RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MFANYABIASHARA Hitek Parik, sasa anatajwa kuwa mtu tishio kutokana na mtindo anaoutumia kujikusanyia mamilioni fedha.
Parik anadaiwa kuvuna mamilioni fedha kwa njia za ulaghai kutoka kwa wakulima na wafanyabiashara na kwamba licha ya kufikisha polisi na kufunguliwa kesi zaidi ya kumi, bado yupo uraiani akiendelea na shughuli zake.
Mmoja wa watu walio karibu naye aliyezungumza na Tanzania PANORAMA jana, alisema Parik tangu alipoingia nchini amevuna mamilioni ya pesa na kwamba sasa anapambana kufanikisha mambo mawili ili atoweke.
Aliyataja mambo anayopambania Parik sasa kuwa ni kupata mkopo wa benki na pili kurudishiwa hati yake ya kusafiria ambayo inashikiliwa na polisi.
“Mnafanya kazi nzuri kwa sababu mnapaza sauti za wanyonge, natamani sasa vyombo vingine vingeichukua hii kazi yenu na kuifanyia kazi ili kubaini ukweli.
“Huyu mtu ni tishio, mimi namfahamu sana. Ile habari yenu ya kwanza ilipofika Mwanza wafanyabiashara walipigwa na butwaa kusoma kuwa kumbe ameishafanya haya mambo yake mikoa mbalimbali. Huko Mwanza amewatapeli zaidi ya milioni 70 wafanyabiashara.
“Wakulima nao ndio hao mamilioni ya pesa wanamdai, mazao yao kachukua na akipelekwa polisi ni mjanja mno anasema ni kweli wananidai najipanga nitalipa anaachiwa anaendelea kuchukua fedha za watu.
“Sasa ninachokijua mimi hivi sasa anataka kufyatua mabomu mawili kisha atoweke. La kwanza ni kupata mkopo wa benki ambao ameomba kwa kutumia hati ya shamba ambalo siyo la kwake na pili kupata pasipoti yake ili akishapata tu huo mkopo atoweke jumla,” alisema mmoja wa watu wa karibu wa mfanyabiasha Parik.
Parik mwenyewe alizungumza na Tanzania PANORAMA juzi na kukiri kuwa anafanyabiashara ya kununua, kusafirisha na kuuza mazao nje ya nchi lakini alipoulizwa kuhusu
kutowalipa wakulima aliochukua mazao yao, kufunga ofisi yake iliyopo Barabara ya Nyerere kwa lengo la kuwakwepa wanaomdai na mipango yake ya sasa ya kuchukua mkopo mkubwa kutoka moja ya benki zilizopo Mkoa wa Dar es Salaam kwa kutumia hati ya shamba ambalo siyo la kwake alisema haelewi lugha ya Kiswahili.
Aidha, Parik aliomba atafutwe baada ya saa moja atakuwa sehemu nzuri kujibu maswali aliyoulizwa lakini alipotafutwa baada ya muda huo hakupatikana na tangu siku hiyo simu yake haipatikani hewani.
Tanzania PANORAMA bado haijafanikiwa kuzungumza na uongozi wa benki ambayo Parik ameomba mkopo kwa kutumia hati ya shamba ambalo siyo la kwake na pia haijamfikia mwenye hati hiyo kuzungumzia suala hilo.
Juzi Tanzania PAANORAMA iliripoti kuwa Parik, mtanzania mwenye asilia ya kiasia ni mmiliki wa Kampuni ya Indo Africa Investment Limited na anadaiwa kuzunguka mikoa mbalimbali akijitambulisha kuwa ni mfanyabiashara mkubwa anayenunua mazao hasa kunde, mbaazi na choroko.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA kutoka kwa watu wa karibu na mfanyabiashara huyo, zimedai kuwa mikoa ambayo amekuwa akifika zaidi kukusanya mazao ni Manyara, Arusha na Mwanza.
Kwamba katika mikoa hiyo anao mawakala wake ambao humkusanyia mazao ya wakulima kwa ahadi kuwa yanakwenda kuuzwa nje ya nchi kwa bei ya juu hivyo wapokee fedha kidogo na baada ya kuuzwa watapewa fedha zilizosalia.
“Huyu mhindi amekuwa tatizo kubwa kwa wakulima, anatumia mawakala wake kukusanya mazao kutoka kwa wakulima na wakati mwingine huwa anafika mwenyewe lakini anakichofanya ni utapeli.
“Anajitambulisha kuwa ni mnunuzi mkubwa wa mazao anayefanya biashara ya kusafirisha na kuuza mazao nje ya nchi. Huwa anawapa wakulima pesa kidogo na kuwaahidi kuwa akishasafirisha mazao wanayompa na kuyauza nje atawapa pesa iliyosalia na wengi huwa wanakubali kwa sababu bei anayowaahidi ni kubwa. Lakini sasa akishachukua mazao huwa harejei na wakulima hawapati chochote,” alisema.
Inadaiwa zaidi kuwa baadhi ya wakulima waliompatia kiasi kikubwa cha mazao na yeye kutokomea nayo, walikwenda kumsaka katika ofisi zake zilizopo eneo la Karakana, Barabara ya Nyerere mkoani Dar es Salaam ambako walikuta amekwishafunga ofisi yake.
“Baada ya kuwa amechukua kiasi kikubwa cha mazao ya wakulima, aliifunga ofisi yake iliyopo eneo la Karakana, Dar es Salaam na shughuli zake akawa anazifanyia nyumbani lakini jitihada za kumsaka zilizaa matunda mwishoni mwa mwaka jana alipokutwa akiwa nyumbani kwake Upanga.
“Walipompata walimpeleka polisi, hivi ninavyozungumza na wewe ana kesi tofauti tofauti zaidi ya kumi ambazo zimefunguliwa mwaka jana mwezi Novemba lakini mpaka sasa hajafikishwa mahakamani.
“Na kwa taarifa za karibuni sasa ameamua kuhamishia hizo shughuli zake kwenye mabenki, kuna benki moja ameomba mkopo lakini huo mkopo hatumii dhamana yake, ametafuta watu wamemtafutie mkulima mmoja ambaye amepewa pesa ili ampatie hati ya shamba lake ndiyo aitumie kuchukulia huo mkopo benki, huyo mkulima naye baadaye atalia tu” alisema mtoa taarifa.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumaane Muliro |
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema yupo kwenye msafara hivyo atafutwe wakati mwingine.
TANZANIA PANORAMA INAENDELEA KUFUATILIA MKASA HUU.