungumzia taratibu zilizowekwa na taasisi yake ambayo ni msimamizi wa mabenki yote nchini.

PANORAMA ililenga kumuuliza Msina kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa na mabenki katika utoaji fedha taslimu ambazo ni nyingi, yeye alisema yuko safarini mkoani Mbeya na kuomba maswali ya PANORAMA yatumwe kwa afisa mwenzake aliyemtaja kwa jina la Lwaga Mwambande.

Afisa Habari wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Lwaga Mwambande

 

Tanzania PANORAMA ilitekeleza maelekezo ya Msina kwa kumtumia Mwambande maswali lakini kama ilivyoelezwa na wasiri wake, hadi sasa zikiwa zimepita siku saba, Mwambande ameshindwa kujibu chochote na kila anapoulizwa ama hapokei simu wala kujibu ujumbe wa maandishi na alipopokea alisema mchakato wa majibu unaendelea kwenye idara husika.

Tanzania PANORAMA Blog inaendelea na jitihada za kumtafuta Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga ili azungumzie sakata hili.

RIPOTI HII ITAENDELEA KESHO.  

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya