Sunday, May 11, 2025
spot_img

TRA YATOA MSIMAMO LUGHA YA KICHINA KWENYE RISITI ZA EFD

Richard Kayombo

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

 

MAMLAKA ya Mapato (TRA) imetoa msimamo wa lugha zinazopaswa kutumika kwenye risiti zinazotolewa na mashine zote za kielekitroniki hapa nchni.

Imesema risiti zote za kielekitroniki zinazotolewa kwa wateja zinatakiwa zitumie lugha rasmi ambazo ni Kiingereza na Kiswahili na si vinginevyo.

Msimamo huo wa TRA umetolewa jana na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alipokuwa akijibu maswali aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu duka kubwa la kuuza mahitaji ya nyumbani (Supermarket) inayofahamika kwa jina la Tai Le China Supermarket, iliyopo Mikocheni, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam kutoa risiti za kielekitroniki zenye maandishi ya kichina.

Tanzania PANORAMA ilimuiliza Kayombo kuwa TRA imeanzisha lini utaratibu wa kutoa risiti zinazosoma maandishi ya lugha za kigeni na lugha ngapi za kigeni zilizoidhinishwa kutumika.

Katika majibu yake mafupi aliyoyatoa jana jioni, Kayombo alisema; “Risiti zote zinatakiwa zitumie lugha rasmi ambazo ni Kiingereza na Kiswahili na si vinginevyo.

“Ningependa kujua jina la supermarket hii ili meneja wetu wa Kinondoni alifanyie kazi.”

Wakati Kayombo akiomba jina la supermarket hiyo ili aliwasilishe kwa meneja wa TRA Kinondoni, Afisa Afya wa Kata ya Mikocheni, Fredy Ernest, mapema jana aliiambia Tanzania PANORAMA kuwa tayari maafisa wa taasisi hiyo wapo kwenye supermarket hiyo na kwamba alikuwa ameitwa kwenda hapo.

Tanzania PANORAMA ilimweleza Kayombo kuwa linazo taarifa kuwa tayari maafisa wa TRA wamekwishafika eneo hilo na ilimuomba aeleze walichobaini; swali hilo Kayombo hakulijibu.

Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata

 

Awali, Kamishna Mkuu wa TRA Alphayo Kidata ambaye aliulizwa pia kuhusu  suala hilo, aliitaka Tanzania PANORAMA kuwasiliana na Kayombo ili aweze kutoa majibu.

Mmoja wa wafanyakazi katika supermarket hiyo (jina linahifadhiwa) aliyezungumza na Tanzania PANORAMA alisema duka hilo lipo muda mrefu na utaratibu wake ni huo siku zote na maafisa wa serikali hufika kufanya ukaguzi na kuondoka hivyo anashangaa habari zao kuanza kuandikwa sasa.

“Mnajisumbua tu nyinyi, hii supermarket ipo hapa zaidi ya miaka mitatu na huu ndiyo utaratibu wao. Maafisa wa TRA, TBS hao OSHA wote wanakuja hapa kukagua na wanawaacha sisi nyie kuanza hizi hekaheka mnahangaika tu.

“Ni wajanja sana hawa, hivi kama wameweza kuwepo miaka mitatu nyie mtaweza leo? Tangu jana mpaka leo mnadhani watakuwa hawajabadilisha hizo mashine? Kwani kuweka hizo lebo inachukua muda gani? Kwani wao ni wajinga? Hili duka japo limejificha humu ndani lakini lina wateja wengi sana tena wakubwa.

“Wenzenu huwa wanakuja wanaongea nao wanaondoka sasa nyie mmeng’ang’ania. Mnajihangaisha tu,” alisema.  

Juzi, Tanzania PANORAMA Blog liliigundua Supermarket hiyo ikiwa na kibao kinachoitambulisha kwa jina la Tai Le China Supermarket katika eneo la Migombani, Kata ya Mikocheni na inamilikiwa na raia wa China aliyejitambulisha kwa jina moja la Wang.

Katika uchunguzi wake ndani ya supermarket hiyo, Tanzania PANORAMA ilibaini bidhaa zake nyingi zimeandikwa kwa lugha ya kichina pekee na hazijawekewa bei yoyote kwa mnunuzi (price tag) kama ulivyo utaratibu wa kawaida.

Baadhi ya bidhaa hizo ni mayai yenye rangi ya kijani kutoka China na yale yanayozalishwa hapa nchini, maziwa, dawa mbalimbali za mswaki, vinywaji baridi, pombe za aina mbalimbali na vyakula vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyama.

Aidha, uchunguzi ulibaini risiti za kielekitroniki zinazotolewa na supermarket hiyo zinaandikwa kichina isipokuwa bei ya jumla ya bidhaa inayouzwa inaandikwa kwa Lugha ya Kiswahili.

Meneja wa Tai Le supermarket,  aliyejitambulisha kwa jina moja la Khadija alisema duka hilo ni maalumu kwa ajili ya raia wa China pekee.

Khadija alisema bidhaa nyingi zinazouzwa hapo zinaagizwa kutoka China yakiwemo mayai yenye rangi ya kijani na taratibu zote za usajili na kufanya biashara zimefuatwa ikiwemo kupatiwa vibali kutoka serikalini.

“Hili duka ni kwa ajili ya raia wa China tu, halitoi huduma kwa watanzania. Ukiona mtanzania kaja hapa basi huyo ni mfanyakazi wa ndani katika nyumba za mchina au mtanzania aliyeishi China miaka mingi.

“Kama unasema ulikuwa na shida na bidhaa lakini hujaona bei yake kwanza jua umeingia katika duka ambalo wewe halikuhusu kwa sababu wewe siyo mchina lakini bei za humu haziandikwi kwa sababu wachina wenyewe wanajua bei zao ndiyo maana unaona wanalipa na wanaondoka bila shida.

“Ila kwa faida yako, humu hatuweki bei ya bidhaa kwa sababu katika siku za karibuni bei zinabadilika mara kwa mara, hivyo tunaweza kuweka leo kesho ikatulazimu kubadilisha tena, inakuwa ni usumbufu. Kwa hiyo bidhaa zetu tunauza kwa bei ya siku hiyo na unazipata hapo kaunta unapokwenda kulipia,” alisema Khadija.

Mmiliki wa Supermarket hiyo, yeye alisema duka lake lina msemaji ambaye ni Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mikocheni.

Eneo ilipo supermarket ya TaiLe

 

“Mimi siruhusiwi kusema lolote, yupo msemaji wa duka hili. Yeye atakujibu au atakupa kibali uje nacho hapa ndiyo mimi nizungumze. Nenda Ofisi ya Mtendaji wa Kata, hao ndio watawapa majibu, mimi siwezi kuzungumza na ninyi. Serikali Kata ndiyo wanaweza kuwapa kibali cha kufika kwangu, kuingia hapa na kuniuliza. Ni hapo mtaa wa nyuma nendeni mkaongea na hao,” alisema Wang.

Tanzania PANORAMA ambayo ilifika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mikocheni kufuatilia suala hilo na kuelekezwa kuzungumza na Afisa Afya wa Kata ya Mikocheni, Ernest ambaye alikiri kulifahamu duka hilo na kusema kuwa bidhaa zote zinazouzwa hapo ni halali na zina vibali vyote vya mamlaka za serikali vinavyohitajika.

Alisema duka hilo ni maalumu kwa ajili ya raia wa China peke yao na kwamba haliwahusu watanzania.

“Kwanza nashangaa mmefikaje huko na kuanza kufanya ukaguzi, nani amewaruhusu kwenda huko? Sisi ndio tuna mamlaka ya kuwaruhusu kuuliza maswali sio kufika na kuanza kuhoji, hiyo  siyo kazi yenu, lazima mpate kibali kutoka hapa.

“Tambua hiyo supermarket ni kwa ajili ya wachina tu, sio kwa ajili ya watanzania na ukiona mtu mweusi hapo basi huyo katumwa na mchina au aliwahi kuishi huko sasa amekwenda kununua bidhaa anazozijua. Watanzania hapo sio kwao,” alisema.

Alisema Mamlaka ya Udhibiti wa Bidhaa (TBS) ndiyo iliyotoa kwa Tai Le kibali cha kuingiza bidhaa zao nchini na kuuza zikiwa zimeandikwa kwa lugha ya kichina bila kulazimiki kuandika bei na kwamba maafisa wa taasisi za serikali hufanya ukaguzi kila mara.

Akizungumzia bei kutowekwa kwenye bidhaa alisema wanaopaswa kujibu ni TRA.

“Lakini labda hilo la kuweka bei kwenye bidhaa wanazouza kama inavyohitajika, najua lipo kisheria, sasa hili niseme kwamba siwezi kuliongelea, nenda kawaulize Mamlaka ya Mapato ambao wamewapa kibali na huwa wanakuja kukagua, wanajua kwanini mashine zao za kielektoniki zinaandika kichina, wao ndiyo watakupa ufafanuzi.

Aidha, Ernest alionya kuwa katika eneo la Kata ya Mikocheni waandishi wa habari hawaruhusiwa kufika kufanya kazi bila kupata kibali kutoka kwenye Ofisi ya Kata na kwamba mwandishi anayekiuka hilo anakiuka taratibu zilizowekwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni.

“Wako waandishi waliongia katika eneo la kata yangu na kuanza kuhoji watu bila kupitia ofisini kwangu. Ofisi ile ya mchina ilikuwa na tatizo la wafanyakazi walipofika mimi nilipigiwa simu na mchina akaniambia waandishi wamekuja, mimi nikapiga simu polisi nikaagiza wakawachukue waandishi wale niwakute polisi Oysterbay.

“Na huu utaratibu umewekwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni, Mkuu wa Wilaya aliyekuwepo aliusimamia na huyu aliyepo sasa anausimamia. Lakini sasa kwa sababu nyie mlikuwa mnapita ndiyo mkaingia humo kununua bidhaa basi ni vizuri tuelewane kuwa siku nyingine kama mnataka kufanya lolote mje kwanza mueleze mnachotaka kufanya na mpate kibali ndiyo muendelee,” alisema Ernest.

Tanzania PANORAMA INAENDELEA NA RIPOTI YA SAKATA HILI

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya