Thursday, May 15, 2025
spot_img

MAJALIWA AMWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA 31 WA APRM

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

 

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kutoa mchango wake kwenye mpango wa nchi za Afrika kujitathmini kiutawala bora (APRM) ili kuziwezesha nchi wanachama kujifunza kwake na yenyewe iweze kujifunza kutoka kwao.

Amesema; “Tutaendelea kuungana na nchi wanachama kwenye mpango huu wa APRM ili tuweze kuwa sehemu ya mchango wa maendeleo ya nchi nyingine na sisi pia tuweze kujifunza kupitia nchi hizo katika maeneo ya kuimarisha demokrasia na utawala bora, usimamizi wa uchumi na maendeleo ya jamii.”

Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo Ijumaa, Februari 4, 2022 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa 31 wa wakuu wa nchi na Serikali ambao ni wanachama wa APRM uliofanyika kwa njia ya video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma. Mkutano huo uliongozwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.

 

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

Alisema mpango huo pia una utaratibu wa kufanya tafiti kwenye nchi wanachama kwa kushirikiana na taasisi za nchi husika kuona masuala mbalimbali ya kimaendeleo, changamoto na namna ya kuzikabili changamoto hizo.

Waziri Mkuu Makaliwa alisema kuwa mpango huo pia unatoa mafunzo kwa jamii kupitia makundi mbalimbali ikiwemo vijana, wabunge, asasi za kiraia, wanawake na watu wenye ulemavu na makundi mengine yanayoshiriki katika masuala ya demokrasia na utawala bora na sekta ya uchumi.

“Tutaendelea kutoa mchango wa umoja wa Afrika na kuelezea mafanikio yetu na changamoto zetu katika umoja huo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa kupitia mpango huo, nchi wanachama zitaweza kupata mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji, ujenzi wa viwanda, kuongeza upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda, maliasili, uvuvi na madini.

“Haya yote yanaangaliwa namna ambavyo nchi inaweza kujipanga katika kuinua uchumi wake,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizunguzia ripoti ya pili alisema Tanzania iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya ripoti  hiyo na itawasilishwa kwenye kikao kijacho cha wakuu wa nchi wanachama wa APRM.

“Tanzania tunatarajia kupeleka taarifa kwa mara ya pili baada ya kupata tathmini ya nchi zote wanachama na sisi Tanzania kuona mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizozipitia,” alisema.

Katika mkutano huo ambao nchi za Namibia, Nigeria na Afrika Kusini ziliwasilisha ripoti za thamini za utendaji katika maeneo mahsusi kama lilivyo lengo la APRM, Burundi ilipokelewa kama mwanachama mpya na kufikisha nchi 42 zilizojiunga na mpango huo.

Katika mkutano huo, Rais Muhamad Buhari wa Nigeria amepitishwa kuwa mwenyekiti mpya wa APRM akichukua nafasi ya Rais Ramaphosa.

 


 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya