Mhandisi Eva Fumbuka |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MKURUGENZI Mtendaji wa Pomy Engeneering Company Limited, Eva Fumbuka amekana kimsingizia aliyekuwa mfanyakazi wake ambaye kwa sasa ni merehemu (jina tumelifadhi), kufa akiwa anadaiwa pesa za mishahara ya wafanyakazi wa kampuni yake.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog juzi kwa simu yake ya kiganjani, Mhandisi Fumbuka alisema kauli yake kuhusu marehemu kufa akiwa na fedha za mishahara alizompatia kwa ajili ya kuwalipa mafundi na vibarua waliokuwa wakijenga miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera ni za kweli.
Mhandisi Fumbuka alisema ni kweli kampuni yake imepewa na Wakala wa Nishati Vijini (REA) kandarasi ya kujenga miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera lakini mafundi na vibarua wanaofanya kazi hiyo hawajui na hajapata kuwaona.
Alisema kazi ya kutafuta na kuajiri mafundi hufanywa na fundi mkuu na ndiye humpatia fedha kwa ajili ya kugharamia malazi, chakula na mishahara.
“Unaniliuza mambo ambayo mimi siyajua, hayo mambo anayepaswa kuyajibu ni marehemu huyo. Mimi hao mafundi na hao vibarua siwajui na sijaoata kuwaona, anayewajua ni yeye fundi mkuu ambaye ndiyo huwa anawatafuta.
“Mimi nilikuwa nampatia kila kitu, fedha zote kwa ajili ya kazi nilikuwa nampa lakini alikuwa mlevi sana. Nilimpa fedha kwa ajili ya mishahara ya mafundi na vibarua akaenda kuzinywea pombe, akaacha kuwalipa mafundi na amekufa ameacha madeni makubwa kijijini. Anadaiwa mpaka na mwenyekiti wa kijiji.
“Sasa hao wanaodai waulize kama mimi wananijua, waulize hata kama walikwishawahi kuiona sura yangu zaidi zaidi labda kunisikia tu. Kwa hiyo aliyekufa ndiyo alikuwa na pesa zao za mishahara, mimi siwajui na wao hawajui,” alisema Mhandisi Fumbuka.
Alipulizwa ni kwanini alikuwa anampa pesa mtu mlevi ambaye alikuwa hawalipi mafundi na vibarua, hakujibu.
Aidha, Mhandisi Fumbuka alipoulizwa iwapo ana uthibitisho wowote wa maandishi wa kumpatia fedha marehemu kwa ajili ya mishahara ya mafundi na vibarua pia hakujibu na badala yake alianza kufoka huku akitaka asifuatwe fuatwe.
Kauli hiyo ya Mhandisi Fumbuka imepingwa Benjamin Mwenda, aliyejitambulisha kuwa mmoja wa mafundi waliokuwa wakifanya kazi kwenye Kampuni ya Pomy Engeneering Company Limited, aliyesema marehmu hakuwa mlevi na kwamba alikufa katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada kuachana na wakaguzi wa kazi waliokuwa wametumwa na Mhandisi Fumbuka kwenda eneo la mradi kukagua mwenendo wa kazi.
Mwenda alisema madai kuwa marehemu alikufa akiwa na madeni mengi kijijini ni ya kweli lakini madeni hayo yanamuhusu moja kwam moja Mhandisi Fumbuka.
Akifafanua alisema marehemu ambaye alikuwa na jukumu la kuwaongoza na kuwasimamia mafundi na vibarua ilibidi aanze kukopa chakula kwa mama ntilie wa kijijini baada ya Mhandisi Fumbuka kutotuma fedha za mishahara kwa muda mrefu.
“Huyu mama sasa anataka kwenda mbali, yaani kamsingia marehemu kufa na mishahara yetu wakati sisi tunajua kabisa ni uongo halafu anamsingia tena na madeni ya kijijini wakati hayo madeni aliyasababisha yeye.
“Ukweli ni kwamba, kwanza asiseme kuwa hatujui, anatujua, anajua kuwa kulikuwa kuna mafundi katika eneo lake la mradi, muulizeni kama hatujui hizo pesa anazodai kumpa marehemu za mishahara ya mafundi na vibarua alikuwa anampa za nini kama hatujui?
“Lakini pili marehemu hakuwa mlevi, kwao ni Kibaha na ndipo tulipomzika na pia wapo ndugu zake ambao tulikuwa tunafanyanao kazi site, tunaomba waulizwe kuhusu tabia ya marehemu. Huyo mama alikuwa hatoi fedha sasa marehemu kama kiongozi alikuwa na wajibu wa kuhakikisha sisi tunapata sehemu ya kulala na chakula ndiyo maana baada ya mama kutotoa hela kwa muda mrefu, marehemu ilibidi aende kwa wanakijiji mama ntilie akawaomba wawe wanatupatia chakula kwa mkopo mpaka atakapotoa hela. Ndiyo kilichotokea na hadi anakufa huyo mama hakuwahi kulipa.
“Na siyo chakula tu hata gari la kubeba nguzo, marehemu ilibidi akope ili nguzo ziwe zinafika eneo la mradi, kiufupi marehemu alijitolea sana lakini huyo mama hana shukrani. Yapo mambo yake ambayo tunayajua sasa itabidi tayaseme. Nendeni kijiji cha Bukuku mkaangalie vifaa alivyofunga kwa sababu huko ule mradi aliufanya yeye, labda avibadilishe sasa lakini kama hivyo vilivyopo mtashangaa” alisema Mwenda.
Alipoulizwa Mhandisi Fumbuka kama ujenzi wa miundombinu ya umeme kijiji cha Bukuku, Kagera aliutekeleza yeye na madai kuhusu kutumia vifaa ambavyo havikununuliwa na kampuni yake alisema hajui kama aliwahi kupata zabuni ya kujenga miundombinu ya umeme katika kijiji hicho.
Awali, Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa Mhandisi Fumbuka anadaiwa na mafundi waliokuwa wakifanya kazi kwenye kampuni yake kuwa anamsingizia marehemu kufa na deni la malimbikizo ya mishahara ya waliokuwa wafanyakazi wake.
Inadaiwa, Mhandisi Fumbuka anadaiwa malimbikizo ya mishahara na waliokuwa wafanya kazi wake waliokuwa wakijenga miundombinu ya umeme kupitia miradi wa REA, unaotekelezwa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.