Ā
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Pomy Engeneering Company Limited, Eva Fumbuka anadaiwa kumsingizia marehemu (jina limehifadhiwa) aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni yake, deni la malimbikizo ya mishahara ya waliokuwa wafanyakazi wake.
Inadaiwa, Mhandisi Fumbuka anadaiwa malimbikizo ya mishahara na waliokuwa wafanya kazi katika kampuni yake ambayo imepewa Ā kandarasi ya kujenga miundombinu ya umeme na Wakala wa Nishati Vijini (REA) katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni, Benjamin Mwenda alieleza kuwa yeye alikuwa mmoja wa mafundi waliochukuliwa na Mhandisi Fumbuka kwenda kufanyakazi kwenye mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme Wilaya ya Ngara na hatimaye kutolipwa stahiki zake.
Alisema Mhandisi Fumbuka aliwatelekeza katika mazingira magumu ya kutokuwa na chakula wala malazi, yeye pamoja na mafundi wenzake kabla hajaamua kulihamishia kwa marehemu deni la mishahara walilokuwa wakimdai.
Katika mahojiano hayo, Mwenda alidai Mhandisi Fumbuka aliyafanya hayo Oktoba mwaka jana siku chake baada ya marehemu aliyefia eneo la mradi kuzikwa Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumzia kifo cha marehemu kilivyotokea, Mwenda alisema marehemu alikuwa msimamizi wao kazini na alikuwa kiongozi wa kudai malimbikizo ya mishahara yao. Kwamba wakati vuguvugu la kudai mishahara likiwa limepamba moto, wakaguzi wa kazi wa Kampuni ya Pomy walifika eneo la mradi na kupokelewa na marehermu.
Alisema marehemu aliwatembeza sehemu mbalimbali walizokuwa wamekwishasimamisha nguzo za umeme na baada ya ukaguzi alikwenda kula na muda mfupi baadaye alianguka, akafariki.
āTunamdai huyu Eva Fumbuka pesa zetu, tunamdai yeye kwa sababu sisi ni mafundi wa mtaani alikuja tu kuchukua kwenda kufanya kazi kwenye huo mradi wake huko Ngara. Tulifika eneo la mradi mwezi Julai mwaka jana, huo mwezi wa kwanza alitulipa lakini baada ya hapo akawa halipi.
āMaisha haya ni magumu sana kwa sasa, hivyo ukiwa na familia inayokutegemea umeiacha mbali kwenda kufanya kazi, tena kazi ngumu halafu huitumii hata senti kwa muda mrefu unaiua. Unaua watoto na mke kwa njaa.Ā
Ā
āMwezi Oktoba mwaka jana, tulifikia hatua mbaya, maana alikuwa hajatulipa kwa miezi miwili wakati sisi hatuna akiba yoyote, tunategemea pesa kidogo tunayopata kwa siku au wiki ndiyo familia ziishi na sisi wenyewe pia.
āWakati tunadai wakaja wakaguzi kuangalia kazi, bosi wetu ambaye ndiyo huyo marehemu akawa nao akiwatembeza eneo la mradi maana sisi kazi yetu ilikuwa ni kisimika nguzo.
āWalipomaliza kukagua alikuja akala na muda mfupi baadaye, kama saa tatu hivi akaanguka ghafla tu akafa, tulikuja kumzika Kibaha, kisha mimi nikarudi eneo la mradi kuendelea na kazi na nilirudi kwa sababu kulikuwa na hela zangu nyingi huko nilizokuwa nadai.
āVinginevyo nisingerudi kwa sababu tulikuwa tunafanya kazi kwa shida na hofu ilikuwa imetushika kutokana na mazingira ya kifo cha msimamizi wetu. Tulitamani sana ufanyike uchunguzi wa kifo chake.
āWale REA wanalipa wakandarasi bila shida na tunaambiwa walimlipa lakini yeye anatufanya sisi kama wanyama na hawa mabosi wa umeme huwa wanafanya wakijua mafundi wamejua mambo mabaya yanayofanya kwenye hiyo miradi. Sasa hatukuwa na fedha kabisa na familia hasa watoto hali zilikuwa mbaya.
āTulipoona hakuna dalili za kulipwa, tukagoma. Ndiyo wakaja watu wake Mhandisi Eva wakiwa na fedha kidogo, wakawalipa vibarua kila mmoja nusu wengine robo ya fedha walizokuwa wanadai, vibarua hao walikuwa kama 16 hivi lakini sisi mafundi hatukulipwa.
āTulipouliza kwanini sisi hatulipwi tukaambiwa kuwa bosi, yaani huyo mama Eva kasema mishahara yetu amekufa nayo marehemu kwa sababu alikuwa amepewa fedha nyingi sana zikiwemo za mishahara yetu.
āNi wazi kabisa marehemu alikuwa anasingiziwa hapo kwa sababu hadi anakufa tulikuwa tunadai pamoja na ndiyo alikuwa kiongozi wetu wa kudai mishahara sasa hizo pesa nyingi alipewa wapi?
āLakini kwa sababu huyu Eva anafahamika mambo yake tangu akiwa Tanesco Mikocheni tulijua ndiyo imekwisha hayo tuondoke yasije kutupata makubwa. Na ni kwa vile tu hii miradi haikaguliwi sawasawa lakini wakikagua hata vifaa anavyofunga kwenye siteanazojenga wataona maajabu.
āHatukuwa na namna tukatafuta nauli tukaondoka lakini mpaka leo bado tunamdai. Hapo tuna madeni makubwa ambayo familia zilikuwa zinakopa tulipokuwa huko Ngara. Kiujumla ametuharibia kabisa utaratibu wa maisha huyu mama, lakini Mungu yupo, atamlipia tu. Tusaidie wakubwa wajue kuna wakandarasi wabaya sana wanaoua watanzania wenzaoā alisema Mwenda.
Alipoulizwa jana Mhandisi Fumbuka kuhusiana na madai hayo alisema yote ni ya uongo na kwamba wanaotoa tuhuma hizo ni watu wenye nia ovu.
āHapa ninapoongea na wewe nipo Kyerwa huku Mkoa wa Kagera kwa shughuli zangu hizi hizi za umeme. Hakuna mtu anayedai hata shilingi moja na hakuna kifaa chochote cha Tanesco ambacho kimetumika katika eneo langu la mradi.
āSisi huku tunafanya kazi ya kusimamisha nguzo tu hakuna kingine na wafanyakazi waliokuwa wamesimamishwa walisimama kazi kwa sababu hakukuwa na vifaa. Hivi tunavyoongea ndiyo niko huku nawarudisha kazini kwa kuwatambulisha kwa wenyeviti wa vijiji baada ya vifaa kupatikana na unaweza kuwauliza hata wao,ā alisema Mhandisi Fumbuka,
Jitihada za kuwatafuta ndugu wawili wa marehemu anayedaiwa kusingiziwa kufariki akiwa na mishahara ya mafundi hao ambao walikuwa wakifanya kazi ya ujenzi huko Ngara chini ya Mhandisi Fumbuka ili kuzungumza kile wanachokijua kuhusu sakata hili zinaendelea.
Ā
Ā