Moja ya vifaa chenye nembo ya Tanesco kilichosimikwa katika barabara iliyopo Wilaya ya Buhigwe ambayo miundombinu ya umeme imejengwa na mkandarasi aliyepewa zabuni na REA |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
SASA kuna hekaheka Wilaya ya Buhigwe. Maofisa wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) wamefanya kikao na mafundi wanaojenga miundombinu ya umeme katika wilaya hiyo na kuwapa maelekezo ya kutozungumza na waandishi wa habari.
Haya yanajiri ikiwa ni siku chache baada ya kuripotiwa kuwepo kwa mkinzano wa taarifa kati ya maofisa wa Tanesco mkoani wa Wilaya ya Buhigwe na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhusu anayepaswa kubeba gharama za ununuzi wa vifaa vinavyotumika katika miradi ya REA kwenye Wilaya ya Buhigwe.
Januari 17, 2022 Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwepo kwa utata mkubwa kuhusu utaratibu wa utekelezaji miradi ya usambazaji umeme vijijini katika Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma.
PANORAMA iliripoti chanzo cha utata huo ni kukinzani kwa taarifa kuhusu anayepaswa kubeba gharama za ununuzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme, kati ya mkandarasi na serikali.
Na kwamba mkinzano huo wa taarifa unawahusisha Meneja Miradi wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Samsoni Mayama, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Hassan Saidy na Meneja wa Tanesco wa Wilaya ya Buhigwe, Elioza Kachira.
Juzi, January 19, 2022 PANORAMA ilidokezwa na vyanzo vyake vya habari vilivyopo eneo la mradi kuhusu kuwepo kwa kikao cha wafanyakazi wote wanaojenga miundombinu ya umeme Wilaya ya Buhigwe kilichodaiwa kuitishwa na Meneja wa Tanesco wa Wilaya ya Buhigwe, Kachira.
Taarifa hizo zilidai kuwa mafundi wote walitakiwa kutokwenda kazini na badala yake wafike ofisi ya Tanesco Buhigwe kuhudhuria kikao hicho ambacho ajenda yake kuu ilikuwa kumsaka ‘mchawi’ aliyevujisha siri kuhusu vifaa vya Tanesco kutumika katika miradi ya REA ambayo kwa mujibu wa Mhandisi Saidy inagharamia ununuzi wa vifaa hivyo.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilidai kuwa mafundi wote walipewa maelekezo kuwa wasiongee chochote na waandishi na habari watakaofika eneo la mradi kunakojengwa miundombinu hiyo na badala yake wakiwaona watu watakaowahisi kuwa ni waandishi, wapige simu polisi haraka au wawataarifu viongozi wa Tanesco wa wilaya.
“Hakukuwa na kazi leo, mafundi wote waliitwa na DM kwenye kikao. Kimeanza asubuhi na kimeisha mchana kabisa na ajenda ilikuwa kujadili nani anayetoa taarifa za vifaa vya Tanesco kutumika kwenye miradi ya REA.
“Mafundi wameambiwa vifaa vya Tanesco vinavyofungwa kwenye mradi huo vimekopeshwa kwa mkandarasi ambaye ameishiwa vifaa na mradi huo unatakiwa kukamilika haraka.
“Lakini DM amewaonywa wasiongee na waandishi wa habari ambao wanapitapita eneo la mradi kuchunguza mambo kwa sababu wanaweza kuingia kwenye matatizo na wakiona mtu anayefanana na mwandishi au anayepiga picha eneo la mradi, wapige simu polisi,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Alipoulizwa Meneja Kachira kuhusu kuwepo kwa kikao hicho alikanusha kwa kuelekeza kuwa hayupo eneo lake la kazi na hajui lolote kuhusu kikao hicho.
“Hakuna kikao tulichofanya. Mimi nipo Kigoma Mjini, nimekuja kwa sababu ya matatizo ya kifamilia. Hapa ninapoongea na wewe nimeishaanza likizo kwa hiyo sijui chochote.
Naye Meneja Miradi wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Samsoni Mayama alipoulizwa kama anafahamu lolote kuhusu kuwepo kwa kikao hicho naye alisema yupo likizo mkoani Mara hivyo hana taarifa zozote.
“Mimi sipo huko niko Musoma lakini hizo taarifa siyo sahihi. Ninachosema sijui na sikuhudhuria kikao cha jana,” alisema Mhandisi Mayama.