Marehemu Mchungaji Getrude Rwakatare |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
IKIWA ni takriban miaka miwili sasa tangu aliyekuwa Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God- Mlima wa Moto na Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Getrude Rwakatare afariki dunia, watoto wake wameingia katika ugomvi mkubwa wa kugombania mali zake.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog kutoka kwa watu walio karibu na familia hiyo na kuthibitishwa na mmoja wa watoto hao, zimeeleza kuwa kizazi cha marehemu Mchungaji Rwakatare sasa kimefarakana na mfarakano huo kimeupeleka serikalini kikiiomba iingilie kati ili kila mmoja apate kufaidi utajiri mkubwa ulioachwa na marehemu Mchungaji Rwakatare.
Kwa mujibu wa taarifa, watoto hao ambao wamegawanyika katika makundi mawili, wanatuhumiani kughushi nyaraka na kuuza mali za marehemu Mchungaji Rwakatare, kukwepa kulipa kodi na kupeana kisogo katika kufaidi mabilioni ya fedha yanayotokana na mauzo ya mali za marehemu huyo.
Inadaiwa kuwa, watoto watatu wa marehemu Mchungaji Rwakatare wameungana wakiwa na nia moja ya kutwaa mali zote zilizoachwa huku wakimtenga mtoto mmoja ambaye amekuwa akipinga ufujaji wa mali hizo na ukiukwaji wa sheria unafanywa na wenzake kwa mali wanazoziuza ikiwemo kughushi nyaraka.
Katika kupinga hilo, mtoto huyo, Tibe Kenneth Rwakatare Disemba 31, 2021 alimuandikia barua Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kumueleza jinsi ndugu zake wanavyokiuka sheria na kutenda makosa ya jinai kwa kughushi nyaraka za mauzo ya baadhi ya mali za marehemu Mchungaji Rwakatare.
Barua hiyo isiyokuwa na kumbukumbu namba lakini yenye simu ya mkononi ya mwandishi, ina kichwa cha maneno kinachosomeka ‘mauzo batili plot no 259 Udindifu Bagamayo.’
Katika barua hiyo, Tibe anaandika kumweleza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa uuzwaji wa kiwanja hicho umehusisha nyaraka za kughushi pamoja na kutolipwa kwa kodi stahiki za Serikali.
Sehemu ya barua hiyo inasomeka hivi; ‘Mimi ni mmoja wa wasimamizi wa mirathi ya Marehemu Getrude Rwakatare, malalamiko yangu yanajengwa kama ifuatavyo; Plot no. 259 ilikuwa inamilikiwa na Marehemu Idd Hashimu Mbita, aliiuzia St. Marry’s International Ltd.’
Kwamba uhamishaji wa umiliki kutoka kwa Mbita kwenda St. Mary’s International Ltd haukufanyika hadi marehemu Mchungaji Rwakatare alipofariki mwaka 2020.
Tibe anaandika; ‘Baada ya mama yetu kufariki, wasimamizi wenzangu wa mirathi, yaani Kellen Rose Rwakatare Kuntu, Humphrey Kaulika Kenneth Rwakatare na Mutta Robbert Rwakatare kwa pamoja waliuza plot hii tena kwa bwana mmoja, mdogo wake mmiliki wa Kibo Complex bila kuwashirikisha wakurugenzi wengine wa St. Mary’s International Academy LTD.’
Tibe anaendelea kumwandikia waziri kuwa ndugu zake wameghushi nyaraka za mauzo ya kiwanja hicho ambapo muuzaji wa sasa inaonyesha kuwa ni Idd Hashimu Mbita ambaye ni marehemu.
Kwamba marehemu huyo anaonekana katika nyaraka zilizoghushiwa na ndugu zake kama muuzaji anayemuuzia mnunuzi wa sasa ambaye haonekani kwenye nyaraka za manunuzi, lengo likiwa kukwepa kulipa kodi ya Serikali.
Anaandika Tibe kuwa; ‘Huu uuzwaji umefanywa juu kwa juu.’
Haishii hapo Tibe, anaendelea kuandika akiemweleza Waziri kuwa amefuatilia suala la uuzwaji wa kiwanja hicho mpaka Ofisi ya Ardhi, Kanda ya Mashariki, Dar es Salaam na Bagamoyo lakini limekuwa halifanyiwi kazi kwa sababu ya rushwa.
Hapo anaandika hivi; ‘Mheshimiwa Waziri ninaomba kwa heshima na taadhima uingilie hili. Utengue mauzo hayo na mali ibaki St. Mary’s International Academy Ltd.’
Tibe alipoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu ugomvi huo alisema yeye amedhulumiwa haki yake na ndugu zake hivyo hakuwa na jingine zaidi ya kuandika barua hiyo.
“Mimi ndiye niliyeandika hiyo barua kweli, nimedhulumiwa haki yangu sina jingine. Kama una jambo la kunisaidia nisaidie lakini kama ni maswali sitaki na siwezi kuzungumza zaidi kwani haki yangu inapotea,” anasema Tibe.
Marehemu Mchungaji Getrude Rwakatare |
Taarifa zaidi zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimeeleza kuwa baada ya kufariki kwa marehemu Mchungaji Rwakatare, alfajiri ya April 20, 2020, kwa vipindi tofauti mmoja wa watoto wake amekuwa akitoweka kwenda mahali kusikojulikana na inadaiwa na watu walio karibu na familia hiyo kuwa amekuwa akijihusisha na mambo ya hatari.
Tanzania PANORAMA Blog ilimtafuta mtoto huyo (jina lake tunalihifadhi kwa sasa) ofisini kwake Sinza Afrika Sana kwa zaidi ya siku kumi bila mafanikio na kipindi hicho chote ilikuwa akielezwa kuwa ametoweka, hajulikani alipo.
ITAENDELEA