Thursday, May 8, 2025
spot_img

‘SUPERMARKET’ YA WACHINA PEKE YAO DAR ES SALAAM

 

RIPOTA PANORAMA

DUKA kubwa la kuuza mahitaji ya nyumbani (Supermarket) linalotoa huduma kwa raia wa China peke yao limegundulika kuwepo katika Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa  Dar es Salaam.

Tanzania PANORAMA Blog imeigundua Supermarket hiyo leo ikiwa na kibao kinachoitambulisha kwa jina la Tai Le China Supermarket. Ipo eneo la Migombani katika Kata ya Mikocheni na mmilikiwa wake ni raia wa China aliyejitambulisha kwa jina moja la Wang.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog ndani ya Supermarket hiyo ulibaini bidhaa zake nyingi zimeandikwa kwa lugha ya kichina pekee na hazijawekewa bei yoyote kwa mnunuzi (price tag) kama ulivyo utaratibu wa kawaida.

Baadhi ya bidhaa hizo ni mayai kutoka China na yale yanayozalishwa hapa nchini, maziwa, dawa mbalimbali  za mswaki, vinywaji baridi, pombe za aina mbalimbali na vyakula vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyama.

Aidha, uchunguzi ulibaini kuwa risiti za kielekitroniki zinazotolewa na supermarket hiyo zinaandikwa kichina isipokuwa bei ya jumla ya bidhaa inayouzwa inaandikwa kwa Lugha ya Kiswahili.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu utaratibu unaotumiwa na supermarket hiyo kufanya biashara, Meneja wa Tai Le supermarket,  aliyejitambulisha kwa jina la Khadija amesema dula hilo ni maalumu kwa ajili ya raia wa China pekee.

Khadija alisema bidhaa nyingi zinazouzwa hapo zinaagizwa kutoka China yakiwemo mayai yenye rangi ya kijani na taratibu zote za usajili na kufanya biashara zimefuatwa ikiwemo kupatiwa vibali kutoka serikalini.

“Hili duka ni kwa ajili ya raia wa China tu, halitoi huduma kwa watanzania. Ukiona Mtanzania kaja hapa basi huyo ni mfanyakazi wa ndani katika nyumba za mchina au Mtanzania aliyeishi China miaka mingi. 


 

“Kama unasema ulikuwa na shida na bidhaa lakini hujaona bei yake kwanza jua umeingia katika duka ambalo wewe halikuhusu kwa sababu wewe siyo mchina lakini bei za humu haziandikwi kwa sababu wachina wenyewe wanajua bei zao ndiyo maana unaona wanalipa na wanaondoka bila shida.

“Ila kwa faida yako, humu hatuweki bei ya bidhaa kwa sababu katika siku za karibuni bei zinabadilika mara kwa mara, hivyo tunaweza kuweka leo kesho ikatulazimu kubadilisha tena, inakuwa ni usumbufu. Kwa hiyo bidhaa zetu tunauza kwa bei ya siku hiyo na unazipata hapo kaunta unapokwenda kulipia,” alisema Khadija.

Mmiliki wa Supermarket hiyo, Wang ambaye anazungumza vizuri lugha ya kiswahili alipoulizwa kuhusiana na bidhaa za duka hilo kutowekwa bei na nyingi kuandikwa lugha ya kichina, alisema duka lake lina msemaji wake ambaye ni Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mikocheni.

“Mimi siruhusiwi kusema lolote, yupo msemaji wa duka hili. Yeye atakujibu au atakupa kibali uje nacho hapa ndiyo mimi nizungumze. Nenda Ofisi ya Mtendaji wa Kata, hao ndio watawapa majibu, mimi siwezi kuzungumza na ninyi. Serikali Kata ndiyo wanaweza kuwapa kibali cha kufika kwangu, kuingia hapa na kuniuliza. Ni hapo mtaa wa nyuma nendeni mkaongea na hao,” alisema Wang.

Tanzania PANORAMA Blog imefika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mikocheni kufuatilia suala hilo ambapo ilielekezwa kuzungumza na Afisa Afya wa Kata ya Mikocheni, Fredy Ernest.

Ernest alikiri kulifahamu duka hilo na kusema kuwa bidhaa zote zinazouzwa hapo ni halali na zina vibali vyote vya mamlaka za serikali vinavyohitajika.

Alisema duka hilo ni maalumu kwa ajili ya raia wa China peke yao na kwamba haliwahusu watanzania.

“Kwanza nashangaa mmefikaje huko na kuanza kufanya ukaguzi, nani amewaruhusu kwenda huko? Sisi ndio tuna mamlaka ya kuwaruhusu kuuliza maswali sio kufika na kuanza kuhoji, hiyo  siyo kazi yenu, lazima mpate kibali kutoka hapa,” alihoji.

“Tambua hiyo supermarket ni kwa ajili ya Wachina tu, sio kwa ajili ya Watanzania na ukiona mtu mweusi hapo basi huyo katumwa na Mchina au aliwahi kuishi huko sasa amekwenda kununua bidhaa anazozijua. Watanzania hapo sio kwao,” amesema.

Ernest amesema Mamlaka ya Udhibiti wa Bidhaa (TBS) ndiyo iliyowapatia Tai Le kibali cha kuingiza bidhaa zao nchini na kuwaruhusu kuuza zikiwa zimeandikwa kwa lugha ya kichina tu na kwamba hawalazimiki kuandika bei katika bidhaa zao.

“Kama ingekuwa ni kosa bidhaa hizo kuwa na lugha hiyo wasingeruhusiwa na TBS kuziingiza nchini na kuziuza kwenye maduka yao, kila kinachouzwa humo kimeruhusiwa na serikali ikiwa ni pamoja na nyama ya ng’ombe na mbuzi kutoka nchini kwao ambayo mmeona inauzwa humo.

“Lakini labda hilo la kuweka bei kwenye bidhaa wanazouza kama inavyohitajika, najua lipo kisheria, sasa hili niseme kwamba siwezi kuliongelea, nenda kawaulize Mamlaka ya Mapato ambao wamewapa kibali na huwa wanakuja kukagua, wanajua kwanini mashine zao za kielektoniki zinaandika kichina, wao ndiyo watakupa ufafanuzi.

Aidha, Ernest alionya kuwa katika eneo la Kata ya Mikocheni waandishi wa habari hawaruhusiwa kufika kufanya kazi bila kupata kibali kutoka kwenye Ofisi ya Kata na kwamba mwandishi anayekiuka hilo anakiuka taratibu zilizowekwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni.

“Wako waandishi waliongia katika eneo la kata yangu na kuanza kuhoji watu bila kupitia ofisini kwangu. Ofisi ile ya mchina ilikuwa na tatizo la wafanyakazi walipofika mimi nilipigiwa simu na mchina akaniambia waandishi wamekuja, mimi nikapiga simu polisi nikaagiza wakawachukue waandishi wale niwakute polisi Oysterbay.

“Na huu utaratibu umewekwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni, Mkuu wa Wilaya aliyekuwepo aliusimamia na huyu aliyepo sasa anausimamia. Lakini sasa kwa sababu nyie mlikuwa mnapita ndiyo mkaingia humo kununua bidhaa basi ni vizuri tuelewane kuwa siku nyingine kama mnataka kufanya lolote mje kwanza mueleze mnachotaka kufanya na mpate kibali ndiyo muendelee,” alisema Ernest.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi Mkuu wa TBS na Kamishna Mkuu wa TRA kuzungumzia suala hili bado zinaendelea.


 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya