Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MAMLAKA ya Mapato (TRA) imeeleza kuwa imechukua hatua mahususi za kiutendaji kwa mujibu wa sheria dhidi ya duka kubwa la kuuza mahitaji ya nyumbani (Supermarket) linalofahamika kwa jina la Tai Le China Supermarket ambalo limekuwa likitoa risiti zilizoandikwa kichina kwa bidhaa linazouza.
Hayo yameelezwa leo mchana na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alipokuwa akizungumzia hatua zilizochukuliwa jana na maafisa wa mamlaka hiyo waliofika kwenye supermarket hiyo kufanya ukaguzi baada ya Tanzania PANORAMA Blog kuripoti madudu iliyobaini hapo.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRa, Richard Kayombo |
“Ni kweli maafisa walishafika hapo kwa ajili ya kufanyia jambo hilo kazi kwa kuchukua hatua mahususi za kiutendaji kwa mujibu wa sheria ambazo hata hivyo sheria haituruhusu kuzitoa hadharani.
“Hata hivyo, TRA inawashukuru sana PANORAMA na wananchi wenye nia njema ambao mara kwa mara wamekuwa wakitupatia taarifa za ukwepaji wa kodi,” alisema Kayombo.
Kauli hii ya Kayombo ilitanguliwa na ile aliyoitoa jana jioni alipotoa msimamo wa TRA kuhusu lugha zinazopaswa kutumika kwenye risiti zinazotolewa na mashine zote za kielekitroniki hapa nchini
Alisema risiti zote za kielekitroniki zinazotolewa kwa wateja zinatakiwa zitumie lugha rasmi ambazo ni Kiingereza na Kiswahili na si vinginevyo.
“Risiti zote zinatakiwa zitumie lugha rasmi ambazo ni Kiingereza na Kiswahili na si vinginevyo.
“Ningependa kujua jina la supermarket hii ili meneja wetu wa Kinondoni alifanyie kazi.” Alisema Kayombo.
Bango lililo sehemu ya mbele ya duka hilo |
Juzi, Tanzania PANORAMA Blog iliigundua Supermarket hiyo ikiwa na kibao kinachoitambulisha kwa jina la Tai Le China Supermarket katika eneo la Migombani, Kata ya Mikocheni na inamilikiwa na raia wa China aliyejitambulisha kwa jina moja la Wang.
Katika uchunguzi wake ndani ya supermarket hiyo, Tanzania PANORAMA ilibaini bidhaa zake nyingi zimeandikwa kwa lugha ya kichina pekee na hazijawekewa bei yoyote kwa mnunuzi (price tag) kama ulivyo utaratibu wa kawaida.
Baadhi ya bidhaa hizo ni mayai yenye rangi ya kijani kutoka China na yale yanayozalishwa hapa nchini, maziwa, dawa mbalimbali za mswaki, vinywaji baridi, pombe za aina mbalimbali na vyakula vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyama.
Aidha, uchunguzi ulibaini risiti za kielekitroniki zinazotolewa na supermarket hiyo zinaandikwa kichina isipokuwa bei ya jumla ya bidhaa inayouzwa ndiyo inaandikwa kwa Lugha ya Kiswahili.
Meneja wa Tai Le supermarket, aliyejitambulisha kwa jina moja la Khadija alisema duka hilo ni maalumu kwa ajili ya raia wa China pekee.
Khadija alisema bidhaa nyingi zinazouzwa hapo zinaagizwa kutoka China yakiwemo mayai yenye rangi ya kijani na taratibu zote za usajili na kufanya biashara zimefuatwa ikiwemo kupatiwa vibali kutoka serikalini.
“Hili duka ni kwa ajili ya raia wa China tu, halitoi huduma kwa watanzania. Ukiona mtanzania kaja hapa basi huyo ni mfanyakazi wa ndani katika nyumba za mchina au mtanzania aliyeishi China miaka mingi.
“Kama unasema ulikuwa na shida na bidhaa lakini hujaona bei yake kwanza jua umeingia katika duka ambalo wewe halikuhusu kwa sababu wewe siyo mchina lakini bei za humu haziandikwi kwa sababu wachina wenyewe wanajua bei zao ndiyo maana unaona wanalipa na wanaondoka bila shida.
“Ila kwa faida yako, humu hatuweki bei ya bidhaa kwa sababu katika siku za karibuni bei zinabadilika mara kwa mara, hivyo tunaweza kuweka leo kesho ikatulazimu kubadilisha tena, inakuwa ni usumbufu. Kwa hiyo bidhaa zetu tunauza kwa bei ya siku hiyo na unazipata hapo kaunta unapokwenda kulipia,” alisema Khadija.
Mahali ilipo supermarket ya Tai Le |
Mmiliki wa Supermarket hiyo, Wang yeye alisema duka lake lina msemaji ambaye ni Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mikocheni.
“Mimi siruhusiwi kusema lolote, yupo msemaji wa duka hili. Yeye atakujibu au atakupa kibali uje nacho hapa ndiyo mimi nizungumze. Nenda Ofisi ya Mtendaji wa Kata, hao ndio watawapa majibu, mimi siwezi kuzungumza na ninyi. Serikali Kata ndiyo wanaweza kuwapa kibali cha kufika kwangu, kuingia hapa na kuniuliza. Ni hapo mtaa wa nyuma nendeni mkaongea na hao,” alisema Wang.
Tanzania PANORAMA ambayo ilifika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mikocheni kufuatilia suala hilo na kuelekezwa kuzungumza na Afisa Afya wa Kata ya Mikocheni, Ernest ambaye alikiri kulifahamu duka hilo na kusema kuwa bidhaa zote zinazouzwa hapo ni halali na zina vibali vyote vya mamlaka za serikali vinavyohitajika.
Alisema duka hilo ni maalumu kwa ajili ya raia wa China peke yao na kwamba haliwahusu watanzania.
“Kwanza nashangaa mmefikaje huko na kuanza kufanya ukaguzi, nani amewaruhusu kwenda huko? Sisi ndio tuna mamlaka ya kuwaruhusu kuuliza maswali sio kufika na kuanza kuhoji, hiyo siyo kazi yenu, lazima mpate kibali kutoka hapa.
“Tambua hiyo supermarket ni kwa ajili ya wachina tu, sio kwa ajili ya watanzania na ukiona mtu mweusi hapo basi huyo katumwa na mchina au aliwahi kuishi huko sasa amekwenda kununua bidhaa anazozijua. Watanzania hapo sio kwao,” alisema.
Alisema Mamlaka ya Udhibiti wa Bidhaa (TBS) ndiyo iliyotoa kwa Tai Le kibali cha kuingiza bidhaa zao nchini na kuuza zikiwa zimeandikwa kwa lugha ya kichina bila kulazimiki kuandika bei na kwamba maafisa wa taasisi za serikali hufanya ukaguzi kila mara.
Akizungumzia zaidi bei kutowekwa kwenye bidhaa alisema wanaopaswa kujibu ni TRA.
“Lakini labda hilo la kuweka bei kwenye bidhaa wanazouza kama inavyohitajika, najua lipo kisheria, sasa hili niseme kwamba siwezi kuliongelea, nenda kawaulize Mamlaka ya Mapato ambao wamewapa kibali na huwa wanakuja kukagua, wanajua kwanini mashine zao za kielektoniki zinaandika kichina, wao ndiyo watakupa ufafanuzi.
Aidha, Ernest alionya kuwa katika eneo la Kata ya Mikocheni waandishi wa habari hawaruhusiwa kufika kufanya kazi bila kupata kibali kutoka kwenye Ofisi ya Kata na kwamba mwandishi anayekiuka hilo anakiuka taratibu zilizowekwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni.
“Wako waandishi waliongia katika eneo la kata yangu na kuanza kuhoji watu bila kupitia ofisini kwangu. Ofisi ile ya mchina ilikuwa na tatizo la wafanyakazi walipofika mimi nilipigiwa simu na mchina akaniambia waandishi wamekuja, mimi nikapiga simu polisi nikaagiza wakawachukue waandishi wale niwakute polisi Oysterbay.
“Na huu utaratibu umewekwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni, Mkuu wa Wilaya aliyekuwepo aliusimamia na huyu aliyepo sasa anausimamia. Lakini sasa kwa sababu nyie mlikuwa mnapita ndiyo mkaingia humo kununua bidhaa basi ni vizuri tuelewane kuwa siku nyingine kama mnataka kufanya lolote mje kwanza mueleze mnachotaka kufanya na mpate kibali ndiyo muendelee,” alisema Ernest.
Tanzania PANORAMA inaendelea kumtafuta Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe ambaye alitajwa na Ernest kufika katika supermarket hiyo mara kwa mara ili azungumzie zuio analodaiwa kulisimamia la waandishi wa habari kutofanya kazi katika Kata ya Mikocheni.