RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
KAMPUNI ya Glames International Trading Tanzania Ltd ya mkoani Dar es Salaam imetoa ufafanuzi kuhusu bidhaa zake aina ya nyembe kuuzwa kwa bei ya chini.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Glames Internatonal Trading Tanzania Ltd, Ashish Tilwani alisema nyembe zinazoagizwa na kampuni yake zilizobainika kuuzwa kwa bei ya chini katika soko la Mkoa wa Dar es Salaam, inawezekana ni zile zilizoibiwa kwenye ghala la kampuni yake lililoko Keko, Dar es Salaam.
Tilwani alisema Oktoba mwaka jana, kampuni yake iliibiwa mzigo mkubwa wa nyembe uliokuwa umehifadhiwa katika ghala la kampuni yake; mzigo ambao hadi sasa haujapatikana na kwamba anahisi ndiyo unaouzwa sasa kwa bei ya chini.
Alisema tukio la wizi huo aliripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na aidha, mfanyakazi mmoja aliyemtaja kwa jina la Richard Godfrey Msumpi, pamoja na walinzi waliokuwa lindo siku ya tukio walihojiwa na polisi lakini jitihada za kuupata mzigo uliobiwa hazikuweza kuzaa.
“Ninachoweza kusema ni kwamba kama kuna nyembe hizo zenye nembo ya inglish – super platinum zinazouzwa kwenye soko la Mkoa wa Dar es Salaam au hata nje ya mkoa kwa bei ya chini kiasi hicho basi ni zile zilizoibiwa kwenye ghala letu la Keko.
“Ni kweli, pamoja na bidhaa nyingine kampuni yangu ndiyo waagizaji wa hizi nyembe kutoka Japan. Lakini mwaka jana mwezi Oktoba, tuliibiwa katoni 40 za nyembe kutoka kwenye ghala letu la Keko, huo ulikuwa mzigo mkubwa sana.
“Nilitoa taarifa polisi kituo kikuu na walifanya uchunguzi kwa kuwahoji walinzi waliokuwa zamu siku ya tukio pamoja na mfanyakazi mmoja anayeitwa Richard Godfrey Msumpi lakini hawakufanikiwa kuupata mzigo huo.
“Naweza kuwapa namba ya kesi niliyofungua na jina la mpelelezi wa kesi hiyo ambaye licha ya jitihada kubwa sana za kuusaka mzigo huo lakini hajafanikiwa kuupata. Nadhani huu ndiyo mzigo wetu ambao wale wezi wanauuza kwa bei ya chini kwa sababu hawana uchungu nao,” alisema Tilwani.
Tilwani ametoa kauli hii baada ya Tanzania PANORAMA Blog, mapema wiki hii kuripoti kuwa baadhi ya wafanyabiasha wa nyembe wa Mkoa wa Dar es Salaam wanailalamika kampuni yake kwa kuangusha bei ya soko la nyembe nchini.
Walisema bei ya kawaida ya bidhaa hizo ni sh 500,000 mpaka 600,000 lakini Glames International Trading Tanzania Ltd inauza kwa bei ya chini ya shilingi 10,000 hadi 50,000.
Mkurugenzi Tilwani akizungumzia bei alisema ni kweli bei ya katoni moja ni sh, 500,000 mpaka 600,000 hivyo inashangaza kama kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaouza kwa bei ya chini.